Social Icons

Pages

Thursday, May 28, 2015

JAMES MBATIA: MWENYEKITI WA NCCR-MAGEUZI



James Mbatia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi
Alianza elimu yake mwaka 1973 katika Shule ya Msingi Iwa – Kirua, Vunjo na kuhitimu mwaka 1979. Aliendelea na masomo kuanzia mwaka 1983 kwenye Shule ya Sekondari Tambaza, Dar es Salaam na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1986.
Historia yake

James Mbatia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alizaliwa Juni 10, 1964, Vunjo mkoani Kilimanjaro (atafikisha miaka 51 Juni mwaka huu).
Alianza elimu yake mwaka 1973 katika Shule ya Msingi Iwa – Kirua, Vunjo na kuhitimu mwaka 1979. Aliendelea na masomo kuanzia mwaka 1983 kwenye Shule ya Sekondari Tambaza, Dar es Salaam na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1986.
Kumaliza kidato cha nne kulimpeleka katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Kilimanjaro ambako alisoma kidato cha tano na sita kati ya mwaka 1980 – 1983.
Mwaka 1987 alianza masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akisomea uhandisi ujenzi, lakini mwaka 1992 alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofukuzwa chuoni, tena akiwa anaelekea kukamilisha masomo yake kutokana na mgomo uliokuwa na ajenda nzito za kudai masilahi makubwa ya wanafunzi ambao ulisababisha wanafunzi kutoa maneno ya kejeli na utani kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Kiu ya Mbatia kujiendeleza kielimu ilirejea baada ya miaka tisa, mwaka 2001 alijiunga UDSM na kupata Cheti cha Juu cha Kompyuta, miaka sita baadaye akaelekea Uholanzi na kuanza shahada ya kwanza ya Uhandisi wa Mazingira na Ujenzi (kwa tafsiri yangu) katika Chuo Kikuu cha Hanze na pia akiwa hapo chuo kikuu akafanikiwa kusoma Stashahada ya Uhandisi na Usimamizi wa Ujenzi wa Kimataifa (pia kwa tafsiri yangu). Amesoma shahada hizi kati ya mwaka 2007 – 2009.
Alipofukuzwa UDSM mwaka 1992, alijiunga na vuguvugu la mabadiliko ya demokrasia nchini na akawa mmoja wa waasisi wa NCCR – Mageuzi na akawa mwenyekiti wa kwanza wa vijana wa chama hicho mwaka 1992 – 1994 na tena mwaka 1994 hadi 2000 akakitumikia chama chake akiwa Katibu wa Idara ya Oganaizesheni na Uchaguzi na mwaka 2000 alichaguliwa kuwa mwenyekiti, wadhifa ambao anautumikia hadi leo. Mbatia ameoa na ana watoto.

Mbio za ubunge
Mwaka 1995 katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi, Vunjo ilichagua mbunge kutoka NCCR Mageuzi, huyu si mwingine – Mbatia huyuhuyu ninayemjadili hapa. Mbatia, wakati huo akiwa kijana wa miaka 31 tu, alichaguliwa kuongoza jimbo hili akiwa na machungu ya kufukuzwa UDSM.
Alipata ushindi mkubwa mno, asilimia 83.9 (kura 57,714) huku mgombea wa CCM, Msaki Leonard akipata asilimia 9.4 (kura 6,468). Kama kuna majimbo ambayo CCM ilishindwa kwa kila kitu mwaka 1995, basi Mbatia alikuwa mmoja wa watu waliopeleka kilio hicho. Alipangua wagombea wa vyama vingine sita wakiwa watu wazima na wazoefu, ilishangaza sana.
Sokomoko ndani ya NCCR Mageuzi lilidhoofisha siasa za siku za mbele za Mbatia katika Jimbo la Vunjo. Augustine Mrema alipohamia TLP bado alikuwa na ubavu wa ushawishi hivyo akampigia debe mgombea wa TLP badala ya Mbatia wa NCCR. Kutopigiwa debe na Mrema pale Vunjo mwaka 2000 kuliathiri safari ya kisiasa ya Mbatia na aliangushwa kwenye uchaguzi huo na mgombea wa TLP, Jesse Makundi ambaye aliongoza Vunjo tokea mwaka 2000 – 2005.
Baada ya kutogombea ubunge mwaka 2005, Mbatia alirejea kwa nguvu mwaka 2010 akilisaka Jimbo la Kawe, Dar es Salaam. Nguvu ya mwanamama Halima Mdee wa Chadema ilifanya mabadiliko makubwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambao ulikuwa na kila sababu ya kumpeleka Mbatia bungeni. Ilitarajiwa kuwa Mbatia angewashinda kina Angela Kizigha wa CCM na Mdee.
Matokeo ya mwisho hayakuwa mazuri kwa Mbatia, alishika nafasi ya tatu. Wananchi wa Kawe niliozungumza nao wanasema walipenda kumchagua Mbatia lakini wakasisitiza kuwa Mdee alikwishajijenga mno.
Hata hivyo, kiu ya James Mbatia kuelekea bungeni kuwatetea Watanzania ilipata jibu Mei 2012, pale Rais Jakaya Kikwete alipomteua kuwa mbunge na tokea wakati ameendelea na shughuli za kibunge, akiwa mmoja wa Watanzania muhimu katika Bunge linalomalizika hivi sasa na atakumbukwa kwa hoja yake ya “mtalaa wa elimu ya Tanzania” ambao uliifanya Serikali na mawaziri kukosa majibu ya kina.

Mbio za urais
Mbatia hajatangaza kuwa atagombea urais wa Tanzania mwaka huu na kwa kipindi cha nyuma hakuwahi kugombea, ila yeye ni mmoja wa Watanzania wanaotajwa kuwa na sifa na vigezo vya kugombea nafasi hiyo.

Nguvu yake
Sifa na nguvu ya kwanza ya Mbatia ni utulivu. Kati ya viongozi ambao wana uwezo mkubwa katika eneo hili hapa Tanzania ni pamoja na yeye. Utulivu huu unaambatana na busara na kufanya uamuzi kwa kufuata taratibu zinazoeleweka. Mara kadhaa amekuwa akipenda kujenga hoja bila kupiga kelele na huku akitoa suluhisho na masuala anayotaka yarekebishwe kwa mifano dhahiri na bila kuacha maswali hewani. Sifa hii inasakwa na marais wengi duniani na hadi leo hawajaipata.
Pili, Mbatia ni mtu mwenye fikra za ujana na vijana. Mara nyingi huzungumzia masuala kwa kuangalia mustakabali wa vijana na kutoligawa Taifa. Anaweza kuhutubia mkutano mwanzo hadi mwisho bila kutaja chama chake NCCR, kila mara anahubiri umoja, maridhiano na mshikamano. Mtindo wake wa siasa unaweza kuwa wa kuigwa na wanasiasa wa upinzani na hata kutoka CCM ambao hutumia muda mwingi kusifia vyama vyao na kusahau sera na mahitaji ya Taifa. Akikutana na vijana, huanzisha mijadala na kuwasikiliza, kisha hawezi kuondoka kabla ya kushauri nini suluhisho la matatizo yao. Nchi kama Tanzania inahitaji watu wa namna hii.
Jambo la pili, Mbatia hapendi vurugu, chokochoko na mambo yasiyofaa kidemokrasia. Ukimfuatilia awapo bungeni, awapo mikutanoni na hata katika mazungumzo ya kawaida, utamjua kuwa anayaishi maisha ya amani, upendo na umoja. Nimewahi kushuhudia akiahirisha mkutano wa NCCR kwa sababu tu Polisi walitaka kuleta vurugu, Mbatia alisisitiza kuwa mikono yake haiwezi kutumika kumwaga damu. Je, ni wanasiasa wangapi hapa Afrika wanaingia ikulu bila vurugu, kumwaga damu na machafuko?
Tatu, Mbatia ni mtu anayeweza kujenga jambo hadi likafanikiwa. Baada ya kuyumba kwa NCCR kutokana na kuondoka kwa Mrema ambaye alielekea TLP, watu wengi walidhani kuwa NCCR inakufa au imekufa. Uongozi wake na mipango yake isiyo na mbwembwe, hatimaye ilikiibua chama chake na wabunge zaidi ya wanne Tanzania Bara kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Haya ni mafanikio makubwa.
Kwa wasiofahamu, katika demokrasia ngumu ya nchi hii ambayo chama kinachoongoza dola na Serikali yake vina udhibiti wa moja kwa moja kwenye tume ya uchaguzi, si jambo jepesi kwa chama kupata mbunge hata mmoja. Mbatia amepambana na hivi sasa chama chake kinakwenda mbele zaidi. Haya ni mafanikio makubwa na mfano bora wa kiongozi ambaye anaweza kukabidhiwa nchi akaweka mipango yake chini na kuleta mabadiliko.
Lakini jambo la mwisho, Mbatia ni mwanasiasa asiyekata tamaa. Alipofukuzwa UDSM, hakurudi nyuma, alipambana na kuwa mbunge kwa kipindi kimoja, hata alipokosa ubunge kwa kipindi cha pili alizidi kukiimarisha chama chake na baadaye akaelekea ughaibuni kuanza shahada ya kwanza huku umri ukizidi kumtupa mkono. Safari yake ya kisiasa ina kila jambo la kujifunza hasa kwa vijana wa sasa ambao wakifukuzwa tu chuo kesho yake wanapanga foleni kwa watawala kutafuta msamaha ili maisha yao yaende. Mtu asiyekata tamaa pia anahitajika katika kurekebisha nchi yetu akiwa pale ikulu.

Udhaifu wake
Jambo moja kubwa ambalo naamini kuwa ni udhaifu wa Mbatia ni kupenda mazungumzo hata katika masuala yanayohitaji msimamo mkali. Kupenda mazungumzo ‘dialogue’ ni sifa kuu ya kiongozi yeyote mzuri, lakini mazungumzo hayo lazima yawe na ukomo. Mbatia anaamini katika mazungumzo na anasahau kuwa kwa siasa za Afrika, inabidi uamini katika mazungumzo ya mezani kwa nusu na nguvu ya wananchi kwa nusu. Serikali ikikusumbua mezani unahamia kwa wananchi, naamini huu ni mtihani mkubwa kwa Mbatia. Hata pale Ikulu tunahitaji Rais ambaye atazungumza na akiona ‘anazinguliwa’ anaondoka kwenye mazungumzo hadi atakapoelezwa kujiunga na mazungumzo yenye tija zaidi.
Lakini jambo jingine, ni uungwana uliopita kiasi. Ili nchi iwe salama inahitaji kiongozi muungwana lakini asiwe muungwana kupita kiasi. Mbatia ni muungwana kupita kiasi na watu wa namna yake huwa wanakuwa na matatizo ya kudhibiti watu wanaowaongoza. Nadhani tatizo hili la uungwana kupita kiasi ndilo linafanya leo unaweza kuona viongozi wa vijana wa NCCR wakitoa matamko mbalimbali ya kusemea Ukawa, au kushauri umoja huo hadharani kwa masuala ambayo walipaswa kumpelekea mwenyekiti wao mezani au vikaoni. Naamini haya yanatokea kwa sababu ya uungwana wa Mbatia, kwamba amekuwa hivyo hadi vijana wake wanaingilia masuala ambayo angeyasemea yeye au viongozi wa juu wa chama chake.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Sababu ya kwanza inayoweza kuifanya NCCR impendekeze kuwa mgombea urais wa chama hicho na hatimaye Ukawa ni uzoefu wa ndani ya NCCR na demokrasia ya vyama vingi kwa ujumla. Kati ya Watanzania walioshiriki moja kwa moja “ladha” ya mageuzi nchini ni pamoja na Mbatia. Tangu akiwa kijana mdogo alishiriki kwenye vuguvugu lote la uanzishwaji wa vyama na akawa kiongozi wa vijana hadi kuwa kiongozi wa Taifa. Kwa NCCR ya sasa naamini hakuna mwanachama mwenye uzoefu wa chama hicho kuliko yeye na huu ni msingi mkubwa kwa NCCR kuweza kumkabidhi kijiti hicho.
Pili, anaweza kuwa mgombea muhimu katika hesabu za kisiasa ikiwa NCCR inataka kumuweka katika viwango vya kushindanishwa ndani ya Ukawa, ikiwa NCCR itapeleka mtu ambaye hafahamiki vizuri au hajajijenga vizuri kisiasa, anaweza kushindwa mapema kwenye mchujo wa ndani ya Ukawa kwa sababu nafahamu kuwa kuna viongozi wenye historia nzito za kisiasa kutoka vyama vingine vinavyounda umoja huo.
Tatu, NCCR inaweza kumpitisha na Ukawa, kugombea urais kwa sababu yeye ni muasisi wa umoja huo. Moja ya viongozi mahiri na mhimili wa Ukawa ni pamoja na Mbatia. Ameshiriki kwenye hatua zote za uanzishwaji wa umoja huo, chama hicho kinaweza kuwa na kila sababu ya kumvusha kwani akipewa nafasi hiyo ya juu kabisa atakuwa na uwezo na ufahamu mzuri wa kuunganisha vyama vinavyoshiriki kwenye umoja na labda kuongoza Serikali itakayoundwa kwa ufanisi na utaratibu (Ikiwa Ukawa itashinda uchaguzi wa Oktoba)

Nini kinaweza kumwangusha?
Mambo kama matatu yanaweza kuifanya NCCR isimpitishe katika kusaka tiketi ya urais wa nchi kupitia chama hicho na hatimaye ukawa:
Mosi ni ikiwa mwana NCCR mwingine mwenye sifa, uwezo na vigezo atajitokeza na kuonekana kuwa kwa mahitaji ya sasa anaweza kuwa na nguvu na ushawishi kwa wapigakura kuliko Mbatia. Tayari mmoja wa makada wa chama hicho na Mhadhiri wa UDSM, Dk George Kahangwa amekuwa akipigiwa chapuo na viongozi wa vijana wa chama hicho. Ikiwa Dk Kahangwa ataonekana kuwa anakidhi vigezo, sifa na mahitaji ya sasa kuanza kutangazwa, Mbatia anaweza kuwekwa pembeni ili kupisha damu changa zaidi kupasha mazoezi ya urais.
Lakini jambo la pili, nafasi ya Mbatia itakosekana “automatically” ikiwa Ukawa itaamua kumpitisha mgombea urais kutoka Zanzibar. Ikiwa Mzanzibari ndiye atakuwa mgombea wa umoja huo, ataikosa sifa hiyo moja kwa moja na atapaswa kushirikiana na mteuliwa kutoka upande huo wa pili wa Muungano kutafuta ushindi wa umoja huo.
Lakini jambo la tatu linaloweza kumwengua moja kwa moja ni ikiwa chama kingine ndani ya Ukawa kitapewa jukumu la kutafuta rais. Jambo hili nalo linaweza kutokea kwa sababu hadi sasa Ukawa haijatangaza itatumia vigezo gani kumpata mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Asipochaguliwa (Mpango B)
Mbatia atakuwa na mambo kadhaa ya kufanya ikiwa hatapitishwa na NCCR na Ukawa kugombea urais wa nchi:
Kwanza nadhani ataendelea na mpango wake wa kugombea ubunge katika Jimbo la Vunjo, mahali ambako aliwahi kuwa mbunge kuanzia mwaka 1995 – 2000. Mipango ya Mbatia kurejea Vunjo ameifanya kwa muda mrefu sasa na tayari mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Augustine Mrema amekwishamshtaki kwa Rais Kikwete na kwa Spika na wabunge, akihitaji kusaidiwa ili asiporwe jimbo lake. Ikiwa Mbatia atagombea ubunge wa Vunjo na kushinda na endapo Ukawa itashinda katika uchaguzi huo, atakuwa mtu muhimu katika Serikali ijayo. Pia, hata kama umoja huo hautashinda, atakuwa mmoja wa wabunge machachari.
Pili, kwa sababu Mbatia ni mfanyabiashara, nadhani atakuwa na muda wa kutosha kuendelea kusimamia biashara zake huku pia akijipa muda wa kufanya shughuli za kitaalamu zikiwamo za kutoa ushauri kwa kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi katika eneo alilobobea. Lakini pia atakuwa na kazi ya kuendelea na uongozi wake ndani ya NCCR ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2019.

Hitimisho
Mbatia ni moja ya nguzo kubwa za kidemokrasia hapa nchini. Mwanasiasa huyu amekuwa akivutia kumsikiliza anavyojenga hoja kwa mifano na kumbukumbu. Akiwa anazungumza anakutajia tukio la mwaka 1950 na tarehe, mwezi, siku na saa. Ni mtu anayejisomea na kutunza sana kumbukumbu na huwezi kumdanganya kirahisi.
Hata hivyo, yeye na chama chake kwa ujumla wanakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka chama kipya cha ACT –Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe, ikumbukwe kuwa ACT kimeutangaza Mkoa wa Kigoma kama moja ya ngome zake muhimu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kuna tetesi kuwa baadhi ya wabunge wa NCCR wanaweza kuhamia katika chama hicho kipya (japokuwa wabunge wote wa NCCR wamekuwa wakikana kuwa na mpango huo).
Ikiwa ACT kitakuwa na nguvu kubwa Kigoma (mkoa ambao ni ngome ya NCCR kwa sasa), ni jambo la wazi kuwa NCCR itaumizwa na huenda Mbatia akawa kwenye na kazi kubwa na mpya ya kuanza tena ujenzi wa chama chake katika majimbo mengine. Pamoja na yote haya, namtakia mwanasiasa huyu kila la heri kwenye safari yake.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: