
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti
jana, Ofisa mtendaji mkuu wa RITA, Phillip Saliboko na Meneja masoko na
mawasiliano, Josephat Kimaro walisema upekuzi wa nyaraka zilizotumiwa na
Sitti uliofanywa na wanasheria wao, tayari umekamilika.
“Kazi yetu (RITA) tumeimaliza na upekuzi wa
taarifa za Sitti umekamilika na kinachofuata sasa ni kupeleka nyaraka
hizo kwenye mamlaka inayohusika ambayo ni polisi, wao ndio wataamua nini
cha kufanya,” alisema Kimaro.
Alisema Rita haiwezi kumhukumu moja kwa moja
mrembo huyo kuwa alighushi nyaraka na kudanganya ili apate cheti hicho
cha kuzaliwa kilichotolewa na RITA Septemba na badala yake wanapeleka
vielelezo walivyonavyo polisi ili nao wavifanyie kazi.
“Sisi (RITA) jukumu letu lilikuwa ni upekuzi wa
nyaraka, kazi ambayo imefanywa kwa ustadi mkubwa na jopo la wanasheria
wetu na hadi sasa imekamilika na kinachofuata ni kuzipeleka nyaraka hizo
polisi ambao wao ndiyo wenye jukumu la uchunguzi na kumchukulia hatua
Sitti au la,” alisema.
Wakati huohuo, Saliboko akieleza kuwa bado wana
changamoto ya baadhi ya watu kudanganya taarifa zao ili wapate vyeti vya
kuzaliwa na kusisitiza kuwa wanaandaa mfumo maalumu ili kukomesha
udanganyifu huo.
“Tukibaini mtu ametumia udanganyifu ili kupata
cheti, kwanza huwa tunamfutia cheti chake na taratibu nyingine za
kisheria zinafuata. Tunafanya hivyo kwa watu wote wanaokuja kuomba vyeti
kwetu na siyo kwa Miss Tanzania peke yake japo hili la Sitti tunaiachia
mamlaka husika ifanye kazi yake,” alisema.
Sitti Mtemvu aliingia kwenye kashfa ya kudanganya
umri wake na nyaraka zake mbalimbali zilionyesha alizaliwa 1989, umri
ambao umepitiliza ule unaotakiwa kwa mshiriki wa mashindano ya Miss
Tanzania, huku cheti chake kikionyesha alizaliwa 1991, hivyo kulazimika
kuvua taji hilo.
Wakati huohuo, mrembo aliyevikwa taji la Miss
Tanzania nambari mbili, Lilian Kamazima anatarajiwa kuwasili leo mjini
Arusha na kupokewa kwa shangwe akiwa na taji lake.
Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa Kampuni ya
Mwandago Entertainment Ltd, Faustine Mwandago iliyosimamia ushindi wake
ngazi ya kanda ilisema kuwa mrembo huyo atawasili kwenye Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) saa 6:00 mchana.
Mwandago alisema kuwa mrembo huyo atapokelewa na
wenyeji wake, wakiwamo wazazi wake na kisha kupanda gari la wazi ili
kuwapa fursa wakazi wa Arusha kumshuhudia.
Alisema kuwa mara baada ya kuwasili Arusha atapelekwa moja kwa
moja nyumbani kwao, Sakina ili kushiriki hafla aliyoandaliwa na wazazi
wake pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.
Wakazi wa Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi
kumpokea mrembo huyo kwa lengo la kumpa moyo na kulikaribisha taji hilo
mara baada ya ukame wa muda mrefu wa kupata taji la Miss Tanzania.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment