Social Icons

Pages

Thursday, May 28, 2015

MATUKIO YA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI YAZIDI KUKITHIRI NCHINI

Jaji Mstaafu, Amir Manento akikata utepe kuzindua Taarifa ya Haki za Binadamu ya Mwaka 2014, Dar es Salaam jana na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba.
Kituo cha Haki za Binaadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), kimewasilisha ripoti ya mwaka 2014 inayoonyesha kuongezeka kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayosababishwa na baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi na mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola.
Mapema, akizindua ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam , Jaji Mkuu mstaafu, Amir Manento alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mikataba ya kimataifa ya kufuata na kutekeleza masuala yote ya haki za binadamu. “Inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zote zinazowagusa moja kwa moja wananchi, zinazokiuka haki zao za msingi,” alisema.
Alisema ripoti hiyo imebainisha kuwa matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayosababishwa na imani za kishirikina zinazochochea matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe, katika baadhi ya maeneo nchini.
Manento alisema matukio ya watu wenye hasira kali kujichukulia sheria mkononi na kuua watu wanaotuhumiwa kutenda makosa mbalimbali yakiwamo ya wizi, yanaongezeka ikilinganishwa miaka ya nyuma.
Mwaka 2005, watu 206 waliripotiwa kuuawa na watu wanaodaiwa kuwa na hasira kali na mwaka 2007, matukio 263 yaliripotiwa wakati mwaka 2011 yalifikia 673, huku mwaka 2014 mpaka kufikia Juni, 2014, matukio 473 yaliripotiwa.
“Hali hii ya kuongezeka kwa matukio ya kujichukulia sheria mkononi inaonyesha kwamba wananchi hawana imani tena na vyombo vya dola na mfumo wa upatikanaji wa haki hususan mahakama,” alisema.
Alisema mpaka sasa jumla ya watu 410 wako gerezani baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo, kati ya hao, 186 walikata rufaa dhidi ya adhabu hiyo na kushindwa, 209 bado wanasubiria kesi zao ziamuliwe katika Mahakama ya Rufani.
Mwakilishi kutoka LHRC, Paul Mikingoti alisema kukithiri kwa vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, kunaendelea kuathiri ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi nchi.
Akizungumzia adhabu ya kifo, Mikingoti alisema imeendelea kutolewa mahakamani na tangu nchi ipate uhuru, wafungwa 238 wameshanyongwa.
Alisema katika kipindi cha miaka 20 wa utawala wa marais, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, hakuna adhabu iliyotekelezwa na mwaka 2005 wafungwa 500 walipunguziwa adhabu hiyo na kuwa ya kifungo cha maisha.

Mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola
Mikingoti alisema matukio hayo yanaongezeka na kupungua katika vipindi tofauti. Alitolea mfano mwaka 2003, matukio 10 yaliripotiwa wakati 2004 yaliripotiwa saba.
“Mwaka 2006 yaliripotiwa matukio ya watu 36 kuuawa, huku mwaka 2010 ndiyo mwaka ambao matukio mengi zaidi yaliwahi kuripotiwa kwani watu 52 walipoteza maisha mikononi mwa polisi, mwaka 2013, watu 23 waliuawa kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili, mwaka 2014 takwimu za mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola hazikupatikana,” alisema Mikongoti.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa Tanzania inaongoza barani Afrika kwa matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino). Toka mwaka 2008 mpaka 2010, jumla ya watu 75 waliuawa, ikimaanisha kwamba kila mwezi takriban watu watatu walikuwa wakiuawa.
Ripoti pia imebaini kuendelea kukithiri kwa matukio ya ubakaji. Mwaka 2008 kulikuwa na matukio 196, lakini mwaka 2014 kwa nusu mwaka pekee, matukio 3,074 yaliripotiwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Hata hivyo, Mikingoti alisema changamoto kwenye ubakaji bado ipo katika ukimya wa waathirika na jamii kwa ujumla. “Na hata wanaojitokeza kuyaripoti, bado hushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi hizo.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Helen Kijo Bisimba alisema Serikali inapaswa kuhakikisha elimu ya haki za binadamu inatolewa kwa kina na kwa ngazi zote.
Alisema pia ihakikishe inawachukulia hatua kali wale wote wanaokiuka ili liwe fundisho kwa jamii inayowazunguka.
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Harusi Miraj Mpatani alisema kwa upande wa Zanzibar, bado kuna upungufu mkubwa wa utekelezaji wa haki za msingi za binadamu.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: