Hali ni ya joto kali jijini Dar es Salaam.
Katika kitongoji cha Maguruwe, Tandika Mikoroshini, nakutana na msichana
Zerish au Zena Mwita. Ni mweusi, mfupi kiasi na mwembamba.
Nakutana naye akiwa amemfunga vyema mtoto wake
mgongoni kwa khanga. Namuona anavyopepesuka, macho yamemlegea huku
akitoa harufu ya sigara. Hapana shaka kuwa amelewa.
Nagundua kuwa Zerish ni mtumiaji wa dawa za
kulevya. Anatumia heroin na wakati mwingine anachanganya na crack
cocaine. Namsalimia na ananijibu katika hali ya udhaifu.
“Niambie shoga yangu, unasemaje?” ananijibu Zerish.
Namweleza kuwa nataka kuongea naye na ananitaka kwanza nimweleze madhumuni ya ujio wangu pale.
“Kwani unataka kuongea na mimi kuhusu nini? Mbona sikuelewi shoga yangu?” ananiuliza.
Baada ya kujitahidi kumfafanulia lengo langu,
anakubali tuzungumze na anaanza kwa kunieleza historia yake akisema ni
mzaliwa wa Dar es Salaam na mkazi wa Yombo Buza.
Anasema alianza kutumia dawa za kulevya mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 17 tu baada ya kufundishwa na rafiki yake wa kiume. “Aliniwekea dawa kwenye bangi, mwanzoni nilikuwa
navuta sigara na bangi, lakini huyo mwanamume akaniwekea heroin kwenye
bangi bila kujua,” anasema.
Anasema siku ya kwanza baada ya kuvuta, hakujua
kama bangi aliyovuta ndani yake ilikuwa na dawa za kulevya; aligundua
baada ya kumaliza kutumia.
“Nilijisikia kutapika, nguvu ziliniisha yaani hali
yangu ilikuwa mbaya sana, nikamuuliza ameniwekea nini mbona leo ‘stimu’
tofauti?” anasimulia. Zerish anasema iliyofuata alijisikia hamu ya
kuvuta tena kilevi alichopewa na rafiki yake wa kiume. Huo ukawa mwanzo
wa kutumia dawa hizo haramu.
Tangu wakati huo, Zerish akawa mwathirika wa dawa za kulevya,
jambo ambalo lilimdhoofisha, akakonda kupita kiasi na akafikia kuwa na
tabia ya udokozi. Baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya, wazazi
wake waliamua kumfungia ndani ikiwa ni njia ya kumtoa kwenye ulevi huo.
“Nilifungiwa ndani miezi kama sita shoga yangu.
Nilipokaa ndani kama miezi minne hivi, nikaacha kabisa kutumia dawa,
yaani niliacha kabisa. Nikapendeza na mwili ukarudi, lakini juzijuzi,
nilipoachwa huru nikarudi tena mtaani,” anasema.
Kitendo cha wazazi wake kumuamini na kumpa uhuru
tena, pengine ni uamuzi mbaya ambao wazazi hao wanaujutia. Zerish
aliingia mtaani kwa kishindo na kuanza upya kutumia dawa za kulevya.
Kwa bahati mbaya, katika kipindi hichohicho alipata ujauzito ambao aliulea huku akivuta dawa hizo kama kawaida. “Nilianza upya kutumia dawa, nikiwa na mimba kwa hiyo mtoto wangu alianza kuwa tegemezi wa dawa akiwa tumboni,” anasema.
Hata baada ya kujifungua, aliendelea kutumia dawa
na anasema hakukaa ndani kama wanawake wengi wa Kitanzania wanavyotakiwa
kufanya, kwa sababu mwili wake ulikuwa unahitaji dawa na bila dawa hali
yake huwa mbaya nusu ya kufa. “Nani akae siku 40 ndani? Mimi nilianza kuzurura
tangu mtoto akiwa na siku mbili. Ilinibidi nitoke ndani niende kutafuta
dawa kwani bila hivyo hali yangu huwa mbaya,” anasema.
Akaanza kuwa mtu wa kuzunguka huku na kule akiwa
na mtoto mgongoni sambamba na mfuko wake wa plastiki wenye mahitaji
muhimu ya mtoto kama nepi na nguo.
“Ndiyo hivyo mwenzangu, inabidi nihangaike na
mtoto huko maskani ili nipate dawa, kwa sababu sitaki kumuacha nyumbani,
kwa hiyo nipo naye kila mahali,” anasema
Anasema anapovuta au kujichoma dawa, mtoto wake
pia hupata ‘stimu’ kwa sababu mtoto hupata dawa hizo za kulevya kupitia
maziwa ya mama yake na hivyo wote wawili kulala fofofo sehemu yeyote
ile.
Lakini kwa Zerish na mtoto wake, anapofikia hali
ya kuwa ‘alosto’ (wakati dawa za kulevya zinapoisha mwilini na hivyo
kuhitaji tena), huwa ni adhabu kali.
Anasimulia kuwa dawa zinapoisha mwilini na mtoto
naye huwa katika hali hiyo na hivyo hulia sana. Hali hiyo humfanya
Zerish akimbie kutafuta dawa ili ‘ajinusuru’ yeye na mwanaye.
Mtoto anapimwa
Mpango wa kuwasaidia waathirika
CHANZO: MWANANCHI
Anasema utegemezi wa dawa humfanya aende mitaa mbalimbali kufanya chochote kile ili apate fedha ya kununua ulevi huo.
“Najua kuwa namsumbua mtoto, lakini lazima nifanye hivyo kwa sababu ninapopata alosto huwa kizaazaa,” anasema.
Anasema dawa anazotumia huchukua saa tatu hadi nne
kuisha mwilini hivyo hutakiwa kununua tena ili awe katika hali ya ulevi
muda wote. Hali ya ulevi ndiyo huwa faraja kwake kuliko hali ya kukosa
kilevi ambayo anasema ni mateso makubwa.
Zerish anasema kila anapopata Sh2,000 tu, hukimbilia Mwembe Yanga, ambako ndiko anakonunua dawa hizo. Hata hivyo, msichana huyu, yu radhi kuacha dawa na amedhamiria kutafuta kituo cha tiba ya methadone ili aache ulevi huo. Mtaalamu wa tiba ya Methadone katika Hospitali ya
Mwananyamala, Dk Elifasi Mritu anasema katika kitengo cha tiba ya
methadone hospitalini hapo, wapo wanawake mbalimbali ambao hupatiwa tiba
pamoja na watoto waliowazaa wakiwa wanatumia dawa za kulevya.
“Ni kweli ukitumia dawa za kulevya wakati unanyonyesha au wakati wa mimba, mtoto naye huathirika,” anasema. Anasema kwa kawaida mtoto hunyonya chembechembe za dawa hizo na kuzoea hali ya matokeo ya dawa hizo.
Mtoto anapimwa
Damu ya mtoto ilichukuliwa na kwenda kupimwa
maabara ya Mwananyamala. Baada ya majibu kutoka, ilionekana kuwa ana
chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroini. Dk Elifasi alisema, damu ya mtoto anayenyonya maziwa ya mama anayetumia dawa za kulevya aghalabu hupata uraibu. Hivyo, hata mama huyo anapoanza matibabu ya
methadone, bado mtoto ataendelea kuwa na uraibu kwani methadone ni
mbadala tu wa heroini.
Mpango wa kuwasaidia waathirika
Mratibu wa mpango wa kuondoa madhara kwa watumiaji
wa dawa za kulevya wa madaktari wa ulimwengu (MDM), Ancella Voet
anasema madaktari hao ambao wamekuwa nchini tangu mwaka 2010, waligundua
kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya wapo katika wilaya za
Ilala, Temeke na Kinondoni na Zanzibar. Wanachokifanya ili kuondoa au kupunguza madhara kwa watumiaji hao ni kugawa sindano, mipira ya kiume na dawa za uzazi wa mpango.
“Tumepata baraka zote kutoka Wizara ya ya Afya na
manispaa husika. Tunashirikiana na hospitali za wilaya kuwasaidia vijana
hawa,” anasema Voet. Anasema wanapofika katika kambi hiyo hutakiwa kuoga, wanapewa sabuni, dawa ya meno, mswaki na mafuta ya kujipaka.
“Wengi wao hawapati mahitaji haya ambayo ni ya
lazima ndiyo maana tunawapa ili wawe wasafi na wawe sehemu inayoaminika
katika jamii,” anasema.
Katika kuhakikisha vijana hao wanaishi kwa
matumaini wanapimwa virusi vya Ukimwi, homa ya ini na TB kila wanapofika
kujiunga na MDM. Wanapewa pia elimu ya kisheria ili wajue haki zao.
Hii ni katika kuondoa unyanyapaa ambao upo kuanzia katika ngazi ya
familia na katika jamii. “Wengi wameanza tiba ya methadone ambayo ni
mbadala wa dawa za kulevya, na baada ya tiba hiyo wengi huwa huru na
hawawezi kurudia tena dawa za kulevya,” anasema.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment