Social Icons

Pages

Monday, December 29, 2014

WATOTO WANAVYOPATA URAIBU WA DAWA ZA KULEVYA


Hali ni ya joto kali jijini Dar es Salaam. Katika kitongoji cha Maguruwe, Tandika Mikoroshini, nakutana na msichana Zerish au Zena Mwita. Ni mweusi, mfupi kiasi na mwembamba.
Nakutana naye akiwa amemfunga vyema mtoto wake mgongoni kwa khanga. Namuona anavyopepesuka, macho yamemlegea huku akitoa harufu ya sigara. Hapana shaka kuwa amelewa.
Nagundua kuwa Zerish ni mtumiaji wa dawa za kulevya. Anatumia heroin na wakati mwingine anachanganya na crack cocaine. Namsalimia na ananijibu katika hali ya udhaifu.
“Niambie shoga yangu, unasemaje?” ananijibu Zerish.
Namweleza kuwa nataka kuongea naye na ananitaka kwanza nimweleze madhumuni ya ujio wangu pale.
“Kwani unataka kuongea na mimi kuhusu nini? Mbona sikuelewi shoga yangu?” ananiuliza.
Baada ya kujitahidi kumfafanulia lengo langu, anakubali tuzungumze na anaanza kwa kunieleza historia yake akisema ni mzaliwa wa Dar es Salaam na mkazi wa Yombo Buza.
Anasema alianza kutumia dawa za kulevya mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 17 tu baada ya kufundishwa na rafiki yake wa kiume. “Aliniwekea dawa kwenye bangi, mwanzoni nilikuwa navuta sigara na bangi, lakini huyo mwanamume akaniwekea heroin kwenye bangi bila kujua,” anasema.
Anasema siku ya kwanza baada ya kuvuta, hakujua kama bangi aliyovuta ndani yake ilikuwa na dawa za kulevya; aligundua baada ya kumaliza kutumia.
“Nilijisikia kutapika, nguvu ziliniisha yaani hali yangu ilikuwa mbaya sana, nikamuuliza ameniwekea nini mbona leo ‘stimu’ tofauti?” anasimulia. Zerish anasema iliyofuata alijisikia hamu ya kuvuta tena kilevi alichopewa na rafiki yake wa kiume. Huo ukawa mwanzo wa kutumia dawa hizo haramu.
Tangu wakati huo, Zerish akawa mwathirika wa dawa za kulevya, jambo ambalo lilimdhoofisha, akakonda kupita kiasi na akafikia kuwa na tabia ya udokozi. Baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya, wazazi wake waliamua kumfungia ndani ikiwa ni njia ya kumtoa kwenye ulevi huo.
“Nilifungiwa ndani miezi kama sita shoga yangu. Nilipokaa ndani kama miezi minne hivi, nikaacha kabisa kutumia dawa, yaani niliacha kabisa. Nikapendeza na mwili ukarudi, lakini juzijuzi, nilipoachwa huru nikarudi tena mtaani,” anasema.
Kitendo cha wazazi wake kumuamini na kumpa uhuru tena, pengine ni uamuzi mbaya ambao wazazi hao wanaujutia. Zerish aliingia mtaani kwa kishindo na kuanza upya kutumia dawa za kulevya.
Kwa bahati mbaya, katika kipindi hichohicho alipata ujauzito ambao aliulea huku akivuta dawa hizo kama kawaida. “Nilianza upya kutumia dawa, nikiwa na mimba kwa hiyo mtoto wangu alianza kuwa tegemezi wa dawa akiwa tumboni,” anasema.
Hata baada ya kujifungua, aliendelea kutumia dawa na anasema hakukaa ndani kama wanawake wengi wa Kitanzania wanavyotakiwa kufanya, kwa sababu mwili wake ulikuwa unahitaji dawa na bila dawa hali yake huwa mbaya nusu ya kufa. “Nani akae siku 40 ndani? Mimi nilianza kuzurura tangu mtoto akiwa na siku mbili. Ilinibidi nitoke ndani niende kutafuta dawa kwani bila hivyo hali yangu huwa mbaya,” anasema.
Akaanza kuwa mtu wa kuzunguka huku na kule akiwa na mtoto mgongoni sambamba na mfuko wake wa plastiki wenye mahitaji muhimu ya mtoto kama nepi na nguo.
“Ndiyo hivyo mwenzangu, inabidi nihangaike na mtoto huko maskani ili nipate dawa, kwa sababu sitaki kumuacha nyumbani, kwa hiyo nipo naye kila mahali,” anasema
Anasema anapovuta au kujichoma dawa, mtoto wake pia hupata ‘stimu’ kwa sababu mtoto hupata dawa hizo za kulevya kupitia maziwa ya mama yake na hivyo wote wawili kulala fofofo sehemu yeyote ile.
Lakini kwa Zerish na mtoto wake, anapofikia hali ya kuwa ‘alosto’ (wakati dawa za kulevya zinapoisha mwilini na hivyo kuhitaji tena), huwa ni adhabu kali.
Anasimulia kuwa dawa zinapoisha mwilini na mtoto naye huwa katika hali hiyo na hivyo hulia sana. Hali hiyo humfanya Zerish akimbie kutafuta dawa ili ‘ajinusuru’ yeye na mwanaye.
Anasema utegemezi wa dawa humfanya aende mitaa mbalimbali kufanya chochote kile ili apate fedha ya kununua ulevi huo.
“Najua kuwa namsumbua mtoto, lakini lazima nifanye hivyo kwa sababu ninapopata alosto huwa kizaazaa,” anasema.
Anasema dawa anazotumia huchukua saa tatu hadi nne kuisha mwilini hivyo hutakiwa kununua tena ili awe katika hali ya ulevi muda wote. Hali ya ulevi ndiyo huwa faraja kwake kuliko hali ya kukosa kilevi ambayo anasema ni mateso makubwa.
Zerish anasema kila anapopata Sh2,000 tu, hukimbilia Mwembe Yanga, ambako ndiko anakonunua dawa hizo. Hata hivyo, msichana huyu, yu radhi kuacha dawa na amedhamiria kutafuta kituo cha tiba ya methadone ili aache ulevi huo. Mtaalamu wa tiba ya Methadone katika Hospitali ya Mwananyamala, Dk Elifasi Mritu anasema katika kitengo cha tiba ya methadone hospitalini hapo, wapo wanawake mbalimbali ambao hupatiwa tiba pamoja na watoto waliowazaa wakiwa wanatumia dawa za kulevya.
“Ni kweli ukitumia dawa za kulevya wakati unanyonyesha au wakati wa mimba, mtoto naye huathirika,” anasema. Anasema kwa kawaida mtoto hunyonya chembechembe za dawa hizo na kuzoea hali ya matokeo ya dawa hizo.

Mtoto anapimwa
Damu ya mtoto ilichukuliwa na kwenda kupimwa maabara ya Mwananyamala. Baada ya majibu kutoka, ilionekana kuwa ana chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroini. Dk Elifasi alisema, damu ya mtoto anayenyonya maziwa ya mama anayetumia dawa za kulevya aghalabu hupata uraibu. Hivyo, hata mama huyo anapoanza matibabu ya methadone, bado mtoto ataendelea kuwa na uraibu kwani methadone ni mbadala tu wa heroini.

Mpango wa kuwasaidia waathirika
Mratibu wa mpango wa kuondoa madhara kwa watumiaji wa dawa za kulevya wa madaktari wa ulimwengu (MDM), Ancella Voet anasema madaktari hao ambao wamekuwa nchini tangu mwaka 2010, waligundua kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya wapo katika wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni na Zanzibar. Wanachokifanya ili kuondoa au kupunguza madhara kwa watumiaji hao ni kugawa sindano, mipira ya kiume na dawa za uzazi wa mpango.
“Tumepata baraka zote kutoka Wizara ya ya Afya na manispaa husika. Tunashirikiana na hospitali za wilaya kuwasaidia vijana hawa,” anasema Voet. Anasema wanapofika katika kambi hiyo hutakiwa kuoga, wanapewa sabuni, dawa ya meno, mswaki na mafuta ya kujipaka.
“Wengi wao hawapati mahitaji haya ambayo ni ya lazima ndiyo maana tunawapa ili wawe wasafi na wawe sehemu inayoaminika katika jamii,” anasema.
Katika kuhakikisha vijana hao wanaishi kwa matumaini wanapimwa virusi vya Ukimwi, homa ya ini na TB kila wanapofika kujiunga na MDM. Wanapewa pia elimu ya kisheria ili wajue haki zao. Hii ni katika kuondoa unyanyapaa ambao upo kuanzia katika ngazi ya familia na katika jamii. “Wengi wameanza tiba ya methadone ambayo ni mbadala wa dawa za kulevya, na baada ya tiba hiyo wengi huwa huru na hawawezi kurudia tena dawa za kulevya,” anasema.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: