Dk Shukuru Kawambwa
Katika siku za hivi karibuni, Serikali imekuwa ikijigamba kuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Majigambo hayo yametolewa kwa nyakati tofauti na
mamlaka mbalimbali za Serikali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete aliyesema
kuwa Serikali yake inajivunia maendeleo katika sekta ya elimu. Hata jana, Bunge la bajeti linaloendelea mjini
Dodoma lilielezwa kuwa sekta hiyo imefanikiwa kwa asilimia 81 na hivyo
kushika nafasi ya kwanza ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Awali, Rais Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa
katika Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), uliofanyika
jijini Arusha Mei 28, alisema Serikali yake inajivunia mafanikio makubwa
katika sekta ya elimu, licha ya kwamba bado zipo changamoto zinazopaswa
kufanyiwa kazi.
Alielezea mafanikio hayo kuwa ni pamoja na
uanzishwaji wa programu za walimu wa kozi za muda mfupi au walimu wa
leseni, ongezeko la kiwango cha uandikishaji wanafunzi, ujenzi wa
maabara na kuondoa utitiri wa vyombo vya kuhudumia madai ya walimu. Pamoja na mafanikio haya, ni ukweli usio na shaka
kuwa uanzishwaji wa programu za kozi za muda mfupi za ualimu, ni sababu
mojawapo ya kushuka kwa kiwango cha elimu nchini. Hili limekuwa
likilalamikiwa mara kwa mara na wadau wa elimu.
Kimsingi, Watanzania hawajasahau makovu waliyoyapata kutokana na walimu wa UPE na wale wa ‘vodafasta’. Katika risala yao, walimu hao walipendekeza mambo tisa ambayo walitaka Serikali iyafanyie kazi ili kuboresha sekta ya elimu.
Baadhi ya mambo hayo waliyoyatoa kama wito kwa
Rais Kikwete ni kufanyia mabadiliko ya mafao ya pensheni, uboreshwaji wa
idara za ukaguzi wa shule na urejeshwaji wa posho za kufundishia.
Hata hivyo, wakati Rais Kikwete na mamlaka
nyingine za Serikali zikieleza mafanikio hayo, Kamati ya Bunge ya Huduma
za Jamii imesema hadi kufikia Machi, baadhi ya taasisi zilizopo chini
ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zilikuwa hazijapata hata fedha
za maendeleo.
Kamati hiyo imeeleza pamoja na kuwapo kwa takwimu
za mafanikio, wanafunzi bado wanakaa chini kwa kukosa madawati, bado
kuna uhaba wa walimu, madarasa na vifaa vya kufundishia, huku karo
katika shule binafsi zikiendelea kuwa juu.
Matatizo hayo ndiyo yaliyoifanya kambi rasmi ya
upinzani bungeni kuhoji aina ya uwekezaji uliofanyika katika sekta ya
elimu hadi ikafikia mafanikio makubwa ya kujivunia kama inavyoelezwa na
mamlaka hizo za Serikali. Kwa mfano, kambi hiyo inazungumzia kilio cha walimu cha
malimbikizo ya mishahara na stahili zao nyingine, ikisisitiza kuwa
walioajiriwa Mei Mosi, 2015 mpaka sasa hawajalipwa fedha zao za
kujikimu.
Kambi hiyo pia imeikosoa sera mpya ya elimu
iliyozinduliwa na Serikali hivi karibuni, ikisema haiwezi kufanikiwa,
huku ikieleza mambo matatu yanayoweza kuifanya ifanikiwe kuwa ni kuwapo
kwa walimu bora, zana bora za kufundishia na walimu wenye motisha.
Ni kweli kuwa si sahihi kusema kwamba Serikali
haijafanya kitu katika sekta ya elimu, lakini tunachokiona sisi ni kuwa
ilichofanya hakijatosheleza.
Ukweli ni kuwa sekta ya elimu bado inakabiliwa
changamoto nyingi na Serikali inapochukua hatua za kujisifia, ni sawa na
kuwapaka mafuta Watanzania kwa mgongo wa chupa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment