Mwenyekiti Mpya wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa
(kushoto) akipongezana na Makamu wake, Jerome Bwanausi baada ya wajumbe
wa kamati hiyo kuwachagua kuwa viongozi wa kamati hiyo katika uchaguzi
uliofanyika Dodoma jana.
Kamati tatu za Bunge
ambazo wenyeviti wake walitakiwa kuwajibika kutokana na kashfa ya
Akaunti ya Tegeta Escrow, zimeanza kuchagua wenyeviti wapya huku ile na
Nishati na Madini ikimchagua Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa kuwa
mwenyekiti wake.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya vuta nikuvute
tangu vilipoanza vikao vya kamati hizo, Januari 13 mwaka huu kutokana
na wajumbe wake kugoma kufanya uchaguzi kwa maelezo kuwa hawajapewa
mwongozo kutoka ofisi ya Spika.
Hata hivyo, Januari 23 Spika wa Bunge, Anne
Makinda alizitaka kamati hizo za Nishati na Madini, Bajeti na Katiba,
Sheria na Utawala kufanya uchaguzi kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa
Bunge, kama linavyosema azimio la tatu la Bunge kuhusu kashfa ya escrow.
Katika Azimio lake la tatu kuhusu kashfa hiyo,
kati ya maazimio manane, Bunge liliazimia: “Kamati husika za Kudumu za
Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa
18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za
kudumu za Bunge.”
Ndassa amechukua nafasi ya Victor Mwambalaswa aliyejiuzulu kutokana na azimio hilo la Bunge.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo
zinaeleza kuwa nafasi ya makamu mwenyekiti imebaki kwa Jerome Bwanausi
ambaye ni Mbunge wa Lulindi.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kamati hiyo imefanya uchaguzi na kumchagua Ndassa kama mwenyekiti wao.
Alisema kuwa kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na ile ya Bajeti zitafanya uchaguzi kama ilivyoelekezwa.
Akizungumzia kuchaguliwa kwake, Ndassa alisema
kamati hiyo ina mambo mengi na inasimamia wizara ambayo mawaziri na
makatibu wakuu wengi wamekuwa wakiondolewa. ”Tutasimamia mikataba ya mafuta na gesi na kutaka
iwe wazi, pia zabuni za utafutaji gesi na mafuta si vibaya wazawa nao
wakahusishwa,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment