Kama ulibahatika
kutazama tamthilia miaka ya 1990 - 2003, basi jina la Nyamayao na
Kibakuli siyo geni masikioni mwako na hata sura zao.
Watoto hawa wawili walikuwa wanaunda familia ya
Mhogo Mchungu. Ni familia iliyokuwa na visa vingi hasa baada ya Mhogo
Mchungu kutaka kumuoza Nyamayao ilhali alikuwa bado kigori. Hadithi hii
ninaikumbuka pindi ninapokutana ana kwa ana na Nyamayao ambaye kwa sasa
ni mama wa familia.
Kibakuli amebadilika hivi sasa si mnene kama
alivyokuwa mdogo, lakini kwa Happyness Wenslaus ‘Nyamayao’ bado ana umbo
na kimo kilekile, ni kati ya waigizaji wa kike ambao wanajitunza kwani
hajabadilika licha ya kupata umaarufu akiwa binti mdogo. Mwananchi lilifanya mahojiano na mwigizaji huyu
ambaye alizungumza mengi, kuhusu anachokifanya kwa hivi sasa,
kilichomfanya aachane na uigizaji, kwanini ameamua kuirudia upya sanaa
na hata ndoto za maisha yake ya baadaye.
Kwa miaka 11 umekuwa nyuma ya kamera na hujatokea tena katika tamthilia wala filamu kulikoni?
Nimekaa muda mrefu kimya kwa sababu tamthilia
yangu ya mwisho nimeigiza mwaka 2003 baada ya hapo nikamaliza elimu ya
sekondari na hapo nikajiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari DSJ,
nilipomaliza chuo nikawa na mambo mbalimbali ya kwangu binafsi.
Ina maana sanaa ndiyo umeipa kisogo?
Ndiyo maana unaniona niko na wasanii wenzangu ina
maana kwamba ninarudi tena kwa kasi. Kwa sasa hivi ninafanya tamthilia,
tumejikusanya wasanii ambao tulikuwa tunafanya kazi zamani kipindi cha
nyuma, na tukaunda kikundi kipya ambacho kinaitwa ‘Kaone Sanaa Group’.
Na tumeanza kufanya tamthilia ambayo Mungu akipenda mwakani mwanzoni
itaanza kuonekana runingani.
Miezi michache nyuma iliwahi kuelezwa kwamba unaigiza filamu imeishia wapi na ni filamu gani?
Nimefanya filamu za watu kama mbili hivi, japokuwa
hazijaingia sokoni nimefanya ya kwangu mwenyewe moja na sasa hivi
nimejikita rasmi katika tamthiliya. Kuna filamu niliyoifanya mwenyewe
imetoka miezi mitatu iliyopita, hizi za watu wengine hazijatoka ‘Malipo’
na ‘Prisoner’.
Kwa faida ya wasomaji nini kilikuweka mbali na sanaa ya uigizaji?
Mambo ya maisha na majukumu yangeniweka mbali na
familia, wakati mwingine ukishaingia katika familia kuna watoto na nini
kuna vitu lazima uhakikishe umeviweka sawa. Kwa upande wangu si kwamba
nilikuwa nimeacha ila kuna mambo yalinilazimu niache kwanza.
Kwa kipindi ulichokaa mbali, huoni kwamba ungekuwa mbali iwapo ungeiendeleza?
Hiyo ni kweli hata mimi nimeliona hilo na pia huwa
nafikiria kila siku, Nyamayao kipaji nilikuwa nacho ila wakati huo
sanaa ilikuwa hailipi ndiyo maana ilikuwa rahisi mtu kufikia maamuzi
hayo, nafikiri nisingeamua kufanya hivyo lakini imeshakuwa na siwezi
kuibadilisha.
Wakati unafanya maamuzi hayo Nyamayao ulikuwa na umri gani?
Nilikuwa si mdogo sana kusema kwamba sielewi
nafanya nini nilikuwa naelewa, nakumbuka mara ya mwisho kutayarisha
tamthilia ilikuwa mwaka 2003 nikiwa na miaka 21, kwa hiyo ni mtu ambaye
nilikuwa nimekomaa si kusema kwamba mtoto mdogo asiyejua anafanya nini.
Wakati ukiwa mbali na sanaa ulikumbana na changamoto zipi?
Changamoto katika maisha zipo uwe unaigiza
hauigizi zipo pale pale, ila sijaziona sana kwa kipindi hicho kwa kuwa
mimi ni mjasiriamali kwa sababu kipindi ambacho nilikuwa naigiza, sanaa
ilikuwa bado haina mwamko wala haitengenezi pesa kama sasa hivi. Kipindi
cha miaka ya 99 mpaka 2000 kuna tofauti kubwa sana na sasa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment