Social Icons

Pages

Tuesday, June 02, 2015

UCHAMBUZI WA BAJETI: BAJETI YA UJENZI IMEKIDHI VIGEZO



Shughuli zinazofanywa na Wizara ya Ujenzi na umuhimu wake kiuchumi zinaifanya iwe wizara mtambuka. Hivyo bajeti yake inapaswa kutazamwa kwa minajili hiyo. Kiuchumi barabara ni muhimu kusafirishia rasilimali watu na bidhaa mbalimbali.
Utangulizi
Miundombinu ya usafirishaji ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote. Miundombinu hii ni pamoja na barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, bandari na nyinginezo. Kiuchumi, hii ni miundombinu migumu (hard infrastructure) ukilinganisha na miundombinu kama ya mawasiliano ikiwamo simu na intaneti ambayo ni miundombinu laini (soft infrastructure) ya kiuchumi. Wizara ya Ujenzi inajihusisha na baadhi ya miundombinu hii migumu. Kwa kiwango kikubwa inajihusisha na barabara na madaraja.

Wizara mtambuka
Shughuli zinazofanywa na Wizara ya Ujenzi na umuhimu wake kiuchumi zinaifanya iwe wizara mtambuka. Hivyo bajeti yake inapaswa kutazamwa kwa minajili hiyo. Kiuchumi barabara ni muhimu kusafirishia rasilimali watu na bidhaa mbalimbali. Pamoja na mambo mengine, barabara nzuri ni mojawapo ya vitu vinavyofanya uwekezaji, uzalishaji mali na biashara mbalimbali kufanikiwa. Hii ni wizara mtambuka. Shughuli nyingi za maendeeo ya uchumi na jamii yanategemea miundombinu inayojengwa na wizara hii.
Kwa mfano, shughuli za kilimo, viwanda, utalii, biashara, elimu, madini na nyinginezo hutegemea miundombinu inayojengwa na wizara hii. Kwa mantiki hii, umuhimu wa kuwa na bajeti nzuri katika Wizara ya Ujenzi hauwezi kupingwa.

Fedha kidogo zilitoka 2014/15
Katika mapitio ya bajeti ya 2014/15 inaonekana kuwa wizara iliidhinishiwa Sh662,234,027,000.00 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Fedha zilizotolewa hadi Aprili, ni Sh444,729,086,445. Hii ni sawa na asilimia kama 67.2 ya fedha zilizopangwa. Hiki ni kiwango kidogo hasa kama fedha zilizobaki hazitatolewa. Pamoja na mambo mengine, fedha za ujenzi zinapokuwa hazitoki kama zilivyoidhinishwa maana yake ni maendeleo duni ya sekta hii na zile zote zinazoitegemea hasa ikizingatiwa kwamba hii ni sekta mtambuka.
Pia, fedha za ujenzi zinapokuwa hazitoki kama zilivyoidhinishwa maana yake ni mrundikano wa madeni kwa watoa huduma na bidhaa katika wizara hii. Kati ya makundi yanayoathirika ni makandarasi wa barabara.
Pamoja na mambo mengine, makandarasi kutolipwa ni kurudisha nyuma sekta binafsi katika shughuli za ujenzi. Uchambuzi wa bajeti ya Wizara ya Biashara na Viwanda unaonyesha kuwa hadi Aprili, zaidi ya asilimia 83 ya fedha zilizopangwa zilitolewa. Ni vizuri Wizara ya Ujenzi ikajifunza mbinu zilizotumiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupata kiasi hicho cha fedha.

Utekelezaji miradi ulikuwa mzuri
Kwa kadri ya mapitio ya Waziri wa Ujenzi, jumla ya kilomita 504.4 kati ya 539 zilizopangwa kujengwa kwa kiwango cha lami zilikuwa zimekamilika hadi kufikia Aprili. Uchambuzi unaonyesha kuwa kiwango cha utekelezaji ni asilimia 93.6. Kama mambo mengine yapo sawa, mfano ubora wa barabara hizi. Hiki ni kiwango kizuri ukizingatia kuwa kilifikiwa kwa kutumia asilimia 67.2 tu ya fedha zilizopangwa. Kwa maneno mengine, kumekuwapo na upungufu wa fedha kwa asilimia 32.8 lakini nakisi ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara zilizopangwa ni asilimia 6.4 tu. Kibajeti hii ni ishara nzuri inayoonyesha kuwa kama fedha zote zilizopangwa zingetoka, ujenzi wa barabara zilizopangwa ungeweza kufikia asimia 100.

Umuhimu wa kandarasi na malighafi za ndani
Zaidi ya kushangilia utekelezaji mzuri wa ujenzi wa barabara kwa maana ya kilomita zilizokamilika, uchambuzi zaidi unahitajika. Pamoja na mambo mengine, ni muhimu kujua ni kiasi gani cha barabara hizi kilijengwa na makandarasi wazawa na pia kiasi gani cha ujenzi huo kilitumia rasilimali za ndani ya nchi.
Kiuchumi, shughuli kama za kujenga kilomita zaidi ya 500 kwa kiwango cha lami zikifanywa na makandarasi wa ndani na kutumia malighafi za ndani kama vile nguvu kazi, saruji, kokoto, mawe, nondo na nyinginezo, ni faida kubwa.
Maana yake ni kuwa fedha nyingi zinakuwa zimebaki ndani ya nchi kuliko katika hali ambayo makandarasi wa nje na malighafi kutoka nje zinapokuwa zimetumika.
Kwa mantiki hii, bajeti ya Wizara ya Ujenzi inaweza kuwa ni chombo cha kuchochea ukuaji na maendeleo ya uchumi na juhudi za kupiga vita umaskini kama mipango ya kimkakati ikiwezesha makandasi wa ndani na malighafi za ndani kutumika. Hata hivyo, suala la msingi ni ubora na ushindani. Kukiwa na ubunifu, wizara inaweza kujenga ubora na ushindani huu.

Bajeti nzuri ya maendeleo
Wizara iliomba Sh932,715,351,000 kwa mwaka wa fedha 2015/16. Sh42,142,581,000 sawa na asilimia 4.5 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Sh890,572,770,000.00 sawa na asilimia 95.5 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kama tarakimu za fedha za matumizi ya kawaida na zile za matumizi ya maendeleo katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi hazijakosewa, hii itakuwa ni bajeti pekee kwa siku za usoni kutenga asilimia kubwa hivi (95.5) ya bajeti kwa shughuli za maendeleo.
Inakuwa ni bajeti ya maendeleo iliyo nzuri kupita kiasi. Hii asilimia 95.5 ni asilimia kubwa kiasi kwamba hiyo asilimia 4.5 iliyotengwa kwa shuguli za kawaida huenda isiweze ‘kuendesha’ na ‘kutumikia’ shughuli za maendeleo zinazomeza asilimia 95.5 ya bajeti. Japokuwa kilio katika bajeti zetu ni kuwa na asilimia kubwa katika maendeleo, lakini ni lazima kujua kuwa kinachotakiwa ni uwiano mzuri. Maji yakizidi saruji na kokoto au saruji na kokoto vikizidi maji, uwiano unaotakiwa kwa ujenzi imara utakasokekana. Hii ni kweli pia katika muktadha wa uwiano wa bajeti ya maendeleo na ile ya matumzi ya kawaida. 

Hitimisho
Kama ilivyo katika bajeti nyingine zilizopita, ni jambo moja kuwa na bajeti na ni jambo jingine kuitekeleza. Kwa miaka kadhaa iliyopita imekuwa kawaida kwa fedha zinazotengwa kutotolewa na kutotolewa kwa muda na kiasi kinachotakiwa. Kusudi bajeti hii isiwe tarakimu tu katika makaratasi ni muhimu kupata maelezo ya kina kwa nini bajeti za miaka iliyopita hazikutekelezeka kwa asilimia 100. Muhimu zaidi ni kueleza nini kilifanywa kuhakikisha kuwa bajeti zinatekelezeka.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: