
Mkuu wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Itimila mkoani
Simiyu, kimelitaka Jeshi la Polisi kusitisha msako wa waganga wa jadi
wanaopiga ramli chonganishi.
Hatua hiyo imekuja huku Jeshi la Polisi katika Mikoa ya Kanda ya
Ziwa, likiwa katika msako mkali wa kuwakamata waganga wa namna hiyo. Mbali ya kulitaka jeshi hilo kusitisha shughuli hiyo, pia CCM
imetaka waganga hao wa jadi wapewe muda wa kutosha ili wapatiwe leseni
za kutambulika kwa kazi zao.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Mohamoud
Mabula, wakati wa mkutano wa waganga wa jadi uliofanyikia katika viwanja
vya Shule ya Sekondari Lagangabilili wilayani humo mwishoni mwa wiki. Mabula alimtaka Mkuu wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo,
aliyehudhuria mkutano huo, kusitisha shughuli hiyo kwa maelezo kwamba
baadhi ya waganga hao wa jadi wamekamatwa kutokana na kukosa leseni
lakini hawajihusishi na upigaji wa ramli.
Hata hivyo, alisema anatambua umuhimu wa agizo la Rais Jakaya
Kikwete, lakini kuhusu uendeshaji wa operesheni hiyo anaipinga kutokana
na waganga wengi kutopewa muda wa kujiandikisha ili kupatiwa leseni. "Operesheni hii inataka kutukumbusha operesheni kimbunga kwa
wahamiaji haramu na kukamata majangili. Operesheni hizi zimeondoka na
viongozi wengi wachapakazi, sasa hatutaki Chama kurudia makosa. Tunataka
operesheini zifanyike kwa amani na siyo kuwashtukiza watu,” alisisitiza
Mabula.
Alieleza kuwa maagizo ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wao
ngazi za juu kwa upande wa serikali, huwaweka katika wakati mgumu
viongozi wa Chama ngazi za mkoa na wilaya kutokana na maagizo hayo
kutekelezwa kwa nguvu. “Sisi kama Chama, tumeanza kupata malalamiko kutoka kwa wapigakura
wetu. Wanasema CCM inataka kuwafukuza waganga wa jadi…kwa hili
hatukubali tulalamikiwe tunachohitaji msako ufanyike lakini kwa amani na
watafutwe wapiga ramli tu na siyo waganga wote,” alisema.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo wa CCM, ilipokewa kwa shangwe na waganga wa jadi zaidi ya 200 waliohudhuria mkutano huo. "Niko tayari kwenda jela kwa niaba ya waganga katika wilaya hiyo ikiwa operesheni hiyo haitasitishwa," aliongeza Mabula. Aidha, alisema atapambana hadi ngazi za juu kuhakikisha kwamba
waganga wanaofanya kazi yao kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni za
nchi, hawaonewi kwa kisingizio cha kupiga ramli chonganishi.
RPC ATII AMRI
Baada ya kauli hiyo ya CCM, Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu,
Mkumbo, alisimama na kutangaza kuwa operesheni hiyo imesitishwa katika
Wilaya ya Itimila. Aidha, Kamanda Mkumbo alitoa mwezi mmoja kwa kila mganga kuhakikisha anapatiwa leseni.
Hata hivyo, alisema baada ya muda huo kumalizika, operesheni hiyo itaendelea. “Tumesitisha operesheni hii kama alivyosema Mwenyekiti na tunatoa mwezi mmoja...lakini baada ya muda huo, tutaanza msako.
Ninachowaomba waganga nyote nendeni kwa viongozi wenu mkajiandikishe ili taratibu za leseni zifanyike," alisema Kamanda Mkumbo.
SHIMAUTITA WAUNGA MKONO MSAKO
Hata hivyo, Shirika la Maendeleo la Utafiti Tiba Asili Tanzania
(Shimautita), limeungana na serikali kutaka operesheni ya kuwatafuta
wapiga ramli chonganishi wasakwe. Katibu Mkuu wa shirika hilo, Dk. Aaron Machokosi, alisema kuwa
kutokana na hali ilivyo hivi sasa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na
vikongwe, operesheni hiyo imekuja wakati mwafaka. “Tunaipongeza serikali kwa uamuzi wake huo. Ni lazima waganga wa
jadi kufuata misingi ya sheria na kanuni za nchi tunachowataka waganga
wote nchi nzima wajiandikishe katika sehemu husika ili kupata leseni,”
alisema Machokosi.
Aidha, Machokosi alimshangaa Mwenyekiti wa CCM kuagiza kusitishwa
kwa zoezi hilo ikiwa ni pamoja na Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, kutii
amri hiyo. Alisema agizo hilo lilitolewa na Kiongozi wa nchi, hivyo linatakiwa kufanyiwa kazi bila ya mzaha.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment