
Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile (kushoto) na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDASA), Prof. Kitila Mkumbo wakikabidhiana nyaraka za makubaliano ya
kuandaa midahalo kwa wagombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Katikati ni Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na
Mawasiliano, Dk Ayoub Rioba.
Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) na ITV/ Radio One wamesaini makubaliano
ya kuandaa midahalo ya wagombea wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba
mwaka huu.
Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo
jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Udasa, Profesa Kitila Mkumbo alisema
katika nchi za kidemokrasia midahalo hufanikisha uchaguzi ulio huru,
haki na wazi.
Pia, alisema midahalo hiyo hutoa fursa muhimu kwa
wagombea kueleza falsafa, sera na mikakati yao ya kutatua matatizo
mbalimbali yanayowakabili wananchi.
Hata hivyo, Profesa Mkumbo alisema midahalo
watakayoendesha haitaegemea chama chochote na kwamba mgombea
atakayekataa kushiriki hawamlazimishi.
“Hatutakuwa na uwezo wa kumlazimisha mgombea, nchi hii ina historia ya wagombea kukimbia midahalo,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema muda rasmi wa kuanza kwa midahalo hiyo
utatangazwa baadaye, wananchi wajue kuwa kupitia matangazo hayo wapiga
kura watajua weledi na umahiri wa wagombea na vyama vyao.
“Tafiti zinaonyesha kuwa midahalo ya wagombea
urais ina nafasi ya kipekee katika kuwawezesha wapiga kura kuamua
mgombea gani wamchague,” alisema.
Alisema kuwa vyama vyote vitakavyoshiriki katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na ambavyo vitasimamisha wagombea wa urais
vitaalikwa kushiriki katika midahalo hiyo.
Pia wagombea wote watakaojitokeza kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu wataalikwa kushiriki mdahalo huo. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na
Radio One, Joyce Mhavile alisema midahalo hiyo itaaminiwa na wananchi
kwa sababu wanaoandaa hawagombei nafasi yoyote katika uchaguzi huo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment