Rais Jakaya Kikwete akimsikiliza Askofu Zacharia John(kulia) baada
ya mkutano na viongozi wa kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam ,Wa tatu
kushoto ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.
Wakati Rais Jakaya Kikwete
akisema msimamo wa Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) wa kuwataka waumini
wao kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira pia
usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa, baadhi ya maaskofu wameshikilia
msimamo huo.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana katika mkutano
wa kamati ya amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe
kutoka mikoa mbalimbali nchini unaowajumuisha viongozi wa dini za
Kiislamu na Kikristo akilenga kuzungumzia tamko hilo la TCF walilolitoa
Machi 12, mwaka huu.
Katika tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa na mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste
Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet liliwataka waumini wake kujitokeza
kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na
kuipigia kura ya hapana Katiba hiyo.
Jukwaa hilo lilitaja sababu mbili za uamuzi wake huo kuwa ni Muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya Taifa kuwa na Serikali isiyo na dini na Kura ya Maoni kusababisha mgawanyiko. “Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana,” lilisema tamko hilo.
Jukwaa hilo lilitaja sababu mbili za uamuzi wake huo kuwa ni Muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya Taifa kuwa na Serikali isiyo na dini na Kura ya Maoni kusababisha mgawanyiko. “Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana,” lilisema tamko hilo.
Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa 1.16, Rais
Kikwete alianza kwa kuwaomba radhi viongozi hao kwa kuchelewa kwa
akisema alikuwa na majukumu mengi. Mkutano huo ulikuwa uanze saa 3.00
asubuhi lakini Rais Kikwete alifika saa 6.30 mchana.
Alisema “Taifa linapitia hali isiyokuwa ya
kawaida, tusipokuwa makini kuidhibiti itakuwa ni tatizo, ni kazi kubwa
inayohitaji moyo, uvumilivu na viongozi wenye kujali masilahi ya Taifa.”
“Mwelekeo wa mambo hauhitaji uwe bingwa kujua hali
hairidhishi sana na kama hatutachukua hatua hatuwezi kufika na
tutasababisha uvunjifu wa amani za kidini na moto wake ni mkali sana,”
aliongeza Rais Kikwete aliyekuwa akizungumza kwa umakini na taratibu.
Jukwaa la wakristo
Kuhusu tamko la Jukwaa la Wakristo, Rais Kikwete
alisema wakati Taifa likisubiri kuona mchakato wa Katiba unakwenda hatua
za mwisho kumekuwapo na matamko kadhaa ambayo hayakumfurahisha. “Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini,
imenishangaza, imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini
wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete
aliyekuwa akizungumza kwa sauti ya chini wakati wote wa hotuba yake.
“Kinachonisumbua ni kuipa sura na mtazamo wa
kidini Katiba Inayopendekezwa, kama ingekuwa inakinzana na uhuru wa
kuabudu hapo ingekuwa sawa lakini ibara ya 41 inatambua uhuru wa kuabudu
na kuitangaza dini, sasa katika mazingira hayo kuwaeleza waumini
kuikataa inanipa tabu sana,” aliongeza.
Alisema, “Katiba hii imezingatia na kutambua makundi mbalimbali
na mimi sina haya kuwaeleza kuwa tuipitishe kwani licha ya upungufu
ilionao, haifikii hii ya sasa. Tusipoipitisha tutaendelea kuitumia hii
na sidhani kama kuna Rais atakuja na kuanza na mchakato wa Katiba, hivyo
hii hii tuipitisheni kama ina upungufu utafanyiwa maboresho kwani
Katiba siyo Msahafu au Biblia.”
Rais Kikwete anayemaliza muda wake wa uongozi
mwaka huu alisema: “Waacheni waumini waamue Katiba wanayoitaka wao, hayo
matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa Serikali kupeleka bungeni
Muswada wa Mahakama ya Kadhi.”
Katika kujenga hoja hiyo alisema Serikali
imepeleka muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ambao ndani kuna
kifungu kinachohusu Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo siyo geni kwa kuwa
limekuwapo kwa kipindi kirefu. “Tunachotaka kufanya ni kutambua hiki ambacho
Waislamu wamekianzisha kwa kuwa na Mahakama ya Kadhi na makadhi,
Serikali haitawasimamia wala kuziendesha mahakama hizo, hivyo hazina
tatizo lolote,” alisema Rais Kikwete akitanguliza maneno kwamba, “naomba
nitumie lugha ambazo sitowakwaza watu.”
“Siyo kila anachokitaka mtu kitakuwamo katika
Katiba, mfano mimi na CCM tulikuwa na mambo 60 tuliyoyaona ya msingi
sana yawemo katika Katiba lakini sidhani kama yanafika hata 12...kwa
kuwa mchakato unaendeshwa kisheria basi tuuache umalizike kisheria,”
aliongeza.
“Sidhani mnachokifanya ni sawasawa, mnawakwaza
waumini wenu, waacheni waamue wao wenyewe kwani mkiendelea hivyo
watawaona ninyi hamfai kwani kila mtu katika hili ana msimamo wake,
mwingine anaona hili linafaa mwingine anaona halifai.”
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa
Dar es Salaam, Sheikh Alhadi Mussa Salum ambaye pia ni Sheikh wa mkoa
huo, alisema wameamua kumwalika Rais Kikwete kuzungumzia na viongozi hao
kutokana na Taifa kuwa katika hali ya sintofahamu. “Tumeamua kukualika wewe uzungumze na viongozi wa
dini zote zitakazosaidia kubadilisha hali iliyopo sasa. Umevumilia mengi
kama Watanzania walikuudhi na kukukera kwa niaba yao uwasamehe,”
alisema Sheikh Salum.
Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Askofu Valentino Mokiwa alisema baada ya mkutano huo kuwa kuna umuhimu
wa kutafakari mambo yanayosumbua na kuendelea kusumbua sana.
“Bado sijajua kama hotuba yake (Rais) aliyoitoa
itatoa dira ya mchakato huu wa Katiba, tusubiri kuona kipi wananchi
wataamua,” alisema Askofu Mokiwa ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la
Anglikana Tanzania Dayosisi ya Dar es Salaam.
Umoja wa makanisa Tanga
Katika tamko lake Umoja wa Makanisa Mkoa wa Tanga
pamoja na kuwataka Watanzania kuikataa Katiba Inayopendekezwa,
umeishauri Serikali kusogeza mbele Kura ya Maoni. Msimamo huo ulitangazwa na Mwenyekiti wa umoja huo, Askofu Dk
Jotham Mwakimage aliyezungumza na waandishi wa habari baada kikao cha
maaskofu na wachungaji wa makanisa mbalimbali ya Tanga.
CHANZO: MWANANCHI
Alisema kikao chao kilichofanyika wiki iliyopita
katika Kanisa la Agape jijini Tanga na kuhitimishwa jana, kimeamua
kutambua na kuheshimu tamko la Jukwaa la Wakristo lililotolewa Machi 10,
mwaka huu la kuwaomba Watanzania waipigie kura ya ‘Hapana’ Katiba
Inayopendekezwa.
Sababu za kuikataa
Alisema Katiba hiyo ni imeligawa Taifa la
Tanzania, iliandaliwa na kupitishwa kwa hila na kimabavu na ndiyo sababu
inalazimishwa ipigiwe kura ya ‘Ndiyo’ bila kuruhusu masahihisho ya
makosa yaliyomo.
Sababu nyingine kwa mujibu wa tamko hilo ni kwamba
Katiba Inayopendekezwa iliandaliwa kwa hila ikiwa na madhumuni ya
kuondoa Rasimu ya Katiba iliyotokana na mawazo ya wananchi walio wengi
yaliyokusanywa na kuratibiwa na Tume ya Jaji Warioba. “Walioleta msukumo wa kupitisha Katiba kimabavu,
ndiyo wanaochochea uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ili kuigawa nchi
kidini,” alisema Mwakimage wakati akielezea sababu ya nne ya kutounga
mkono katiba pendekezwa.
Umoja huo wa makanisha umesema katika tamko hilo
kwamba ili kuondoa mkanganyiko, unaishauri Serikali kusogeza mbele Kura
ya Maoni kwa sababu muda wa mwezi mmoja hautoshi kwa wananchi kuisoma,
pia nakala zilizotolewa ni chache.
Sababu nyingine ya kupendekeza kusogezwa mbele kwa
Kura ya Maoni ni kutoa nafasi ya kutosha ya kuboresha Daftari la
Wapigakura na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. “Sisi umoja wa makanisa tunasisitiza kuwa
Watanzania wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la
Wapigakura na kupigia Katiba Inayopendekezwa kura ya Hapana, sawa na
tamko la maaskofu,” alisema Mwakimage.
Baraza la makanisa
Wakati huohuo, Baraza la Makanisa ya Kipentekoste
Tanzania (CPCT) limetoa tamko kuhusu hali ya kisiasa nchini likiwamo
suala la Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na kusisitiza uamuzi wa kuwataka Wakristo kujiandikisha kwa wingi na kuipigia kura ya ‘Hapana’ katiba hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu CPCT, Askofu David Batenzi
alitoa tamko hilo jana katika Kanisa la Bethel jijini Arusha mbele ya
maaskofu wakuu 70 waliohudhuria na kujadili pamoja na mambo mengine,
hali ya kisiasa nchini, akisema wamefikia hatua ya kutoa tamko hilo ili
kuondoa mkanganyiko uliokuwapo.
Akifafanua mkanganyiko huo, Askofu Batenzi alisema
kumekuwapo madai ambayo siyo ya kweli kuwa miongoni mwao kuna maaskofu
wanaonyesha nia ya kuwaunga mkono wagombea urais na wengine wanatoa
matamko kinzani dhidi ya tamko la Jukwaa la Wakristo (TCF), chombo
ambacho CPCT ni mwanachama.
Askofu Batenzi alisema kuwa CPCT haina chama wala
mgombea na kwamba wanaamini katika kumwomba Mungu awape kiongozi
atakayelifaa Taifa.
“Mtu yeyote anayedai kuwa ni Mpentekoste
aliyetenda au atakayetenda kinyume na msimamo huu, hakutumwa na wala
hatakuwa ametumwa na CPCT,” alisema. Alisema uwakilishi wa viongozi na wajumbe wa CPCT
kwenye kikao cha TCF kilichotoa tamko, ulikuwa na baraka zote za baraza
hilo na madai yoyote kwamba CPCT inaburuzwa na mwenyekiti na katibu wake
kwenye tamko hilo yapuuzwe, kwa kuwa hayana msingi wowote.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment