Rais Barack Obama akihutubia taifa juu ya mabadiliko ya sera ya Marekani kuelekea Cuba.
Baada ya zaidi ya nusu karne ya uhasama, hatimaye Marekani na Cuba
zinarejesha mahusiano yao kidiplomasia, hatua ambayo imeungwa mkono na
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.
Kwanza lilianza tangazo la Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye
wakati akilihutubia taifa usiku wa jana, alisema wakati wa kubadili
muelekeo wa nchi yake kuelekea Cuba umefika. "Leo Marekani inabadilisha
mahusiano yake na watu wa Cuba na mageuzi makubwa kabisa kwenye sera
yetu ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka 50. Tutaumaliza mtazamo wa
zamani ambao kwa miongo kadhaa umeshindwa kuendeleza maslahi yetu, na
badala yake tutayaweka sawa mahusiano kati ya nchi zetu mbili," alisema
Obama kwenye hotuba hiyo.
Muda mchache baadaye, kauli ya Obama ikathibitishwa na Rais Raul
Castro wa Cuba, ambaye akilihutubia taifa alisema nchi yake inatambua na
inampa heshima anayostahiki Rais Obama kwa hatua zake za kunyoosha
mkono wa maridhiano, akaongeza kwamba kutokana na mazungumzo kwa ngazi
za juu, yakiwemo yale aliyofanya jana na Rais Obama kwa njia ya simu,
"tumeweza kusonga mbele na kutatua maeneo kadhaa yanayohusu maslahi ya
mataifa yote mawili."
Kuachiwa kwa majasusi
Katika kile kinachoonekana kutilia nguvu mahusiano haya mapya,
Cuba ilimwachia huru raia wa Marekani, Alan Gross, ambaye amekuwa
akishikiliwa tangu mwaka 2009, kwa tuhuma za kuingiza nchini Cuba vifaa
vya mawasiliano kwa ajili ya ujasusi. Vile vile, Obama na Castro, walitangaza kwamba nchi zao
zilibadilishana majasusi wa kila upande ambao walikuwa wamefungwa upande
mwengine.
Hatua hii ya aina yake sasa inaashiria kwamba vikwazo vya kiuchumi na
kibiashara kati ya majirani hao ambao wameishi kwa uhasama kwa zaidi ya
nusu karne vitaondoshwa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon,
ameisifu hatua hii akisema ni ishara njema kwa mataifa yote mawili.
"Habari hii ni njema - kuyaweka sawa mahusiano ya nchi mbili. Kwa
hali hiyo, naipongeza sana hatua hii. Ninatarajia kuwa tangazo hili
litasaidia kuongeza mualaka baina ya watu wa mataifa hayo mawili ambao
wametenganishwa kwa muda mrefu", alisema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
Marekani kufungua ubalozi Cuba
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amesema ndani
ya kipindi kifupi kijacho, Rais Obama atatuma ujumbe wake maalum nchini
Cuba, ambao huenda ukafuatiwa na yeye kuwa waziri wa kwanza wa mambo ya
nje wa Marekani ndani ya kipindi cha miaka 60 kuzuru Havana.
Mabadiliko haya ya sera ya Marekani kuelekea Cuba ni matokeo ya
mazungumzo ya siri ya miezi 18 yaliyojumuisha mikutano kadhaa nchini
Canada na uingiliaji binafsi wa Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa
Francis. Pia yanaakisi hatua isiyo ya kawaida ya Obama bila ya idhini ya bunge
katika wakati huu anapomalizia muhula wake wa urais. Obama anapanga
kupitia upya sheria ya Marekani inayoitambua Cuba kama taifa
linalofadhili ugaidi.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment