Social Icons

Pages

Monday, March 30, 2015

MBUNGE AZILIPUA WIZARA ZILIZOVUKA BAJETI

Mbunge wa Pangani (CCM), Saleh Pamba amezilipua wizara tatu kwa kutumia fedha zaidi ya bajeti iliyotengewa ikiwamo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo ilitengewa Sh35 bilioni lakini ikatumia Sh154 bilioni.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana, wakati akichangia mjadala wa muswada wa Sheria ya Bajeti wa mwaka 2014 iliyopitishwa na Bunge jana.

Wizara nyingine alizozitaja ni Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Nishati na Madini.
Katika mjadala huo wabunge wengine waliopata nafasi ya kuchangia muswada huo wameitaka Serikali ijipange upya na kuja na mikakati thabiti ya kujiongezea mapato ikiwa ni pamoja na kuwabana wafanyabiashara wakubwa walipe kodi ili nchi iache kutegemea wahisani.
Walisema nidhamu ya matumizi ya bajeti kwa Serikali hairidhishi kutokana na ukweli kuwa, taasisi nyingi pamoja na wizara zimekuwa zikitumia fedha bila kujali uzio ulioweka na Bunge (budget fence).
Hata hivyo, Pamba ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti alisema kabla ya mwaka haujaisha wizara hiyo ilitumia Sh154 bilioni kwa safari.
Alisema Wizara ya Ujenzi kwenye bajeti yake ya mwaka 2014/15 ilitengewa Sh445 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara lakini hadi sasa wizara hiyo imevuka kiwango hicho na ina madeni ya Sh998 bilioni.
Wizara ya Nishati, Pamba alisema katika mwaka wa fedha wa 2014/15 walitengewa Sh20 bilioni kwa ajili ya kununulia mafuta machafu ili kuendesha mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL lakini hadi sasa bado hawajamaliza mwaka huo wa fedha, tayari wameshatumia Sh400 bilioni.
Juzi Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, wakati akiwasilisha muswada huo alisema mambo muhimu yaliyozingatiwa ni kubainisha majukumu kati ya Serikali na Bunge ya kiutendaji na usimamizi katika mfumo wa uandaaji na utekelezaji wa bajeti. “Kuweka misingi ya bajeti katika maeneo makuu matatu ambayo ni mipango, mapato na matumizi ya Serikali. Kurasimisha kisheria mzunguko wa bajeti.” alisema.
Alisema mambo mengine yanayozingatiwa katika muswada huo ni kutambua kisheria majukumu ya kibajeti ya Kamati ya Bunge ya masuala ya bajeti na Ofisi ya Bunge. Pia alisema jambo jingine ni kuitambua kisheria kamati ya kitaifa ya uandaaji mwongozo wa mipango na bajeti.
Mkuya alisema, muswada huo unalenga katika kuhusisha masuala ya kibajeti yaliyopo katika sheria mbalimbali za fedha ndani ya sheria hii. “Kuishirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kubainisha hatua za kuchukua kwa atakayekiuka matakwa ya sheria hii,” alisema.
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Fedha, James Mbatia alisema utaratibu wa bajeti kwa sasa hauko wazi. “Hakuna uwazi kwenye bajeti ya mwaka 2014/15 kwamba fedha hizi zitatoka kwenye kasma gani?” alihoji Mbatia.
Michango ya wabunge
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema) David Silinde aliitaka Serikali kuangalia kifungu cha Katiba kinachobana wabunge katika upitishwaji wa bajeti ambapo endapo wabunge hao watagoma kupitisha bajeti, Rais ana uwezo wa kuingilia na kuvunja Bunge na kuitisha uchaguzi mpya.
“Mheshimiwa Spika kifungu hiki cha Katiba kinatubana na ndiyo maana wakati mwingine hata kama bajeti hairidhishi tunalazimika kusema ndiyo ili tu tusiondolewe katika nyadhifa zetu za ubunge,” alisema.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Godluck Ole Medeye (CCM) alisema kuna uhaba wa fedha za kukidhi mahitaji yote ya nchi lakini bado matumizi ya fedha nyingi yamekuwa yakitumika kiholela tofauti na mpango mzima wa bajeti.
“Kumezuka mtindo wa baadhi ya viongozi wa wizara na watendaji wao kuchukua fedha na kutumia katika mambo ambayo hatujayaidhinisha hapa bungeni. Napendekeza fedha za taasisi zisimamiwe na hazina na si wizarani ili zitumike katika maeneo husika,” alisema Ole Medeye.
Mbunge wa Kisesa(CCM), Luhaga Mpina alisema muswada huo ni mzuri lakini hakuna kipengele cha adhabu ambacho kinaonyesha atakayekwenda kinyume atapewa adhabu gani.
“Katika muswada huu hautoi adhabu za mtu ambaye atakwenda kinyume na sheria hii,” alisema Mpina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Biashara na Viwanda.
Omary Nundu (Tanga Mjini-CCM), alisema tatizo kubwa linalohitaji kufanyiwa kazi na Serikali kwa sasa ni eneo la utekelezaji wa bajeti ambalo kwa sasa pamoja na kupitishwa na Bunge kila mwaka halina uhalisia.
Alisema utekelezaji wa bajeti umekuwa hauendani na matarajio, kwani kinachopangwa siyo kinachofanyika na hayatekelezwi ipasavyo. Naye Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisema jambo kubwa linaloisumbua bajeti ya Tanzania ni uhaba wa fedha ndiyo maana mipango mingine inapata fedha na mingine kukosa kabisa.
Aliishauri Serikali kuanza kuweka mikakati ya kujiongezea mapato na si kutegemea wafadhili.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu (CCM) aliitaka Serikali ijikite katika kuongeza mapato ili kuwa na bajeti inayojitegemea lakini pia kugawa fedha za bajeti kwa uwiano tofauti na sasa ambapo kuna baadhi ya maeneo yanapatiwa fedha hadi za ziada na wengine wakipewa pungufu.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: