Social Icons

Pages

Thursday, May 28, 2015

BAJETI YATENGWA KUONDOA MSONGAMANO BARABARANI DAR


Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.
Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya barabara kuondoa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Lengo la mradi huo ni kujenga, kufanya upanuzi na ukarabati wa barabara zenye urefu wa kilomita 109.35 za jiji hilo ili kupunguza msongamano wa magari. Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, aliliambia Bunge jana wakati akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, wizara hiyo imeomba iidhinishiwe jumla ya Sh. 932,715,351,000.00 kwa ajili ya matumizi ya wizara, kati ya hizo Sh. 42, 142,581,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. 890,572,770,000.00 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Dk. Magufuli alisema katika mwaka huu wa fedha 2015/16, kiasi cha Sh. milioni 245.000 kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobakia kwa barabara za mzunguko wa barabara ya Kawawa –Bonde la Msimbazi –Jangwani/Twiga.
Shilingi milioni 73.000 kwa ajili ya malipo ya mwisho ya mkandarasi wa Barabara ya Ubungo Terminal –mzunguko wa Kigogo na Sh. milioni 523.000 kwa ajili ya malipo ya mkandarasi wa barabara Jet Corner – Vituka – Devis Corner.
Aidha, alisema Sh. milioni 1,013,000 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Tabata Dampo – Kigogo – Kigogo, Sh. milioni 2,026,000 kwa ajili ya barabara ya Mbezi – Malambamawili – Kinyerezi – Banana. Barabara nyingine zilizotengewa kiasi hicho cha fedha ni Tegeta – Kibaoni – Wazo Hill – Goba – Mbezi (Morogoro Road), Tangi Bovu –Goba, na Kimara Baruti – Msewe – Changanyikeni na ujenzi wa barabara ya Kimbamba – Kisopwa (sehemu ya Kibamba – Mloganzila – kilomita 4.0).
Dk. Magufuli alitaja barabara nyingine kuwa ni Banana – Kitunda – Kivule –Msongola (kilomita 14.7).
Alisema mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart) na vituo vyake unaendelea. Alisema kiasi cha Sh. Milioni 20,000 zitatumika kufuatilia na kusimamia ujenzi wa miundombinu ya Dart.
Kuhusu mradi wa Barabara ya Dar es Salaam – Mbagala (Kilwa Road) – Gerezai (Sehemu ya Kamata –Bendera Tatu, kilomita 1.3), alisema lengo la mradi huo utakaogharimu Sh. milioni 2,037.702  ni kukarabati na kupanua barabara ya lami kutoka njia mbili za sasa hadi nje nne kwa msaada wa serikali ya Japan na kuchangiwa na serikali ya Tanzania.
Kwa upande wake, Kamati ya Miundombinu Imelalamikia adha ya matuta makubwa barabarani hasa barabara kuu. Ilisema matuta hayo yamekuwa yakiambatana na matuta madogo madogo yajulikanayo kwa jina la rasta.
“Kamati kwa miaka mitano sasa, imekuwa ikishauri matuta yaliyopo yapunguzwe na kujengwa kwa viwango ambavyo havitaleta madhara na matuta madogo madogo yaondolewe,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof Juma Kapuya, wakati akisoma taarifa ya kamati yake.
Aidha, Kamati hiyo imesema pamoja na kuwapo kwa vituo vingi vya mizani bado barabara zimekuwa zikiendelea kuharibika. Kamati hiyo ilisema changamoto kubwa ya uharibifu wa barabara ni magari makubwa yanayobeba mizigo yenye uzito mkubwa.
“Magari mengi ya aina ya fuso kwa wastani yanatakiwa kubeba mzigo usiozidi tani 3.5 lakini mengi yanazidisha na kubeba hadi tani nane.

CHANZO: NIPASHE

No comments: