Kundi kubwa zaidi la waasi nchini Colombia la FARC limetangaza
usitishaji mapigano wa upande mmoja usiyo na kikomo, katika mgogoro huo
wa miaka 50, kufuatia duru nyingine ya mazungumzo ya amani.
Kundi la Revolutionery Armed Forces of Colombia FARC, lilitoa tangazo la
kusitisha mapigano kwa muda usiyo na kikomo nchini Cuba mwishoni mwa
duru nyingine ya mazungumzo ya amani yanayolenga kumaliza uasi wa muda
mrefu zaidi katika bara la Amerika ya Kusini.
"Kwa kuwa tunaamini kwamba tumeanzisha njia halisi kuelekea amani pamoja
na mchakato wake, tumeazimia kutangaza usitishaji mapigano wa upande
mmoja na kukomesha uhasama wote kwa muda usiyojulikana, ambao unapaswa
kupelekea mapatano ya kusitisha vita," alisema Ivan Marquez, mwakilishi
wa FARC katika mazungumzo ya mjini Havana.
CELAC,CICR, ICRC kusimamia mchakato
Alisema ili hatua hiyo ifanikiwe kikamilifu, wanategemea usimamizi wa
muungano wa mataifa ya Amerika Kusini, Jumuiya ya mataifa ya Amerika na
Caribbean, Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundi na ngao pana ya
amani. Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya kundi hilo,
usitishaji huo mapigano utaanza kutekelezwa dakika moja baada ya saa
sita usiku Jumamosi hii ya tarehe 20 Desemba.
Waasi hao wamekuwa wakitoa wito wa usitishaji mapigano wa pande mbili
kama sehemu ya mchakato wa amani unaoendelea, lakini rais Santos, ambaye
ametoa kipaumbele kwa mazungumzo ya amani amekataa matakwa hayo,
akisema waasi wanaweza kutumia fursa ya makubaliano kujipanga upya na
kurefusha zaidi mgogoro.
Mtego kwa serikali ya Juan Manuel
Hata hivyo, tangazo la jana la FARC litaiwekea shinikizo serikali ya
Colombia kuchukuwa hatua sawa, alisema mtaalamu wa siasa Jorge Restrepo,
anaeongoza kituo cha uchambuzi wa migogoro cha Colombia. Ingawa FARC
wamekuwa wakitangaza usitishaji mapigano kuelekea siku kuu ya Krismasi,
hii itakuwa mara ya kwanza wamekubali kuweka chini silaha kwa muda usiyo
na kikomo tangu miaka ya 1980.
Mazungumzo hayo yalikuwa yamekwama kufuatia mgogoro uliyosababishwa na
kutekwa kwa jenerali wa jeshi Ruben Dario Alzate Novemba 16. FARC
ilitetea hatua yake ya kumteka Jenerali huyo kama kitendo halali cha
kivita, lakini ilimuachia Novemba 30 ili kuunusuru mchakato wa amani. Kama moja ya masharti ya kuanzisha upya majadiliano, pande mbili
zilikubaliana kuweka mfumo wa kudumu wa kutatua migogoro inayojitokeza
usoni, ambao utasimamiwa na Cuba na Norway, mataifa mawili yanaoongoza
juhudi za amani.
Mazungumzo ya matumaini zaidi
Mazungumzo hayo yaliyodumu miaka miwili katika mji mkuu wa Cuba Havana,
ndiyo juhudi ya matumaini zaidi kukomesha mgogoro huo wa miongo mitano,
ambao umeshindwa kutatuliwa na juhudi zote za nyuma.
Mpaka sasa majadiliano yamezaa makubaliano kuhusu mageuzi ya sera ya
ardhi, mapambano dhidi ya usafirishaji madawa ambao umechochea mgogoro
huo, na ushirikishwaji wa waasi kisiasa. Mgogoro huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 220,000 and zaidi ya
milioni 5.3 wameyakimbia makaazi yao tangu FARC ilipoanzishwa kufuatia
uasi wa wakulima mwaka 1964.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment