Pages

Wednesday, December 17, 2014

MAKOCHA WAIPONDA YANGA

Kocha Hans van Pluijm akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere usiku wa kuamkia jana tayari kujiunga na Yanga.

Makocha wanaofundisha katika klabu za Ligi Kuu wameukosoa uongozi wa Yanga kwa kumtimua kocha, Marcio Maximo kwa kutumia kisingio za mechi ya Mtani Jembe.
Wakizungumza na gazeti hili, makocha Mecky Mexime wa Mtibwa, David Mwamaja wa Prisons, Felix Minziro wa JKT Ruvu, Jackson Mayanja wa Kagera Sugar waliutaka uongozi wa Yanga kueleza sababu nyingine ya kumfukuza Maximo na si kutumia mechi ya Mtani Jembe.
“Hiyo ni fitina tu, lakini bado Maximo ni kocha mzuri na amefanya kazi nzuri Yanga, tangu amekuja hadi sasa timu iko kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi,” alisema Jackson Mayanja wa Kagera Sugar.
Alisema Maximo alipaswa kupewa muda tofauti na ilivyofanya Yanga kumtimua hata kabla ya msimu kumalizika na kusisitiza kuwa kocha huyo kafukuzwa kwa utashi wa viongozi, lakini bado ana kiwango kikubwa.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime alisema “Labda Yanga ituambie ukweli kuwa kuna sababu nyingine, lakini hii mechi ya Mtani Jembe siyo kigezo cha Maximo kufukuzwa, kwanza ni mechi ya kirafiki ingekuwa na uzito kiasi hicho wachezaji wasingecheza bila kusajiliwa.
“Yanga imefanya papara haikustahili kumfukuza kocha wao na kwa kufanya hivyo, basi itabadili makocha kila wakati kwa kuwa hakuna timu ambayo haifungwi popote duniani, lakini wanachokifanya siyo sahihi,” alisema Mexime.
Wakati kocha wa Prisons, David Mwamaja alisema hana muda na timu hiyo ingawa hafurahishwi na kitendo chao cha kufukuza makocha ovyo bila kuangalia upande wa pili.
Huku kocha Minziro aliyewahi pia kutimuliwa Yanga alisema, “Ni kawaida makocha kutimuliwa wanaposhindwa kutoa msaada, lakini kwa Tanzania ni shida hasa kwenye timu kubwa kama Simba na Yanga, kwa mtindo huu watafukuzana sana.”

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment