Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Asha-Rose Migiro
Hotuba ya Waziri ya Katiba na Sheria ililenga kutoa bajeti kwa wizara hii na taasisi zake.
Utekelezaji bajeti ya 2014/2015
Utekelezaji bajeti ya 2014/2015
Kama ilivyo katika bajeti nyingi za miaka
iliyopita, kumekuwapo na pengo kubwa kati ya fedha zilizohidhinishwa na
Bunge na zile zilizotolewa. Kufikia Aprili 2015, fedha zote
zilizopokelewa na wizara ni sawa na asilimia 46.5 tu ya bajeti
iliyoidhinishwa ya Sh234.25 bilioni. Sh64.85 bilioni zilitolewa kwa
matumizi mengineyo na Sh1.15 bilioni zikiwa ni fedha za maendeleo kutoka
nje. Kinachojitokeza hapa ni upungufu wa fedha katika bajeti, na la
muhimu ni kuelewa kwanini hili linatokea. Kuna umuhimu wa kupanga bajeti
kulingana na uwezo wa makusanyo, hili lisipofanyika hatutaepuka bajeti
zisizotekelezeka.
Bajeti 2015/2016
Katika mwaka wa fedha 2015/2016, wizara
itaimarisha huduma zake ili kukidhi dhima ya kukuza utawala wa sheria,
haki na usawa kwa kutoa huduma bora na kwa wakati. Ili kufikia azma
hiyo Wizara itaelekeza rasilimali zake katika maeneo sita ya kipaumbele
ambayo ni Mabadiliko ya Katiba; mfumo wa sheria na utoaji haki; hifadhi
ya haki za binadamu na utawala bora; usajili wa matukio muhimu ya
binadamu; ushauri wa kisheria na kuiwakilisha Serikali katika masuala ya
kisheria na kuimarisha mifumo ya kitaasisi.
Maombi ya fedha 2015/2016
Ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake
katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara iliomba kuidhinishiwa Sh223.87
bilioni kwa ajili ya wizara na taasisi zake. Kiasi hiki ni Sh10.38
bilioni (asilimia 4.4) pungufu ya zile ya mwaka 2014/15.
Ni vizuri bajeti ya mwaka huu imepunguzwa
ukilinganisha na ile ya 2014/15, hata hivyo swala la mjadala ni kuwa
kupunguzwa huku hakuendani na uhalisia wa mwaka 2014/15. Upungufu wa
fedha hadi kufikia Aprili 2015 ulikuwa asilimia 55.4.
Juhudi za ziada
Ili kupata fedha za kukidhi bajeti ya 2015/16 ni
vyema kujiuliza na kujibu ni jambo gani jipya litafanyika mwaka huu wa
fedha ili kupata fedha hizi za ziada? Kiuhalisia, inaonyesha uwezo ni
kupata asilima kama 46 tu ya fedha zilizopangwa. Ili kufikia asilimia
100 itabidi ziwepo juhudi za ziada kuongeza mapato. Katika mwaka huu wa
uchaguzi, wanasiasa hawatapenda kuwabebesha wapiga kura mzigo mkubwa
zaidi wa kodi. Pia ukizingatia kuwa lengo la bajeti kuu kwa mwaka
2015/16 ni kupunguza utegemezi wa nje kutoka asilimia kama 14 hadi
asilimia kama 8 tu ya bajeti yote, kupata kiasi cha fedha kilichoombwa
katika bajeti hii itakuwa kazi ngumu.
Mgawanyo fedha za bajeti
Kati ya Sh223,87 bilioni za bajeti ya 2015/16, kiasi cha Sh197.8
bilioni (asilimia 88.4) ni kwa matumizi ya kawaida zikiwamo Sh68.8
bilioni kwa ajili ya mishahara na Sh128.99 bilioni kwa matumizi
mengineyo.
Fedha za Maendeleo ni Sh26.06 bilioni ambayo ni
sawa na asilimia 11.6 tu. Kati ya hizo Sh24 bilioni sawa na asimilia
10.7 tu ya bajeti yote ni fedha za ndani na Sh2.06 bilioni za nje.
Ni wazi kuwa kiwango cha fedha kwa ajili ya
maendeleo ni kidogo sana. Kwa kiwango cha asilimia 10.7 tu ya bajeti
yote kama fedha za ndani zitakazokwenda katika maendeleo na ukizingatia
kuwa kuna uwezekano wa kutokupatikana kiasi hiki cha fedha kama
ilivyokuwa katika bajeti nyingine, hivyo uwezekano wa kuwapo shughuli za
maana za maendeleo katika wizara na taasisi zake ni mdogo.
Bajeti ya kimaskini
Katika bajeti kuu ya nchi kwa mwaka 2015/16 lengo
ni kuwa asilimia kama 25 ya bajeti iende katika shughuli za maendeleo.
Asilimia hizi 25 ni ndogo. Hivyo basi, asilimia 11.6 kwa shughuli za
maendeleo ya wizara hii ni ndogo kwa viwango vyovyote vile. Hii
inaonyesha kile nadharia za uchumi inachoona kuwa ni hali halisi ya
mipango na bajeti za watu na nchi maskini.
Maskini huwekeza kidogo katika maendeleo na kiasi
kikubwa katika matumizi ya kawaida. Matokeo yake ni mzunguko wa umaskini
unaotokana na kutokuwa na uwezo wa kuwekeza katika maendeleo na matokeo
yake ni kuwa maskini kwa sababu tupo maskini.
Makusanyo ya maduhuli ya Serikali
Katika mwaka wa fedha 2015/2016 wizara inatarajia
kukusanya Sh17.02 bilioni ikiwa ni maduhuli ya Serikali, sawa na
asilimia 7.6 u ya bajeti nzima ya wizara. Hili sio jambo la ajabu kwa
sababu wizara hii kama zinavyotakiwa kuwa wizara nyingine, si vitega
uchumi vya kuingiza mapato serikalini bali sehemu ya kutoa huduma.
Hitimisho
Kama ilivyo katika bajeti nyingne zilizopita, ni
jambo moja kuwa na bajeti na ni jambo lingine kutekeleza bajeti husika.
Kwa miaka kadhaa iliyopita imekuwa kawaida kwa fedha zinazotengwa
kutokutolewa na kutopatikana kwa muda na kwa kiasi kinachotakiwa. Ili
bajeti hii isiwe tarakimu tu katika makaratasi, ni muhimu kupata maelezo
ya kina kwanini bajeti za miaka iliyopita hazikutekelezeka kwa asilimia
100.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment