
Kamera
Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salam (Udasa) juzi ilitangaza mpango wake wa kuendesha midahalo ya
wagombea urais wakati wa kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopangwa
kufanyika mwezi Oktoba.
Jumuiya hiyo ilisema kuwa imeandaa midahalo hiyo
kwa kushirikiana na kituo cha televisheni cha ITV ili kuwawezesha
wananchi wote kufuatilia hoja za wagombea wa nafasi hiyo nyeti za
kutetea ilani, sera, na mikakati ya vyama vyao kuendeleza nchi. Kwa mujibu wa Udasa, midahalo hiyo itawawezesha
wagombea kueleza falsafa, sera na mikakati yao ya kutatua matatizo
yanayoikabili nchi, huku pia ikiwapa wananchi fursa ya kuwajua kwa
undani watu wanaotaka kupewa dhamana hiyo kubwa ya kuongoza nchi.
Midahalo hiyo pia itakuwa ni fursa nzuri kwa vyama
kuelezea ilani zao, sera na mikakati ya kuendeleza uchumi wa nchi na
maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Tunapenda kuunga mkono uamuzi wa wasomi hao wa
kufanya kitu hicho muhimu katika Uchaguzi Mkuu ambao kwa kawaida huamua
mustakabali wa nchi. Hoja zilizotolewa na Udasa kuhusu umuhimu wa
midahalo zinajitosheleza kwa kuwa wananchi wana haki ya kuwajua wagombea
kwa undani ili wafanye uamuzi sahihi wa kumpigia kura mgombea.
Kwa mara ya kwanza na ya mwisho, mdahalo wa
wagombea urais ulifanyika mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa
vyama vingi, lakini tangu wakati huo wagombea wamekuwa wakiikwepa na
hata kuibeza. Mwaka 2010, kituo cha televisheni cha TBC1
kinachomilikiwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kilianzisha
mdahalo kwa wagombea ubunge, lakini ghafla midahalo hiyo ikafutwa, huku
chama tawala, CCM kikizuia wanachama wake kushiriki.
Uamuzi kama huo ni wa kuwanyima fursa wapigakura
kuwajua wagombea na kuwapima na pia kuwanyima fursa wagombea kuelezea
sera na mikakati yao huku wakisikiliza changamoto kutoka kwa wapinzani
wao. Ili uchaguzi uwe huru na haki, ni lazima wapigakura wawaelewe
vizuri wagombea wao, sera na ilani za vyama vyao ili wanapofanya uamuzi
wa kumchagua mgombea mmoja, wafanye kwa usahihi badala ya kufanya kwa
kubahatisha na hivyo kupata viongozi ambao hawajui vizuri matatizo ya
wananchi na hawajui watayatatuaje.
Tunapenda kushauri wagombea watakaopitishwa na
vyama vyao, kutokwepa midahalo hiyo ambayo hutoa pia fursa kwa
wapigakura kuuliza maswali ili waweze kuwajua vizuri wanaoutaka urais na
kuwapima kabla ya kupiga kura. Vyama navyo havina budi kutoa ushirikiano kwa
Udasa kufanikisha azma hiyo kwa kuruhusu wagombea watakaopitishwa,
kushiriki kwenye midahalo hiyo muhimu katika kukamilisha dhana nzima ya
demokrasia kwenye Uchaguzi Mkuu.
Mtu ambaye amepitishwa na chama kugombea urais, ni
yule ambaye ameaminika kuwa ana uwezo wa kutekeleza sera za chama chake
katika kuiendeleza nchi, kushughulikia matatizo ya wananchi, na pia ni
mtu mtu msafi, mwadilifu, muwazi, na mzalendo. Wale wasio na sifa hizo ndiyo rahisi kukimbia
mdahalo kuhofia uwezo wao mdogo kuwa bayana na pia uovu wao kuanikwa.
Kwa maana hiyo mtu huyo hafai hata kugombea urais. Matumaini yetu ni kuwa wale wote watakaopitishwa wana uwezo na sifa hizo
na hawahofii uovu wao kuanikwa kwenye midahalo kwa kuwa ni wasafi,
waadilifu na wazalendo na hivyo wataitikia wito wa Udasa wakati wowote
watakapoombwa kushiriki midahalo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment