Mbunge wa Moshi Vijijini
na Mjumbe wa NEC ya CCM, Dk Cyril Chami, amewaomba walimu zaidi ya
2,700 wamuombee Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ili ‘ndoto’ yake
iweze kutimia.
Wakati Dk. Chami akiwaomba walimu hao, mtandao wa
marafiki wa Lowassa Kanda ya Kaskazini, juzi walikuja na staili mpya ya
kumshawishi Mbunge huyo wa Monduli agombee nafasi ya Urais.
Staili hiyo mpya imekuja wakati CCM ikiwa imempiga
‘stop’ kuendelea na utaratibu wake wa kupokea makundi ya watu
wanaomshawishi kugombea urais na yeye (Lowassa) kuridhia na kuwaomba
wananchi wasubiri maelekezo ya CCM.
Marafiki hao ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu
mkoani Kilimanjaro, walikwenda kitengo cha damu salama Kanda ya
Kaskazini kuchangia damu kama njia ya kutambua na kuenzi upendo wa
Lowassa.
Tukio hilo la wanafunzi hao kwenda katika kitengo
hicho, kilitanguliwa na tukio la mkutano mkuu wa Chama cha Akiba na
Mikopo (Saccos) ya Walimu Moshi Vijijini kufanya mkutano wao mkuu.
Katika mkutano huo, Dk Chami aliyekuwa mgeni rasmi, aliwaambia amekwenda
pale akiwa na salamu kutoka kwa Lowassa kwamba anawapenda sana walimu.
“Anasema anawapenda na anawakumbuka sana na anawaomba mmuombee ili ndoto
yake na ile safari yake (bila kuitaja) itimie,” alisema Dk Chami na
walimu hao kulipuka kwa vigelegele.
Katika tukio la uchangiaji wa damu, wanafunzi
zaidi ya 100 wa vyuo vikuu mkoani Kilimanjaro, walitumia tukio hilo
kumuunga mkono Lowassa wakimsihi atangaze nia ya kuwania Urais 2015.
Mratibu wa marafiki wa Lowassa, Noel Nnko, alisema
wanafunzi hao wameamua kuchangia damu kumuunga mkono kada huyo kwa vile
wao hawana uwezo wa kutoa fedha za kuchangia fomu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment