Pages

Thursday, October 29, 2015

UTANGAZAJI MATOKEO MBAGALA WAKWAMA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
Utangazaji wa matokea Jimbo la Mbagala ngazi ya ubunge imeshindikana baada ya mawakala na wabunge wa jimbo hilo kutoa mashariti matatu ikiwamo la kutaka uchaguzi huo kurudiwa.
Hatua hiyo imemfanya Mkurugenzi wa Uchaguzi Majimbo ya Temeke na Mbagala, Fotidus Kagimbo, kuahirisha kuendelea na mchakato wa kuhesabu kura za wabunge katika jimbo hilo na kuhaidi kutoa msimamo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) leo asubuhi.
Kagimbo alisema wakiwa katika chumba cha kuhesabia kura, mawakala hao na wabunge waligomea kuendelea na kazi ya kuhesabu kura kwa madai kuwa mchakato huo uligubikwa na dosari nyingi.
Alisema kutokana na hali hiyo, waliitaka Nec kurudia uchaguzi huo ama kuendelea na kazi ya kuhakiki kwa kata zenye dosari, huku wengine wakitaka kazi ya kuhakiki kura ianze upya kwa kata zote 10.
Kagimbo alisema suala la kurudia uchaguzi hawezi kulitolea majibu ya hapo hapo hadi atakapowasiliana na uongozi wa juu, huku suala la kuhakiki kata zote ni suala litakalochukua muda mrefu.
“Nec tumeshindwa kuendelea na kazi ya kumtangaza mshindi ngazi ya ubunge katika Jimbo la Mbagala kutokana na mawakala na wabunge wa vyama husika kutoa masharti au mapendekezo matatu ambayo siwezi kuyaamua mimi hadi ngazi husika itamke. Hivyo naahirisha kazi hii hadi kesho asubuhi (leo),” alisema Kagimbo.
Mgombea ubunge kwa Chama cha Wananchi (CUF), Kondo Bungo, alisema dosari zilizojitokeza katika uchaguzi huo ni pamoja na kupotea kwa makaratasi 24 yenye idadi ya wapigakura katika kata ya Mbagala Kuu.
Alisema dosari nyingine ni kuwapo kwa taarifa za uongo ikiwamo ya yeye kupata kura moja katika kata ya Tuangoma huku nakala aliyokuwa nayo ikionyesha amepata kura 78.
Alisema dosari nyingine ni pamoja na makaratasi yenye majumuisho ya kura kutoka kata mbalimbali kutokuwa na saini za mawakala, jambo ambalo hajawahi kupewa taarifa yoyote kutoka kwa wakala wake kuwa hawakusaini karatasi hizo.
Kwa upande wake, mgombe ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Issa Mangungu, alisema uchaguzi ulikuwa wa haki na ana imani kuwa ameshinda hivyo wafuasi wa CUF wameanzisha malalamiko ili urudiwe.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment