Katika makala haya tutawaletea uhakiki mfupi wa
kitabu chake kiitwacho “Kumbukumbu zangu za Afrika Mashariki (My
Reminiscences of East Africa).
Kitabu hiki kimeandikwa na Paul Emil von
Lettow-Vorbeck. Huyu alikuwa ni Jenerali katika jeshi la Ujerumani na
kamanda mkuu wa vikosi vya Ujerumani katika koloni lao la Afrika
Mashariki (Tanganyika, Rwanda na Burundi). Anakumbukwa kutokana na umahiri wake katika Vita
Kuu ya Kwanza ya Dunia kwa namna alivyowapeleka puta Waingereza na
washirika wao.
Von Lettow Vorbeck anaeleza kuwa baada ya kuanza
kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kule Ulaya mnamo Julai 1914 na baadaye
kusambaa kwenye makoloni, yeye kama kamanda alitambua kuwa isingekuwa
rahisi kwa Wajerumani na jeshi lao kuishinda Uingereza na washirika wake
katika Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.
Kwahiyo, alichoamua ni kutumia kikosi kidogo cha
askari ili kuwabana maadui zao na kuhakikisha kuwa maadui zao
wanaendelea kuleta askari zaidi Afrika Mashariki, badala ya kuwapeleka
kwenye mapambano makubwa barani Ulaya.
Lengo la mkakati huu ni kupunguza shinikizo kwa
jeshi la Ujerumani huko Ulaya. Wajerumani katika Afrika Mashariki
hawakushindwa vitani bali walisalimu amri wiki mbili baada ya vita
kwisha rasmi huko Ulaya.
Wakiwa katika mji wa Abercone huko Zambia, Von
Lettow na askari wake walipata taarifa za uhakika kuwa Ujerumani
ilisalimu amri na vita vilikuwa vimekwisha kule Ulaya. Kwahiyo, hawakuwa na sababu ya kuendelea kupigana ikiwa nchi waliyokuwa wakiipigania iliamua kusalimu amri.
Kitabu hiki kinahusu kumbukumbu za Jenerali huyu
mahiri kuhusu matukio ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Barani Afrika,
hususan Afrika Mashariki. Kitabu kina utajiri mkubwa wa taarifa kuhusu
maelezo mbalimbali ya kampeni za kijeshi na utaalamu katika lojistiki.
Kubwa zaidi katika kitabu hiki ni namna Von Lettow
Vorbeck alivyolijenga jeshi lake katika nidhamu ya hali ya juu. Askari
wa Kijerumani walikuwa maili nyingi mbali na nyumbani lakini kamanda wao
aliwajenga kusahau hamu ya kutaka kurejea nyumbani badala yake
wapiganie koloni lao akiwaaminisha kuwa Afrika Mashariki nako ni
nyumbani.
Askari walihimizwa kupigana kwa ushujaa, kujituma
na kujitolea kwa moyo wao wote kupigana dhidi ya maadui zao. Walikuwa na
nidhamu ya hali ya juu na hakukuwa na ubaguzi baina ya askari weusi na
weupe.
Kutokana na ukweli huu, Von Lettow anatoa
changamoto kwa wapinzani wote wa ukoloni wa Wajerumani barani Afrika
kuthibitisha madai kuwa Wajerumani walikuwa ni makatili dhidi ya wenyeji
katika makoloni yao. Anahoji kuwa ikiwa madai ya ukatili ni ya kweli kwanini wenyeji
wa Afrika Mashariki waliwaunga mkono wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia?
Pia, ikiwa Wajerumani hawakuwa watu wema
iliwezekanaje askari wenyeji wakapigana bega kwa bega na kamanda wao
tena wakati mwingine bila kulipwa chochote?
Wakosoaji wa kitabu hiki wanadai kuwa maeneo mengi
aliyoyataja kwenye kitabu chake hayamo kwenye ramani alizoziweka
kitabuni na lugha iliyotumiwa siyo laini sana kumvutia msomaji.
Hata hivyo, mwenyewe anakiri kuwa kumbukumbu
nyingi alizokuwa nazo wakati wa vita zilipotea na alichokiwasilisha
hakiwezi kwenda bila ya upungufu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment