Pages

Monday, November 02, 2015

CTI YAMPONGEZA DK. MAGUFULI


Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI), limempongeza Rais mteule, Dk. John Magufuli, kufuatia ushindi alioupata kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga, alimpongeza pia Samia Suluhu Hassan, kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Makamu wa Rais hapa nchini.
“Kwa niaba ya CTI na mimi binafsi, napenda kuwasilisha pongezi zetu za dhati kwa Dk. John Magufuli, kwa ushindi alioupata. Ushindi huu ni kiashiria tosha cha imani kubwa waliyonayo Watanzania kwake,’’ alisema Tenga.
Alibainisha kuwa pamoja na kujipanga kushirikiana kwa ukamilifu na serikali ijayo ya Dk. Magufuli, CTI inaamini kuwa sekta ya viwanda nchini ina uhakika wa kufanya vizuri zaidi kutokana na msimamo aliouonyesha Dk. Magufuli wakati akiwaomba Watanzania ridhaa aliyopatiwa.
“Tulikuwa tukifuatilia kwa ukaribu ahadi za wagombea wote walizokuwa wanazitoa wakati wa kampeni na kinachotupa faraja zaidi ni kwamba miongoni mwa ahadi kubwa aliyozisisitiza Dk. Magufuli ni kuigeuza Tanzania kuwa nchi inayotegemea uchumi wa viwanda…tupo tayari kushirikiana naye kwenye hilo,’’ aliongeza.
Akitoa maoni yake kwa serikali ijayo juu ya namna ya kufanikisha hilo, Tenga aliyataja baadhi ya maeneo muhimu yanayohitaji kutazamwa upya kuwa ni pamoja na uwapo wa mfumo wa kodi usiobadilika badilika.
“Kwa sasa mapato mengi ya serikali yanatoka kwenye kundi dogo la walipa kodi na kwa maoni yetu tunaona kundi hili dogo limekuwa likibebeshwa mzigo mkubwa wa kodi kuliko uwezo wake na matokeo yake taifa limeshindwa kutimiza mapato yanayohitajika kuleta tija kwa taifa,’’ alisema.
Alisema kwa sasa sekta ya viwanda na biashara inakabiliwa na changamoto ya wingi wa kodi huku akitoa wito kwa serikali kuangalia namna ya kupunguza idadi ya mamlaka zinazofanya majukumu yanayofanana ili kupunguza urasimu na mzigo mkubwa wa kodi kwa wafanyabiashara nchini.
Aidha, Tenga alitaja changamoto nyingine kuwa ni suala zima la ukosefu wa miundombunu imara kwenye sekta ya uchukuzi huku akisisitiza haja ya uboreshaji kwenye usafiri wa reli nchini, mfumo wa barabara na uwapo wa nishati ya umeme wa uhakika sambamba na upatikanaji wa maji ya kutosha.
“Kuna haja ya kuboresha zaidi reli yetu na kuiweka kwenye kiwango cha kisasa zaidi. Pia ipo haja ya kuboresha muundo wa uingizaji na utoaji wa mizigo kwenye bandari zetu na hili liende sambamba na kuboreshwa kwa utendaji wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na Mamlaka ya Bandari nchini (TPA),’’ alisema.
Aliongeza kuwa upo umuhimu mkubwa wa serikali ijayo kuangalia upya upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali hasa wenye biashara na viwanda vya kati na vidogo.
Tenga alisema kwa sasa suala la upatikanaji wa mikopo ni changamoto kubwa kwa kuwa linahusisha masharti mengi sambamba na riba kubwa, jambo linalokwamisha ukuaji wa viwanda kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Tenga, ni muhimu kwa serikali hiyo kuhakikisha inawapa kipaumbele wawekezaji wazalendo wanaoonyesha nia ya kushiriki kwenye uwekezaji wa rasilimali zinazogunduliwa hapa nchini hususanimadini na gesi ili kuondoa tishio la sekta hiyo kunufaisha zaidi raia wa kigeni.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment