Kocha Hans van Pluijm akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere usiku wa kuamkia jana tayari kujiunga na Yanga.
Makocha wanaofundisha katika
klabu za Ligi Kuu wameukosoa uongozi wa Yanga kwa kumtimua kocha, Marcio
Maximo kwa kutumia kisingio za mechi ya Mtani Jembe.
Wakizungumza na gazeti hili, makocha Mecky Mexime
wa Mtibwa, David Mwamaja wa Prisons, Felix Minziro wa JKT Ruvu, Jackson
Mayanja wa Kagera Sugar waliutaka uongozi wa Yanga kueleza sababu
nyingine ya kumfukuza Maximo na si kutumia mechi ya Mtani Jembe.
“Hiyo ni fitina tu, lakini bado Maximo ni
kocha mzuri na amefanya kazi nzuri Yanga, tangu amekuja hadi sasa timu
iko kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi,” alisema Jackson
Mayanja wa Kagera Sugar.
Alisema Maximo alipaswa kupewa muda tofauti na
ilivyofanya Yanga kumtimua hata kabla ya msimu kumalizika na kusisitiza
kuwa kocha huyo kafukuzwa kwa utashi wa viongozi, lakini bado ana
kiwango kikubwa.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime alisema “Labda Yanga
ituambie ukweli kuwa kuna sababu nyingine, lakini hii mechi ya Mtani
Jembe siyo kigezo cha Maximo kufukuzwa, kwanza ni mechi ya kirafiki
ingekuwa na uzito kiasi hicho wachezaji wasingecheza bila kusajiliwa.
“Yanga imefanya papara haikustahili kumfukuza
kocha wao na kwa kufanya hivyo, basi itabadili makocha kila wakati kwa
kuwa hakuna timu ambayo haifungwi popote duniani, lakini wanachokifanya
siyo sahihi,” alisema Mexime.
Wakati kocha wa Prisons, David Mwamaja alisema
hana muda na timu hiyo ingawa hafurahishwi na kitendo chao cha kufukuza
makocha ovyo bila kuangalia upande wa pili.
Huku kocha Minziro aliyewahi pia kutimuliwa Yanga
alisema, “Ni kawaida makocha kutimuliwa wanaposhindwa kutoa msaada,
lakini kwa Tanzania ni shida hasa kwenye timu kubwa kama Simba na Yanga,
kwa mtindo huu watafukuzana sana.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment