Taa aina ya Chemli inayotumika hasa maeneo ya vijijini ambayo umeme haujafika 
            
 Wauguzi wa Zahanati ya Kurugee katika 
Kijiji cha Bulaga wilayani hapa wanalazimika kutumia chemli wodini 
wakati wa kuwahudumia wagonjwa kutokana na kukosekana kwa umeme.
Mganga wa zahanati hiyo, Micoruah Simion 
alimwambia meneja wa mkoa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mara, 
Henry  Byabato, kuwa awali walikuwa wakitumia karabai ambazo kwa sasa 
zimeishiwa gesi na halmashauri ya wilaya haijatoa fedha za kununulia 
gesi nyingine mpaka sasa.
Simion alisema halmashauri pia ilikuwa ikipeleka 
mafuta ya taa, lakini ni kipindi kirefu haijapeleka na inapotokea 
mjamzito anataka kujifungua usiku, inabidi atumie taa ya chemli ya 
nyumbani kwake.
Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo, Simion
 alisema zahanati hiyo ina upungufu mkubwa wa vifaa tiba na dawa, 
zikiwamo za chanjo mbalimbali za watoto wachanga.
Alisema tatizo la upungufu wa chanjo linasababishwa na sehemu ya kuhifadhia kwani nyingi huhitaji kuhifadhiwa kwenye majokofu.
Alisema zahanati hiyo yenye wahudumu watatu, 
inatoa huduma kwa wakazi 14,215 wanaotokana na kaya 2,226, wa vijiji 
vitatu vya Bulaga, Bukumi na Busekera.
Naye Byabato alisema ingawa mkataba na mkandarasi 
hauonyeshi eneo hilo kupatiwa umeme, aliahidi kuwa atahakikisha zahanati
 hiyo inaunganishiwa umeme.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment