Pages

Thursday, October 23, 2014

WAUGUZI WA ZAHANATI WATUMIA CHEMLI KUHUDUMIA WAGONJWA

Taa aina ya Chemli inayotumika hasa maeneo ya vijijini ambayo umeme haujafika 
Wauguzi wa Zahanati ya Kurugee katika Kijiji cha Bulaga wilayani hapa wanalazimika kutumia chemli wodini wakati wa kuwahudumia wagonjwa kutokana na kukosekana kwa umeme.

Mganga wa zahanati hiyo, Micoruah Simion alimwambia meneja wa mkoa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mara, Henry  Byabato, kuwa awali walikuwa wakitumia karabai ambazo kwa sasa zimeishiwa gesi na halmashauri ya wilaya haijatoa fedha za kununulia gesi nyingine mpaka sasa.
Simion alisema halmashauri pia ilikuwa ikipeleka mafuta ya taa, lakini ni kipindi kirefu haijapeleka na inapotokea mjamzito anataka kujifungua usiku, inabidi atumie taa ya chemli ya nyumbani kwake.
Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo, Simion alisema zahanati hiyo ina upungufu mkubwa wa vifaa tiba na dawa, zikiwamo za chanjo mbalimbali za watoto wachanga.
Alisema tatizo la upungufu wa chanjo linasababishwa na sehemu ya kuhifadhia kwani nyingi huhitaji kuhifadhiwa kwenye majokofu.
Alisema zahanati hiyo yenye wahudumu watatu, inatoa huduma kwa wakazi 14,215 wanaotokana na kaya 2,226, wa vijiji vitatu vya Bulaga, Bukumi na Busekera.
Naye Byabato alisema ingawa mkataba na mkandarasi hauonyeshi eneo hilo kupatiwa umeme, aliahidi kuwa atahakikisha zahanati hiyo inaunganishiwa umeme.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment