Majuma mawili tangu Umoja wa Vijana wa Chama cha
NCCR-Mageuzi umtake, Dk George Kahangwa (46) kugombea urais, mhadhiri
huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema ameridhia wito huo.
Machi 8, mwaka huu Kitengo cha Vijana cha NCCR - Mageuzi kilimpendekeza Dk Kahangwa kugombea nafasi hiyo kwa kuwa kimeridhishwa na utendaji wake wa kazi, ujana na ucha Mungu wake.
Machi 8, mwaka huu Kitengo cha Vijana cha NCCR - Mageuzi kilimpendekeza Dk Kahangwa kugombea nafasi hiyo kwa kuwa kimeridhishwa na utendaji wake wa kazi, ujana na ucha Mungu wake.
Akizungumzia mapendekezo hayo mwishoni mwa wiki,
Dk Kahangwa alisema: “Mwanzoni yalikuwa mapendekezo tu ya vijana na
mpaka sasa nilikuwa sijatoa kauli rasmi, lakini baada ya kupata ushauri
na kutafakari, nimeona sina kikwazo katika jambo hilo.” Msomi huyo wa masuala ya elimu, alisema
inawezekana akasita kwa kuwa jukumu hilo ni kubwa lakini uungwaji mkono
na hamasa anayopata na kauli wanazomwambia zinaonyesha inawezekana na
wanamwamini.
Vipaumbele vyake
Alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kuzalisha
rasilimali watu bora, elimu isiyo na ubaguzi, uchumi wa ushirika
mamboleo utakaosisitiza kujitegemea na afya bora wakati wote. Pia, ujenzi wa miundombinu ya kuleta maendeleo kwa
kasi, demokrasia huru na ya kweli, umoja wa kitaifa na michezo ambayo
siyo tu itailetea sifa Tanzania, bali kutoa ajira kwa vijana.
Alipoulizwa anaionaje changamoto ya uteuzi wa
wagombea ndani ya Ukawa, Dk Kahangwa alisema umoja huo utadumu iwapo
wataweka mbele masilahi ya Taifa na wananchi badala ya ubinafsi. “Tunatambua kugombea ni kushindana lakini
tutangulize masilahi ya Taifa, masilahi ya wananchi kabla ya masilahi ya
chama kimoja ndani ya Ukawa,” alisema.
Sitishwi na umaarufu
Dk Kahangwa alipuuza madai kwamba umaarufu wake ni
mdogo na hivyo atakuwa na wakati mgumu kupambana na wagombea wengine wa
Ukawa na CCM ambao ama wametajwa au kujitangaza wenyewe kuwania urais. “Umaarufu una sura nyingi; wapo wanaojulikana kwa
mambo ya hasara ambayo hayana msaada kwa Taifa. Unaweza usiwe na jina
maarufu lakini una sifa za uongozi na uadilifu, kwa hiyo sina hofu
kupambanishwa na mgombea mwingine yeyote ndani na nje ya Ukawa,”
alisema.
Alitolea mfano wa Rais, Benjamin Mkapa na Rais wa Zanzibar, Dk
Ali Mohammed Shein kuwa ni miongoni mwa watu ambao hawakuwa maarufu,
lakini walishinda uchaguzi.
Msimamo wa NCCR- Mageuzi
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema amefarijika kusikia Dk Kahangwa amekubali kuwania nafasi hiyo
akimtaja kuwa ni miongoni mwa makada ambao ni nguzo ya chama hicho. “Dk Kahangwa hatujamwokota barabarani, ni mtu
tunayemfahamu, kumheshimu na kuthamini mchango wake ndani ya chama na
yeye anakijua chama hiki vizuri,” alisema Nyambabe.
Alipoulizwa anamlinganishaje Dk Kahangwa na
wagombea wengine kutoka vyama vinavyounda Ukawa na CCM, alisema: “Mimi
namtia moyo kwa sababu hata nikimlinganisha na wagombea wengine naona
anafaa zaidi. Kama hoja ya urais ni ujana, huyu ni kijana mwenzao na
kama hoja ni kwenda na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, huyu ni
msomi aliyebobea.”
Alitoa wito kwa makada wengine wa NCCR-Mageuzi
kujitokeza kuchukua fomu ili kuleta ushindani wenye tija ndani ya chama
hicho. Dk Kahangwa ana Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) katika
masuala ya elimu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment