Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amesema upatikanaji wa viwanja vilivyopimwa utaondoa tatizo
la mafuriko kwenye miji mbalimbali nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mpango wa
ukopeshaji viwanja bila riba, Dk. Bilal alisema hatua hiyo pia
itabadilisha muonekano wa miji na kurahisisha huduma za kijamii.
Mradi huo unaoendeshwa kwa pamoja kati ya Benki ya Amana na kampuni
ya kizalendo ya Property Tanzania, itawapatia nafasi wateja kupata
viwanja hivyo kwa kuanza kulipa asilimia 20 za malipo na kiasi
kilichobaki kitalipwa taratibu.
“Mradi huu utakuwa mkombozi kwa watu wa kipato cha chini, naamini
mkienda mbali kwa kushirikisha halmashauri, mtawafikia watu wengi na
kuwaepusha na majanga ya asili kama mafuriko,” alisema Dk. Bilal.
Awali, Mkurugenzi wa Property, Abdul Haleem, alisema kati ya miradi
yote itakayoendeshwa, itatoa kipaumbele kwa wananchi wa hali ya chini
ambao wanakosa fursa ya kupata mikopo katika benki mbalimbali.
Alisema kwa watu wanaohitaji viwanja hivyo, watatakiwa kufungua akaunti kwenye benki hiyo na kulipa kiasi hicho cha fedha.
Alisema kampuni yake yenye uwezo wa kupima viwanja 600 kwa siku,
inashirikiana na halmashauri za wilaya katika uuzaji wa viwanja hivyo.
Alitaja baadhi ya viwanja vilivyotangaza kuwa sokoni ni Vikuruti na
Bokotimiza vilivyopo eneo la Kibaha na Chekeni Village eneo la
Kigamboni.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment