Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Serikali imesema haitahusika na uuzaji wa ardhi ya
wananchi wa Kigamboni bali suala hilo linaachwa kwa wamiliki wenyewe,
ambao wanaruhusiwa kuwasiliana na kukubaliana na mnunuzi yeyote kutoka
nje au ndani ya nchi kwa makubaliano watakayofikia.Pia imesema itapitia upya waraka wa aliyekuwa Waziri Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, kuhusu mapendekezo na
mpango wa kuendeleza eneo la mji wa Kigamboni lenye ukubwa wa hekta
6,494.
Waziri wa Wizara hiyo, William Lukuvi, alisema hayo katika mkutano
wake na wadau kuhusu mpango kabambe wa kuendeleza mji mpya wa Kigamboni
na mwendelezo wa mahitaji ya kisheria. Aliwataka wananchi wanaomiliki ardhi kuwatumia wapimaji wa serikali
na wasio wa serikali ili wapimiwe na kupata hati mapema kama ulinzi na
uthibitisho ili wawe na maamuzi kuhusu ardhi wanazozimiliki.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Selasie Mayunga, alisema ndani ya miezi
mitatu serikali itahakikisha mpango wa kuandaa rasimu unakamilika na
kwamba, kutakuwa na dawati maalumu la kushughulikia hati miliki za ardhi
kwa wananchi wa Kigamboni litakalokuwa katika eneo hilo ili wapate hati
zao kwa urahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Saidiki, aliwataka
viongozi wa Mpango wa Maendeleo ya Mji Mpya Kigamboni (KDA)
kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Halmashauri ya Temeke , wilaya,
kata na vitongoji vyake ili kuhakikisha kila hatua zinazochukuliwa na
wamiliki wa ardhi wanapata taarifa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment