Viongozi wa nchi za Ghuba za Kiarabu.
Nchi za Ghuba za Kiarabu zenye utajiri wa mafuta zimesimama kidete dhidi
ya nchi zenye kuzalisha mafuta ghafi ambazo sio wanachama wa Shirika la
OPEC na kuapa kutopunguza kiwango cha uzalishaji.
Nchi za Ghuba za Kiarabu zenye utajiri wa mafuta zimesimama kidete dhidi
ya nchi zenye kuzalisha mafuta ghafi ambazo sio wanachama wa Shirika
Linalosafirisha Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC na kuapa kwamba
hazitopunguza kiwango cha uzalishaji na wala kuitisha mkutano wa dharura
wa shirika hilo kusaidia kuimarisha bei ya mafuta.
Wazalishaji wakuu wa mafuta katika shirika la OPEC Saudi Arabia na
Kuwait zimesema hazitopunguza kiwango cha uzalishaji hata kama nchi
ambazo sio wanachama wa OPEC zitapunguza uzalishaji wao wakati Umoja wa
Falme za Kiarabu na Iraq zikipuuza wito wa kuitishwa kwa mkutano wa
dharura wa shirika hilo.
Saudi Arabia imezilaumu nchi ambazo sio wanachama wa OPEC kwa koporomoka
huko kwa bei ya mafuta.Imesema haitopunguza kiwango chake cha
uzalishaji iwapo nchi nyengine hazitoanza kuchukuwa hatua hiyo. Ali al-Naimi waziri wa mafuta wa Saudi Arabia amewaambia
waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano wa nishati hapo Jumapili mjini
Abu Dhabi Umoja wa Falme za Kiarabu kwamba nchi zisizo wanachama wa
OPEC zinataka kupunguza uzalishaji zinakaribishwa lakini sio Saudi
Arabia haitofanya hivyo.
Amekaririwa akisema "Hatujuwi nini kitakachotokea kipindi cha usoni.Kile
tunachokijuwa kwa uhakika ni kwamba nchi zenye uzalishaji mkubwa na
ulio bora ndizo zitakazodhibiti soko."
Zashupalia msimamo wao
Waziri wa mafuta wa Kuwait Ali al-Omair akiunga mkono kauli ya Saudi
Arabia amesema hafikiri kwamba kuna haja ya kupunguza uzalishaji na
kwamba licha ya kutowa fursa kwa nchi nyengine kufanya hivyo nchi hizo
haziko tayari kuchukuwa hatua hiyo. Ameongeza kusema kwamba OPEC haitopunguza uzalishaji na kwamba hakuna
kitakachotokea hadi mwezi wa Juni na pia hakutokuwa na mkutano wa
dharura.
Soko la mafuta duniani limezidi kuwa na ushindani katika miaka ya hivi
karibuni kutokana na ongezeko la uzalishaji wa mafuta ya mwamba tope
kutoka nchi ambazo sio wanachama wa shirika la OPEC lilioundwa miongo
mingi iliopita.
Sababu za kushuka kwa bei
Bei za mafuta zimeshuka kwa takriban asilimia 50 tokea mwezi wa
Juni kwa kiasi kikubwa kutokana na kushehena kwa usambazaji, uchumi
dhaifu wa dunia na dola ya Marekani kuwa na nguvu.Wachambuzi wengine
wanasema sababu nyengine ya kuyumba kwa bei ya mafuta ni ongezeko la
uzalishaji wa gesi mwambatope. Waziri wa mafuta wa Iraq Adel Abdulmahdi akifuta uwezekano wa kufanyika
kwa mkutano wa dharura amesema inabidi wasubiri kuona jinsi masoko na
nchi yatakvyokabiliana na hali hiyo.Anaamini kwamba bei ya mafuta
itatulia na kuja kuwa dola sitini kwa pipa.
Saudi Arabia,Kuwait,Umoja wa Falme za Kiarabu,Qatar na Iraq huzalisha
mapipa milioni 20 kwa siku au theluthi mbili ya mafuta ya yanayozalishwa
na OPEC. Shirika hilo mwezi uliopita liliamuwa kuendelea na kiwango cha
uzalishaji wake wa mapipa milioni 30 kwa siku jambo ambalo limepelekea
kuanguka kwa bei za mafuta.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment