Shahidi wa kwanza katika kesi inayomkabili Katibu wa
Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, (pichani)
aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Morogoro, Sadick Tindwa, amedai kuwa
alitoa kibali cha kufanya kongamano kwa sharti la kutokashfu dini
nyingine.
Akiongozwa na wakili wa Serikali, Benard Kongola Tindwa, alidai
kuwa Julai 31, mwaka 2013, akiwa OCD Wilaya ya Morogoro alipokea barua
kutoka kwa Umoja wa Wahadhiri wa dini ya Kiislamu, wakiomba kufanya
kongamano la siku kuu ya Iddi pili katika uwanja wa Shule ya Msingi
Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro Agosti 9, 2013.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mery
Moyo, Tindwa ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Handeni,
alidai siku ya kongamano akiwa na maafisa wengine wa polisi waliimarisha
ulinzi na kuangalia kama masharti yaliyoelezwa katika kibali hicho
yanafuatwa.
Shahidi huyo alitoa ushahidi wake kwa zaidi ya saa mbili na wakati
wote huo, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika viwanja vya
mahakama hiyo na kuwadhibiti wafuasi wa Sheikh Ponda, ambao walizuiwa
nje ya uzio. Alidai kuwa wahadhiri mbalimbali walitoa mada katika kongamano
hilo na msemaji wa mwisho alikuwa ni Ponda, ambaye alitoa maneno yenye
mtazamo ya uchochezi, kashfa na kuumiza imani za dini nyingine kinyume
cha kibali kilichotolewa.
Tindwa alinukuu maneno aliyozungumza Sheikh Ponda katika kongamano
hilo kuwa ni “Waislamu wenzangu tuiangalie Serikali yetu, wananchi wa
Mtwara walikuwa wanadai haki yao ya gesi, lakini wameweza kupata
matatizo makubwa ya kupelekewa majeshi kwa sababu tu asilimia kubwa ya
wananchi wa Mtwara ni Waislamu,”. Aliendelea kunukuu “Pia angalieni wananchi wa Loliondo walikuwa
wanadai haki yao ya ardhi, lakini hawakupelekewa majeshi kwa sababu
asilimia kubwa ya wananchi wa Loliondo ni Waskristo, pia Kamati za
Ulinzi na Usalama za dini zimeundwa na Bakwata pamoja na Serikali kwa
manufaa yao binafsi, hivyo kamati hizo zikija katika misikiti yenu
kujitambulisha wafungieni milango na madirisha kisha muwapige sana,”
alinukuu.
Alieleza kuwa kwa taratibu za Jeshi, alilazimika kumueleza Kamanda
wa Polisi mkoa wa Morogoro wakati huo, Faustine Shilogile, juu ya kauli
hizo na alipewa maagizo ya kumkamata Sheikh Ponda na kumfikisha katika
kituo kikuu cha Polisi. Alidai kuwa hakumkamata kutokana na wingi wa watu waliokuwapo
kwenye kongamano hilo kutokana na kuzingirwa na wafuasi wake na kuondoka
naye kusikojulikana.
Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mashahidi wengine kutoa ushahidi wao.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment