Katibu Mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad akionyesha fomu za kuwania nafasi ya urais wa kisiwa
hicho kupitia chama hicho baada ya kukabidhiwa na Katibu wa chama hicho
wa Wilaya ya Magharibi, Saleh Muhammed Saleh. Kulia ni Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho, Duni Haji.
Katibu Mkuu wa CUF
Maalim Seif Sharif Hamad amerudisha fomu ya kuwania nafasi ya urais wa
Zanzibar kupitia chama hicho na kusema anajisikia raha kuwa mgombea
pekee akiwa na dhamira ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuwatumikia
Wazanzibari.
Alisema hayo jana baada ya kukabidhi fomu hiyo kwa
Katibu wa Wilaya ya Magharibi A, Saleh Mohammed Saleh katika hafla
iliyohudhuriwa na waziri wa zamani wa SMZ, Mansour Yussuf Himid.
“Ninajisikia raha kuwa mgombea pekee katika chama
kwa sababu lengo langu ni kuwatumikia wananchi wa Zanzibar,” alisema
Maalim Seif.
Maalim Seif alisema mwanachama yeyote wa CUF kwa
mujibu wa katiba ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, lakini wanachama
wamekuwa hawajitokezi wakiamini ana sifa na uwezo wa kuleta mabadiliko
Zanzibar.
Hata hivyo, alisema ili uchaguzi uwe huru na wa
haki, Tume ya Uchaguzi Zanzibar lazima ihakikishe kazi ya uandikishaji
wapiga kura inafanyika vizuri.
Alisema pamoja na Sekretarieti ya Tume kutokuwa na
mabadiliko yoyote, utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
utapimwa katika uandikishaji wa wapiga kura unaotarajiwa kuanza leo
Kisiwani Pemba. Alisema matukio ya watu kupigwa mawe wakitoka kwenye
mikutano na kuzuia mikutano ya hadhara, ni kinyume na misingi ya amani
na utulivu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment