Mkurugenzi wa kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Bisimba.
Wanaharakati nchini wamesema rais ajaye anaweza
kuwa mwanamke kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo wingi na hamasa
waliyonayo wanawake katika upigaji kura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema ingawa wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama wanawake na jamii itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais mwanamke.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema ingawa wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama wanawake na jamii itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais mwanamke.
Wanaharakati hao kutoka vyama vya Umoja wa
Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Kigoda
cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walisema hakuna
kinachoshindikana kama wanawake wataamua.
Ulingo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania
(Ulingo), Anna Abdallah alisema, baada ya wanawake kuangaliwa kama
kundi duni katika nyanja za siasa kwa muda mrefu, sasa ni zamu yao
kujitokeza wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya urais.
“Lengo letu sisi ni mwanamke kujitokeza,
akijitokeza tutamuunga mkono kwa umoja wetu bila kujali anatoka chama
gani cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo aliyeeleza kuwa jamii ya sasa
ina imani kubwa na mwanamke.
Aliongoza “Iwapo wanawake watafanya kile
tunachotaka , kwa maana ya kuwaunga mkono wagombea, kupiga kura, wakati
wa kupata rais mwanamke umefika. Hilo halina ubishi na linawezekana.”
Anna alitaja sababu nyingine za kuwashawishi wanawake wajitokeze
kugombea urais kuwa ni kuongezeka kwa uelewa wa wanawake katika masuala
ya siasa.
TGNP
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP),
Lilian Liundi alisema wanawake kuwa viongozi siyo ajabu kwani tayari
wameshafanya hivyo katika nafasi mbalimbali. Isipokuwa wanahitaji
kuungwa mkono katika nafasi za kisiasa.
Alisema mtandao huo utamuunga mkono mwanamke
yeyote atakayeonyesha nia ya kugombea bila kuangalia itikadi ya chama
anachotoka, huku ukiamini kuwa wanawake wanaweza kufanya vizuri zaidi
wanapopata nafasi. “Japokuwa historia inaonyesha wanafanya vizuri,
tunahitaji kuwaunga mkono kwa nia thabiti ili wakalete mabadiliko ya
kweli, ” alisema Liundi.
Kigoda cha Taaluma
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama, alisema kuwa huko nyuma
ilikuwa kazi wanawake kuwa viongozi, lakini sasa njia ipo, kwani wapo
waliotangulia kuwa viongozi na wakafanya vizuri.
Alisema moja ya mambo yatakayofanikisha hilo ni
wanawake wenyewe kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi huo
kwenye ngazi zote; udiwani, ubunge na urais. “Wakati wa kusubiri kutengewa viti maalumu
umekwisha na wanawake walitambue hilo, hivyo wajitokeze katika harakati
za kugombea uongozi badala ya kusubiri kuteuliwa,” alisema na kubainisha
kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura wa Tanzania ni wanawake.
“Kuna viongozi wanaume hawana uwezo kabisa
historia inaonyesha na wanatuongoza, wamepenya katika uongozi kwa sababu
wanaungana mkono na wanatafuta ushawishi, sasa kama wapo wanawake wenye
uwezo wa kuongoza kwa nini wasifanye hivyo na kwa nini wasiungwe mkono
kwanza na wanawake wenzao halafu wanaume wafuatie,” alihoji Profesa
Mlama.
LHCR
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Bisimba alisema, kuna wanawake wamefanikiwa kupitia
harakati hizi za kuwataka wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, kwa
sababu walikuwa na uwezo lakini walikuwa wagumu kujitokeza.
Alisema iwapo ushawishi kwa wanawake utapamba moto
kama ilivyo sasa na wengi wakajitokeza kugombea, matokeo ya uchaguzi
mkuu ujao yatashuhudia wanawake wengi wakishika nafasi mbalimbali za
uongozi. “Kuna nafasi kubwa ya kupata rais mwanamke kwa
sababu wagombea wengi wanaoshinda nafasi za juu ikiwamo urais
wanawategemea wanawake kama wapiga kura wao wakuu, hivyo wakijipigia
wenyewe nafasi ya kushinda itakuwa kubwa, ” alisema Bisimba.
Alifafanua kuwa juhudi zao za kuwaunga mkono siyo
za fedha bali kuwapa moyo na kuwajengea uwezo kwani mfumo uliopo una
vikwazo vingi kwa mwanamke.
“Tunawajengea kujiamini, kusimama mbele za watu na
kujinadi kwa mifano iliyo hai siyo hadithi, kuzungumza bila woga mbele
za watu, tuna imani tutashinda mapambano haya,” alisema Bisimba.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment