Pages

Wednesday, December 17, 2014

SERIKALI KUTAFUTA SOKO LA UTALII NCHI ZA GHUBA


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kutafuta soko la utalii kutoka nchi za Ghuba na Mashariki ya Kati ili kuongeza idadi ya watalii nchini na kukuza pato la Taifa kupitia sekta hiyo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo inasema Pinda ametoa rasi hiyo alipofungua Kongamano la siku mbili la Utalii na Uwekezaji lilionza leo kwenye Hoteli ya Le Meridien, jijini Dubai, Falme za Kiarabu.
“Tunao mkakati wa kukuza utalii nchini lakini wengi wamekuwa wakitoka Ulaya na Marekani. Eneo ambalo tumeona tuwekeze kwa nguvu kwa maana ya kuongeza idadi ya watalii ni hili la nchi za Ghuba na Mashariki ya Kati,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kimahusiano Tanzania iko karibu na nchi hizo za ghuba lakini pia wanao uwezo wa kifedha wa kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya utalii.
Alitoa wito kwa makampuni yanayotaka kuwekeza nchini yaangalie fursa zilizopo kwenye ujenzi wa hoteli za kawaida, hoteli za mahema (tented camps) na hoteli zenye kutoa huduma za vyakula (special cuisine restaurant).
Hata hivyo, Pinda aliwataka wawekezaji watakaokuja wafanye juhudi ya kushirikiana na Watanzania wazawa ili nao wajione ni sehemu ya uwekezaji huo.
Mapema, akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka mitano, Tanzania imeweza kuongeza idadi ya watalii kutoka 714,367 mwaka 2009 hadi kufikia watalii 1,095,884 kwa mwaka 2013.
“Kiwango cha mapato ya watalii hao kiliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.8 katika kipindi hicho hicho cha miaka mitano,” alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo inaajiri watu zaidi ya 400,000 kuchangia asilimia 17 kwenye pato la Taifa.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na washiriki wa kongamano hilo alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuhifadhi rasilmali zake na kuzitumia kwa utalii.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment