Pages

Wednesday, March 25, 2015

MAFURIKO YAKOSESHA MAKAZI MAELFU DAR

Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali kwa waathirika wa mafuriko eneo la Buguruni Kwa Mnyamani, jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea eneo hilo jana.Zaidi ya wakazi  5,000 wa Buguruni kwa Mnyamani, jijini Dar es Salaam hawana makazi kutokana na nyumba zao zaidi ya 500 kujaa maji. Idadi hiyo ilijulikana jana baada ya Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal, kutembelea eneo hilo lililoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo.
Dk. Bilal ambaye  aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, alisema serikali iko tayari kuwasaidia wakazi hao na kuahidi  kupeleka haraka kikosi cha maafa kutoka Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kushughulikia tatizo hilo. Pamoja na kuwapa pole kwa kukumbwa na adha hiyo, Dk. Bilal aliahidi pia kwamba serikali itapeleka dawa kwa ajili ya kupuliza katika maji hayo ambayo yametuama.
Alisema kwa kuwa maji hayo  ni machafu ni rahisi  wakazi hao kupatwa na magonjwa.
 
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, naye jana alitembelea maeneo hayo yaliyokumbwa na mafuriko na kusema serikali ipo tayari kuwasaidia waathirika ikiwa watahitaji msaada. “Serikali tuko tayari kuwasaidia wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani  tena haraka endapo watasema wanahitaji msaada, kwa sababu tukio lao halina uhusiano na lile la wakazi wa mabondeni ambao tumepiga kelele sana kuhusu kuhama, lakini bado wanaendelea kukaidi,”  alisema na kuongeza: “Eneo la Buguruni halina historia ya mafuriko isipokuwa eneo lao kujaa maji kumesababishwa na kuziba kwa bomba la kupitisha maji, hivyo maji kupoteza mwelekeo na kusambaa katika makazi. Mpaka sasa uongozi wa mtaa haujatueleza matatizo yao, lakini wakisema wanahitaji tuko tayari kuwasaidia.”
Kadhalika, alisisitiza kuwa, serikali haitawajibika kwa kuwasaidia wakazi wa mabondeni ambao wameendelea kukaidi agizo la serikali la kuhama katika maeneo hayo. “Serikali tumesisitiza sana kuhusu wakazi wa mabondeni kuhama, lakini wameendelea kukaidi. Ni lazima watambue kwamba serikali haitawajibika kwa lolote endapo yatatokea maafa mengine kwa wakazi hao kwa sababu tumepiga makelele sana na wale wastaarabu wamekwisha hama. Kama yatatokea maafa wakaumia tutawatibu kama ajali lakini sio msaada mwingine,” alisema.
Kuhusiana na jitihada za kuondoa maji Buguruni Mnyamani, Sadiki alisema tayari wameomba msaada kutoka kwa kampuni ya Wachina ya Railway Jianchang Engineering (CRJE) kusaidia kunyonya maji hayo. Pia alisema wameagiza mipira mingine ya kutolea maji hayo baada ya iliyokuwapo  kuzidiwa  nguvu.
Akizungumzia idadi ya watu waliokufa mpaka sasa,  Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema waliokufa kutokana na athari za mvua ni watu watano na kwamba watu wawili waliokufa kwa kuangukiwa na nguzo, Kimara Baruti ilikuwa ni ajali ya kawaida. “Idadi ya waliokufa kutokana na athari za mvua hadi sasa ni watano na wale waliokufa juzi huko Kimara haikusababishwa na mvua isipokuwa kuna mtu aligonga nguzo ya umeme na katika  harakati za kutaka kuwakimbia polisi aliita ndugu zake wamsaidie kutoa gari lake ndipo walipigwa na shoti ambayo ilikuwa imesambaa kwenye maji,” alisema Kova.
Kova alisema bado Jeshi la Polisi linaendelea na doria katika eneo lote la jiji kwa kushirikiana na Shirika  la Umeme Tanzania (Tanesco), pamoja na Kikosi cha Zima Moto.
 
LIPUMBA ATOA POLE
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, ni miongoni mwa viongozi waliokwenda kuwatembelea waathirika hao na kutoa msaada wa Sh. 500,000. Prof. Lipumba alisema ilitakiwa kutatua tatizo hilo mapema hata kabla ya kutokea kwa sababu lilikuwa linajulikana  hata katika serikali ya mtaa.
Alisema majanga mengi nchini yanatokea kutokana na uzembe wa uwajibikaji kuanzia serikali za mtaa hadi serikali kuu na kwamba ikiwa kila moja kwa upande wake ingekuwa inawajibika ipasavyo matatizo kama hayo yasingekuwa yanatokea. Alisema anasikitishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali kwa wakazi hao ambao mpaka sasa hawana chakula wala mahali pa kulala.
“Sifurahishwi na hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwasaidia waathirika hawa, wamepata matatizo ni siku ya tatu sasa, watu hawana mahali pa kulala, watoto na wanawake wanahangaika, lakini serikali haijahangaika kufahamu wanaishije,” alisema Prof. Lipumba. Aliongeza: “Ni vema serikali ikaleta msaada wa haraka kuwasaidia waathirika hawa, ikiwamo kuleta kikosi cha maafa kutoa msaada wa haraka.”
 
MWENYEKITI WA MAAFA
Mwenyekiti wa Maafa wa mtaa huo, Ahmad Abdulfaris, alisema wanashangaa hadi sasa hawajapatiwa msaada wowote wa kuhakikisha maji hayo yanaondolewa japokuwa waliahidiwa kusaidiwa  na ofisi ya mkuu wa mkoa tangu Machi 20 yalipotokea. “Mkuu wa mkoa alikuja akasema wanaleta vifaa ambavyo vitaondoa maji hayo, wameleta havijafanya kazi ikabidi waondoke na hadi sasa wanakuja wanaondoka hawafanyi kazi yeyote, kwa kifupi hatujaona jitihada za dhati za kushughulikia tatizo hili,” alisema.
Mpaka sasa watu watano wameshafariki kutokana na athari za mvua zilizoanza kunyesha Machi 20, mwaka huu, mmoja akiangukiwa na nyumba, mwingine kusombwa na maji hadi mto Mbezi na wengine watatu wakiangukiwa na nguzo za umeme. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agness  Kijazi, akizungumza juzi na NIPASHE,  alisema mvua hizo zitaendelea kunyesha kwa mfululizo kuanzia jana, leo na kesho.
Alisema mvua hizo zitanyesha katika ukanda wote wa Pwani, Tanga, Mtwara, Dar es Salaam, Lindi, Visiwa vya Unguja na Pemba. Alisema mvua hizo zitanyesha kwa saa 24 kwa ukubwa wa milimita zinazozidi 50. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment