Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Wabunge wameishukia serikali kwa kushindwa kutatua
tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam ambalo sasa linaigharimu
serikali hasara ya Sh. bilioni nne kila siku.
Aidha, wameitupia lawama Wizara ya Ujenzi kwa kusababisha vifo vya
makandarasi wanne ambao walifikwa na umauti huo kutokana na serikali
kushindwa kuwalipa madeni wanayodai. Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia, akichangia bajeti ya
Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2015/2016, alisema tatizo la msongamano wa
magari katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa sugu bila kuwapo mipango
yoyote ya serikali katika kulipatia ufumbuzi.
Alisema Januari 13, mwaka 2009, alimwandikia barua Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, kuhusu tatizo la msongamano wa magari na kutoa
mapendekezo 10 ambayo yangesaidia kukabiliana na tatizo hilo, lakini
bahati mbaya hakuna kilichofanyika hadi sasa hali inayoonyesha serikali
kutokuwa makini katika kushughulikia mambo ya msingi.
Mbatia alisema moja ya mapendekezo hayo ni kuitaka serikali
isimamishe au kutoendelea kutoa vibali vya kujenga ofisi, maduka makubwa
na madogo katikati ya Jiji.
Alisema pendekezo lingine lilikuwa ni kutaka Ofisi za Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara
ya Ulinzi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Wizara ya Ujenzi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Makao Mkuu ya Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na uwanja ndege vihamishwe katikati ya
Jiji. “Hali ni mbaya Dar es Salaam, watu wanakaa kwenye foleni kwa zaidi
ya saa nane, foleni hii inaigharimu serikali zaidi ya Sh. bilioni nne
kwa siku ambazo zingetumika kujenga zahanati na kununua madawati ambayo
yangesaidia watoto shuleni,” alisema.
Alisema Sh. bilioni nne ambazo serikali inapata hasara kila siku
kutokana na foleni zingetumika kununua madawati 80,000 kwa bei ya Sh.
50,000 kwa dawati moja. Mbatia alisema pia fedha hizo zingetumika kujenga vituo viwili vya
afya vya kisasa, ambavyo gharama zake kila kimoja ni Sh. bilioni mbili.
Aliongeza kuwa Waziri Mkuu aliahidi kuunda Kamati ambayo
ingeshughulikia tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam, lakini
hadi sasa hakuna kilichofanyika. Mbatia alisema Waziri Magufuli awe mkweli kwani kimsingi, hali ya
sekta ya barabara ni mbaya na mwanzoni mwa mwezi huu serikali ilitoa
taarifa kwamba wapo makandarasi wanne wamepoteza maisha kutokana na
kutolipwa madeni wanayoidai serikali.
Alisema serikali ihakikishe inalipa madeni makandarasi ambayo
yamefikia zaidi ya Sh. bilioni 850 kabla serikali ya awamu ya nne
haijaondoka madarakani. “Inashangaza fedha za ujenzi wa barabara zinapelekwa BVR (vifaa vya
uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki), wakandarasi
wamefariki dunia kwa kutolipwa halafu watu wengine wanafurahia,
mnashabikia mauaji,” alisema.
Alisema barabara zinazojengwa nyingi zinakuwa chini ya kiwango na
kutolea mfano za Mkoa wa Kigoma ambazo licha ya kwamba zimejengwa hivi
karibuni, lakini zimebaki kama mahandaki katika baadhi ya wilaya.
Alisema viongozi wakuu wanatumia ving’ora tu kwenda huku na kule, lakini hakuna kinachofanyika. Kadhalika, Mbatia alihoji sababu za serikali kuweka bandari kavu
katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Pwani kwa lengo la kuondoa msongamano
katika jiji hilo.
MCHUNGAJI MSIGWA
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msingwa, alisema
tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam linatokana na kukosekana
‘master plan’ na pia barabara zinajengwa baada ya miezi minne, lakini
zinahabirika kutokana kujengwa chini ya kiwango.
Aidha, Mchungaji Msigwa alimshukia Waziri Magufuli kwamba amenunua
kivuko kibovu kwa gharama kubwa ambacho kinafanya safari zake kati ya
Dar es Salaam na Bagamoyo. Alisema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 300 na kila abiria
hutozwa nauli ya Sh. 1,500 na kupatikana Sh. 450,000, hivyo
kinaendeshwa kwa hasara kwani gharama za kuweka mafuta ni Sh. 2,400,000.
“Hizi suti tunazovaa tusiwadanganye Watanzania, barabara
zinazojengwa hapa nchini zinakuwa za kiwango cha chini sana, kila siku
wabunge tunapata nafasi kwenda nje tunaangalia barabara za wenzetu
zilivyo na ubora,” alisema.
SAID ARFI
Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi, alisema kwa uhai wa
Taifa wa miaka 50 ni aibu hadi sasa hakuna barabara za maana
zilizojengwa na kwamba fedha zinatengwa lakini hazipelekwi na Hazina
katika wizara husika. Alisema tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na
mambo mengine, linasababishwa na magari makubwa ya mizigo yanayobeba
mizigo kutoka bandarini.
PUDENSIANA KIKWEMBE
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi (CCM), Pudensiana Kikwembe,
alisema serikali iangalie uwezo wa makandarasi wanaopewa kazi wasiwe
wenye uwezo mdogo wa fedha ambao wanasubiri hadi walipwe na serikali
ndipo waendelee na ujenzi.
SYLVESTER KOKA
Mbunge wa Kibaha (CCM), Sylvester Koka, alisema changamoto
zinazojitokeza katika Wizara ya Ujenzi zinahitajika wizara kuwa na
mipango ya kudumu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment