Kuna wakati baadhi yetu tunapenda kufanya vitu
kwa mazoea, japo vinaweza kuwa na madhara makubwa katika maisha yetu.
Nitavitaja baadhi. Picha: Maktaba
Tangu kuja kwa teknolojia ya simu za mkononi na
mitandao ya kompyuta, watumiaji wengi tunafanya mambo kiholela tukisahau
kuwa kuna watu wanaweza kutudhuru kwa kutumia vifaa hivi vya
mawasiliano.
Kwa mfano, baadhi yetu tunamiliki anuani kadhaa za
baruapepe kama vile za kazini, binafsi na nyingine kwa ajili ya masomo
au shughuli kama za biashara, lakini tunajisahau na kutumia nywila (neno
la siri)linalofanana kila mahali.
Hii inamaanisha kama mhalifu akifanikiwa kuiba
nywila ya baruapepe moja, ana uwezo wa kujua nyingine zote na baada ya
hapo kitakachotokea ni maumivu.
Tumia nywila tofauti kwenye kila anuani au kama
unashindwa kutengeneza nywila tumia programu maalumu ambazo ni bure
zinazoweza kukusaidia kutengeneza nywila.
Aidha, wengi wetu tunapenda kubadilisha kompyuta
na simu mara kwa mara au kutoa vifaa vyetu kwa watu tunaowaamini huku
tukiacha vitu muhimu kwenye vifaa hivyo kama picha, taarifa za kibenki
na nyaraka nyingine muhimu.
Taarifa hizi zinaweza kuibwa au kuingia kwenye
mikono ya mtu ambaye si sahihi na ndipo tunapoona nyaraka kuvuja au
mawasiliano ya watu kujulikana au hata picha za watu kusambazwa kwenye
mitandao.
Kukaa kwenye meza na kiti chako huku ukitumia
kompyuta kwa zaidi ya saa nane au zaidi kunaweza kukusababishia madhara
kwenye misuli yako, tatizo la uzito, kisukari na magonjwa mengine
mbalimbali.
Kama wewe ni mwajiriwa unaweza kuongea na mwajiri wako akutafutie viti vizuri vya kutumia ukiwa kazini.
Kuna utamaduni wa watu kutumia vifaa vya wenzao
kama kompyuta kwa ajili ya kuangalia baruapepe au kusoma chochote kile.
Hili nalo si sahihi, kwani wengi wanajikuta wakisahau kufunga kurasa za
mitandao wanayofungua ikiwamo baruapepe.
Kama umezoea tabia hii unashauriwa kuacha hata
kama ni kifaa chako. Unapomaliza kutumia jiondoe kwa kufuata utaratibu
uliowekwa na watengenezaji wa ukurasa unaoupitia.
Kompyuta inapotumika kwa muda mrefu inaweza
kusababisha madhara kwa programu na vitu vingine unavyofanya.
Unashauriwa uizime kabisa ipumzike au uzime na kuwasha ‘restart’.
Ukiiamrisha kwa kupitia ‘sleep au standby mode’ itaifanya kompyuta yako kuwa na mwendo mdogo na pengine kuharibu programu.
Unashauriwa kuangalia simu yako kabla ya kulala na
zaidi izime ndiyo ulale au kama inawaka basi iweke mbali na upeo wa
kichwa chako.
Utafiti uliofanyika siku za karibuni na taasisi
moja ya nchini Marekani, imegundua mwanga wa simu una madhara katika
usingizi wa mwanadamu
Ule mwanga wa bluu unaotoka kwenye simu yako
unaweza kuufanya mwili kufikiri ni alfajiri, kwa hiyo una vuruga mfumo
wako wa usingizi.
Kila kifaa cha mawasiliano na programu zilizoko
ndani yake zinahitaji kuboreshwa kwa kufanyiwa ‘updates’ kwa hiyo kama
umepata ujumbe wa kufanya update kwenye simu yako au kompyuta yako na
ukathibitisha ujumbe huo ni halisi, tafadhali timiza ulichoelekezwa.
Kufanya hivi kunaweza kukuepusha na mambo mengi
mabaya yanayoweza kuathiri kifaa chako cha mawasiliano. Hii ni sawa na
mtu anayekula au kutumiwa dawa kama anavyoelekezwa kwa ajili ya kulinda
afya yake.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment