Pages

Tuesday, November 18, 2014

ACHA TABIA HIZI UNAPOTUMIA VIFAA VYA MAWASILIANO

Kuna wakati baadhi yetu tunapenda kufanya vitu kwa mazoea, japo vinaweza kuwa na madhara makubwa katika maisha yetu. Nitavitaja baadhi. Picha: Maktaba
Tangu kuja kwa teknolojia ya simu za mkononi na mitandao ya kompyuta, watumiaji wengi tunafanya mambo kiholela tukisahau kuwa kuna watu wanaweza kutudhuru kwa kutumia vifaa hivi vya mawasiliano.
Kwa mfano, baadhi yetu tunamiliki anuani kadhaa za baruapepe kama vile za kazini, binafsi na nyingine kwa ajili ya masomo au shughuli kama za biashara, lakini tunajisahau na kutumia nywila (neno la siri)linalofanana kila mahali.
Hii inamaanisha kama mhalifu akifanikiwa kuiba nywila ya baruapepe moja, ana uwezo wa kujua nyingine zote na baada ya hapo kitakachotokea ni maumivu.
Tumia nywila tofauti kwenye kila anuani au kama unashindwa kutengeneza nywila tumia programu maalumu ambazo ni bure zinazoweza kukusaidia kutengeneza nywila.
Aidha, wengi wetu tunapenda kubadilisha kompyuta na simu mara kwa mara au kutoa vifaa vyetu kwa watu tunaowaamini huku tukiacha vitu muhimu kwenye vifaa hivyo kama picha, taarifa za kibenki na nyaraka nyingine muhimu.
Taarifa hizi zinaweza kuibwa au kuingia kwenye mikono ya mtu ambaye si sahihi na ndipo tunapoona nyaraka kuvuja au mawasiliano ya watu kujulikana au hata picha za watu kusambazwa kwenye mitandao.
Kukaa kwenye meza na kiti chako huku ukitumia kompyuta kwa zaidi ya saa nane au zaidi kunaweza kukusababishia madhara kwenye misuli yako, tatizo la uzito, kisukari na magonjwa mengine mbalimbali.
Kama wewe ni mwajiriwa unaweza kuongea na mwajiri wako akutafutie viti vizuri vya kutumia ukiwa kazini.
Kuna utamaduni wa watu kutumia vifaa vya wenzao kama kompyuta kwa ajili ya kuangalia baruapepe au kusoma chochote kile. Hili nalo si sahihi, kwani wengi wanajikuta wakisahau kufunga kurasa za mitandao wanayofungua ikiwamo baruapepe.
Kama umezoea tabia hii unashauriwa kuacha hata kama ni kifaa chako. Unapomaliza kutumia jiondoe kwa kufuata utaratibu uliowekwa na watengenezaji wa ukurasa unaoupitia.
Kompyuta inapotumika kwa muda mrefu inaweza kusababisha madhara kwa programu na vitu vingine unavyofanya. Unashauriwa uizime kabisa ipumzike au uzime na kuwasha ‘restart’.
Ukiiamrisha kwa kupitia ‘sleep au standby mode’ itaifanya kompyuta yako kuwa na mwendo mdogo na pengine kuharibu programu.
Unashauriwa kuangalia simu yako kabla ya kulala na zaidi izime ndiyo ulale au kama inawaka basi iweke mbali na upeo wa kichwa chako.
Utafiti uliofanyika siku za karibuni na taasisi moja ya nchini Marekani, imegundua mwanga wa simu una madhara katika usingizi wa mwanadamu
Ule mwanga wa bluu unaotoka kwenye simu yako unaweza kuufanya mwili kufikiri ni alfajiri, kwa hiyo una vuruga mfumo wako wa usingizi.
Kila kifaa cha mawasiliano na programu zilizoko ndani yake zinahitaji kuboreshwa kwa kufanyiwa ‘updates’ kwa hiyo kama umepata ujumbe wa kufanya update kwenye simu yako au kompyuta yako na ukathibitisha ujumbe huo ni halisi, tafadhali timiza ulichoelekezwa.
Kufanya hivi kunaweza kukuepusha na mambo mengi mabaya yanayoweza kuathiri kifaa chako cha mawasiliano. Hii ni sawa na mtu anayekula au kutumiwa dawa kama anavyoelekezwa kwa ajili ya kulinda afya yake.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment