Pages

Saturday, January 17, 2015

WAGOMBEA URAIS WASIKWEPE MIDAHALO

Kamera 
Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam (Udasa) juzi ilitangaza mpango wake wa kuendesha midahalo ya wagombea urais wakati wa kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba.
Jumuiya hiyo ilisema kuwa imeandaa midahalo hiyo kwa kushirikiana na kituo cha televisheni cha ITV ili kuwawezesha wananchi wote kufuatilia hoja za wagombea wa nafasi hiyo nyeti za kutetea ilani, sera, na mikakati ya vyama vyao kuendeleza nchi. Kwa mujibu wa Udasa, midahalo hiyo itawawezesha wagombea kueleza falsafa, sera na mikakati yao ya kutatua matatizo yanayoikabili nchi, huku pia ikiwapa wananchi fursa ya kuwajua kwa undani watu wanaotaka kupewa dhamana hiyo kubwa ya kuongoza nchi.
Midahalo hiyo pia itakuwa ni fursa nzuri kwa vyama kuelezea ilani zao, sera na mikakati ya kuendeleza uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Tunapenda kuunga mkono uamuzi wa wasomi hao wa kufanya kitu hicho muhimu katika Uchaguzi Mkuu ambao kwa kawaida huamua mustakabali wa nchi. Hoja zilizotolewa na Udasa kuhusu umuhimu wa midahalo zinajitosheleza kwa kuwa wananchi wana haki ya kuwajua wagombea kwa undani ili wafanye uamuzi sahihi wa kumpigia kura mgombea.
Kwa mara ya kwanza na ya mwisho, mdahalo wa wagombea urais ulifanyika mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, lakini tangu wakati huo wagombea wamekuwa wakiikwepa na hata kuibeza. Mwaka 2010, kituo cha televisheni cha TBC1 kinachomilikiwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kilianzisha mdahalo kwa wagombea ubunge, lakini ghafla midahalo hiyo ikafutwa, huku chama tawala, CCM kikizuia wanachama wake kushiriki.
Uamuzi kama huo ni wa kuwanyima fursa wapigakura kuwajua wagombea na kuwapima na pia kuwanyima fursa wagombea kuelezea sera na mikakati yao huku wakisikiliza changamoto kutoka kwa wapinzani wao. Ili uchaguzi uwe huru na haki, ni lazima wapigakura wawaelewe vizuri wagombea wao, sera na ilani za vyama vyao ili wanapofanya uamuzi wa kumchagua mgombea mmoja, wafanye kwa usahihi badala ya kufanya kwa kubahatisha na hivyo kupata viongozi ambao hawajui vizuri matatizo ya wananchi na hawajui watayatatuaje.
Tunapenda kushauri wagombea watakaopitishwa na vyama vyao, kutokwepa midahalo hiyo ambayo hutoa pia fursa kwa wapigakura kuuliza maswali ili waweze kuwajua vizuri wanaoutaka urais na kuwapima kabla ya kupiga kura. Vyama navyo havina budi kutoa ushirikiano kwa Udasa kufanikisha azma hiyo kwa kuruhusu wagombea watakaopitishwa, kushiriki kwenye midahalo hiyo muhimu katika kukamilisha dhana nzima ya demokrasia kwenye Uchaguzi Mkuu.
Mtu ambaye amepitishwa na chama kugombea urais, ni yule ambaye ameaminika kuwa ana uwezo wa kutekeleza sera za chama chake katika kuiendeleza nchi, kushughulikia matatizo ya wananchi, na pia ni mtu mtu msafi, mwadilifu, muwazi, na mzalendo. Wale wasio na sifa hizo ndiyo rahisi kukimbia mdahalo kuhofia uwezo wao mdogo kuwa bayana na pia uovu wao kuanikwa. Kwa maana hiyo mtu huyo hafai hata kugombea urais. Matumaini yetu ni kuwa wale wote watakaopitishwa wana uwezo na sifa hizo na hawahofii uovu wao kuanikwa kwenye midahalo kwa kuwa ni wasafi, waadilifu na wazalendo na hivyo wataitikia wito wa Udasa wakati wowote watakapoombwa kushiriki midahalo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment