Mmiliki wa IPTL, Habinder Sethi.
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL) imejiondoa katika kesi ya kikatiba iliyoifungua
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga utekelezaji wa maazimio
nane yaliyopitishwa na Bunge baada ya kushindwa kupinga mapingamizi
yaliyowasilishwa na upande wa serikali.Mbali na IPTL kampuni nyingine zilizohusika kupinga maazimio hayo
ni Pan Africa Power Solution Ltd (PAP) mmiliki wa IPTL, Habinder Sethi
(pichani), na mmiliki wa kamapuni VIP Engineering and Marketing Ltd,
James Rugemalira.
Mbele ya Jaji Stella Mugasha, wakili wa upande wa utetezi, Gabriel
Munyele, akisaidiana na wakili Joseph Sungwa, aliiambia mahakama kuwa
hakuna haja ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwani zuio la muda
waliloomba lilikuwa limeshaanza kutekelezwa na Bunge.
Upande wa serikali ukiongozwa na naibu Mwanasheria Mkuu, Gabriel
Malata, ulidai kuwa ulipwe gharama za kesi kutokana na usumbufu
uliofanywa na IPTL kung’ang’ania kupinga maazimio ambayo yalikuwa
yalishaanza kutekelezwa.
Malata alidai kuwa IPTL inatakiwa kulipa gharama za uendeshaji wa
kesi zikiwamo uchapishaji wa majalada na muda waliotumia kuja
mahakamani. Aidha aliiomba Mahakama itumie vifungu vya sheria vinavyoelezea na
masuala ya gharama za kesi kuiamuru IPTL kulipa gharama hizo.
Malata aliiomba mahakama itende haki ili kukomesha usumbufu
unaofanywa na kampuni au watu wanaofungua kesi wakati wakijua hawawezi
kushinda. Jaji Mugasha aliitaka kampuni ya IPTL iwajibike kwa kulipa gharama
za kesi kwa kushindwa kujiondoa mapema kupinga maazimio hayo, huku
wakijua fika yalishaanza kutekelezwa.
Wakili Malata alisisitiza kuwa upande wa serikali utafuatilia ili kuhakikisha IPTL inalipa gharama za kesi kwa wakati mwafaka. Desemba 31 mwaka jana serikali iliwasilisha mapingamizi matano
katika mahakama hiyo kupinga maombi ya IPTL juu ya maazimio
yaliyopitishwa na bunge.
Moja ya mapingamizi ni kuwa maombi yaliyowasilishwa na IPTL hayana msingi kwa kuwa yalishaanza kutekelezwa. Pingamizi la pili IPTL hawakufungua kesi ya msingi bali walileta maombi ya kupinga utekelezaji.
Mapingamizi yaliyowasilishwa na hayatekelezeki kwa kuwa hakuna vifungu vya sheria vinavyoeleza maombi waliyoomba. Katika kesi hiyo namba 57 iliyosajiliwa mwaka jana IPTL ilifungua
kesi ya maombi kupinga ya maazimio nane yaliyopitishwa na bunge
yakiwamo.
Miongoni mwa maazimio hayo ni Bunge kuitaka Takukuru, Jeshi la
Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua
stahiki za kisheria watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)) kuhusika na kashfa ya uchotaji wa
zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment