Katika barua yake kwa Rais Jakaya Kikwete, Jaji
Werema alisema ameomba kujiuzulu kwa sababu; “ushauri wake kuhusiana na
suala la Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa.”
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu
ilisema jana kuwa Rais Kikwete amekubali ombi hilo la kujiuzulu na
amemshukuru Jaji Werema kwa; “utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na
uadilifu.”
Jaji Werema ambaye mara kwa mara amekuwa akitetea
ushauri katika sakata hilo, amechukua uamuzi huo katika siku ya mwisho
ya wiki moja iliyoahidiwa na Rais Kikwete kukamilisha uchambuzi wa
taarifa za Bunge na kutoa uamuzi dhidi ya wahusika wa sakata hilo.
Uamuzi wa Werema unatokana na mazimio ya Bunge ya
kutaka yeye na baadhi ya vigogo wachukuliwe hatua kutokana na madai ya
kuhusika kwenye sakata la uchotwaji fedha katika akaunti hiyo.
Mwanasheria huyo alilalamikia maazimio hayo
akisema hayakuwa ya haki kwa wote waliotuhumiwa na uamuzi huo ulifanywa
kwa hasira na kufuata mkumbo.
Bunge liliazimia Jaji Werema kushughulikiwa kwa
mujibu wa sheria kutokana na kuipotosha Serikali kuhusu malipo ya Sh306
bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, akishauri fedha hizo zilipwe
kwa Kampuni ya IPTL iliyo na mkataba wa ufuaji umeme na Tanesco bila ya
kukata kodi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment