Kiongozi wa Kanisa katoliki duniani papa Francis ametoa karipio kali kwa
uongozi wa Vatican, na kukosoa kile alichokieleza kuwa ni ugonjwa
ulioukumba uongozi huo, ukiwemo wa kuteta, na uchu wa madaraka.
Katika orodha ya madhambi saba makubwa zaidi ya Kanisa Katoliki, Papa
Francis ameongeza kile alichokiita magongwa 15 yanayowakabili wasaidizi
wake ndani ya Vatican, na kuwataka watumie muda huu wa Krismas kutubu
dhambi zao na kulifanya Kanisa kuwa mahala penye afya na patakatifu
zaidi mwaka 2015. Papa Francis alizungumza juu ya wale wanaojigeuza kuwa mabosi, na
wanaojiona wako juu ya kila mmoja na hawamtumikii yeyote. Alionya pia
juu ya kile alichokiita "ugonjwa wa madaraka" na kuwaonya dhidi ya
nargisi ya wale wanaojijali wenyewe bila kuwahurumia walio dhaifu na
wanaohitaji zaidi.
Tamaa ya vyeo na ubinafsi
Aliwakosoa pia wasiowaheshimu wakubwa zao akisema,"ugonjwa wa kutomtii
mkubwa ndiyo ugonjwa wa wale wanaowasifu wakubwa zao wakitumai kupata
kitu kutoka kwao. Hao ni wahanga wa tamaa ya vyeo na ubinafsi,
wanawaheshimu binaadamu na siyo Mungu." Na wakati miongoni mwa wasikilizaji walikuwepo waliokunja sura zao, papa
alizungumzia ugonjwa wa kile alichokiita sura za msiba, akibainisha
kuwa watu wasioridhika na wanaokunja sura, wale wanaojaribu kuva sura za
ukali, wanawatendea wengine, hasa wale wanaoamini ni wa hadhi ya chini,
kwa dharau na kwa kibri. Francis ambaye ndiye papa wa kwanza kutoka Amerika Kusini na hakuwahi
kufanyakazi katika baraza la uongozi wa kanisa hilo linalodhibitiwa na
Wataliana kabla ya kuchaguliwa, hakuona haya kulalamika juu ya porojo,
tamaa ya vyeo, na hila za madaka vinavyoikabili Vatican. Lakini wakati
ajenda yake ya mageuzi ikizidi kushika kasi, alionekana mwenye kuthubutu
zaidi hata kuweza kubainisha yale yanayoikwamisha taasisi hiyo.
Hotuba kali zaidi
Wafuatiliaji wa masuala ya Vatican walisema hawajawaji kusikia hotuba
kali kama hiyo kutoka kwa papa, na kuongeza kuwa huenda ameamua kuweka
mambo hadharani kutoka na upinzani anaokabiliana nao katika kutekeleza
mageuzi yake. "Ukweli kwamba anaielekeza hotuba yake ya Krismas kwa magonjwa 15 ya
kiroho kwa namna hiyo, kwa maoni yangu ni ishara kwamba anachukulia
mageuzi katika uongozi, na mageuzi ya kiroho kiujumla, kama hatua muhimu
anayotaka kuendelea kuchukuwa, kwamba bado kuna upinzani mkubwa,na
kwamba pengine upinzani umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni,"
alisema Iacopo Scaramuzzi, ripota wa gazeti la TMNews mjini Vatican. Mwanahistoria wa kanisa katika chuo kikuu cha Seton Hall Padri Robert
Wister, alisema kimsingi Papa Francis alikuwa anaomba wasaidizi wake
wajitathmini wenyewe, akiwaomba kuangalia namna walivyotenda dhambi
mbele ya Mungu kabla ya kwenda kutubu. Aliongeza kuwa pengine anaamini
karipio kali linaweza kusaidia kubadili mambo.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment