
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe,
ametahadharisha kuongezeka kwa mitandao ya uhalifu wa kimataifa na
ugaidi, akisema kama haitadhibitiwa mapema na vyombo vya dola, inaweza
kujipenyeza katika sekta mbalimbali ikiwamo kufadhili watafuta uongozi
wa nchi.
Pia, amelitaka Jeshi la Polisi nchini kupanga mikakati thabiti ya
kuhakikisha amani na utulivu uliopo nchini unaendelea kuimarishwa hasa
wakati wa kampeni na upigaji kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa. Alitoa tahadhari hiyo jana mjini hapa alipokuwa akifungua mkutano Mkuu wa mwaka wa maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi nchini.
Alisema uhalifu wa kimataifa hutumia fedha chafu zinazopatikana kwa
njia haramu na kuwa ni hatari kwa usalama wa taifa kutokana na kwamba
kutokana na uwezo mkubwa wa kifedha wa mitandao hiyo, ni rahisi kujipenyeza hata katika uongozi. “Hawa watafuta uongozi kwa kutumia fedha zao ili kujiwekea kinga na
kujenga misingi ya kuendeleza uhalifu wao, ni hali inayohatarisha
utawala wa sheria, mfumo wa demokrasia na upatikanaji wa haki nchini,”
alisema Chikawe.
Alilitaka Jeshi hilo kutovumilia watumishi wa aina hiyo na lisisite
kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria mtumishi atakayejiingiza
katika ushirikiano na mitandao hiyo hiyo ambayo inahatarisha amani na
usalama wa nchi. Kuhusu kuibuka kwa makundi ya kihalifu kama vile ‘Panya road’,
Chikawe alisema hali hiyo haikubaliki na kulitaka Jeshi hilo kutimiza
wajibu badala ya kusubiri matukio yatokee. “Wananchi wa Dar es Salaam
wanahoji inakuwaje baada ya taharuki ya ‘Panya road’ Jeshi la Polisi
linakamata watu zaidi ya 1200?Je Jeshi la polisi lilikuwa linawafahamu
kabla...Wananchi wanalituhumu Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam kuwa baada ya kuwakamata vijana wengi lilifanya mradi kwa kauli
ya kuwa kuingia bure kutoka kwa pesa,” alisema bila kufafanua.
Alibainisha kama malalamiko hayo ni ya kweli baadhi ya askari
wasiowaaminifu wametumia fursa hiyo kujinufaisha na kuwanyanyasa
wananchi. Aliaagiza hatua stahiki zichukuliwe endapo ikithibitika kuwa kuna ukiukwaji wa maadili mema ya Jeshi la polisi.
Kuhusu kuvamiwa kwa kituo cha Polisi Ikwiriri, mkoani Pwani,
Chikawe alisema serikali imesikitishwa sana na tukio hilo na IGP
amemhakikishia polisi hawatalala mpaka watuhumiwa wote waliofanya unyama
huo wapatikane na kufikishwa katika mkono wa sheria.
Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu, alisema pamoja na mambo
mengine Jeshi la Polisi inaweka mkakati kwa kushirikiana na vyama vya
siasa, Msajili wa vyama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kudhibiti
matukio ya uvunjifu wa amani katika uchaguzi mkuu ujao na upigaji kura
ya maoni ya Katiba.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment