Mwanasheria nguli nchini Profesa Chris Peter Maina,
amesema kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni hasara kubwa kwa nchi kwani
fedha zilizotumika kuandaa uchaguzi huo ni za walipakodi ambao
watalazimika kubeba gharama nyingine zaidi.
Alisema kilichofanywa na Zec kimeteteresha imani ya wananchi kwa
tume hiyo kwani Mwenyekiti wake alipaswa kuwachukulia hatua mara moja
makamishna waliokiuka sheria na kanuni siku ya kupiga kura.
“Zec ilitakiwa iwe na uwezo wa kukamata watu waliovunja sheria na
kuwachukulia hatua, siyo kusubiri siku zimepita ndipo wanayasema haya na
kufuta matokeo…naona kama hawakuzingatia sheria kwa kutotoa taarifa
mapema,” alisema.
Aliongeza: “Zec wamepoteza imani ya wananchi na fedha za walipakodi ambazo zingelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.”
Hata hivyo, alisema kwa sasa itamlazimu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohammed Shein, kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Wawakilishi ili
kuidhinisha muda wa kuendelea kukaa madarakani hadi hapo uchaguzi
mwingine utakapofanyika.
STOLA: DEMOKRASIA IMEBANWA
Akizungumzia uamuzi huo wa Zec, Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Francis Stola, alisema pamoja na kwamba hautaathiri
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kitendo hicho
kimebana demokrasia.
Alisema inasikitisha kuona kuwa kasoro ndogo zinaahirisha uchaguzi
na kufuta matokeo, akifafanua kuwa hilo linachangiwa na kuwapo kwa
masalia ya sheria za chama kimoja ambazo zinapaswa kufutwa kwa kuwa
haziwezi kufanya kazi kwa haki katika uchaguzi wa kidemokrasia.
Hata hivyo, alisema uchaguzi wa Rais wa Zanzibar pamoja na
wawakilishi unasimamiwa na Zec na kwamba tume hiyo ni wakala wa Nec
ambaye hana mamlaka ya kutengua matokeo ya Jamhuri ya Muungano.
“Uchaguzi wa Zanzibar siyo suala la Muungano kwa sababu urais na
uwakilishi upo chini ya Zec…Nec itatazama hizo kasoro na itaamua kwa
sababu Zec ni wakala tu wa Nec,” alisema.
SUNGUSIA: NI UTATA MKUBWA
Naye mwanasheria mwingine ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utetezi na
Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold
Sungusia, alisema kufutwa kwa uchaguzi huo kunaweza kuwa na athari kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihoji wapigakura wanaodaiwa kushiriki
uchaguzi wakiwa hawana vitambulisho vyao.
Alisema kama Nec na Zec hazijafuta matokeo ya uchaguzi wa wabunge
visiwani humo, ni vigumu kujiridhisha kama wapigakura wanaolalamikiwa na
Zec hawakupigakura za urais na ubunge wa Jamhuri ya Muungano kwa kuwa
kura zilipigwa siku moja.
“Tunaweza kusema kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar hakuna athari zozote
kwa urais na ubunge wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu unasimamiwa na
mamlaka mbili tofauti…lakini mimi kama mwanasheria naona bado kuna utata
mkubwa ambao ningetamani mamlaka zetu (Zec na Nec); zingetoa ufafanuzi
zaidi,” alisema.
Sungusia alisema moja ya sababu za kufuta uchaguzi huo ambayo ni
kuwapo kwa wapigakura wasio halali, inaweza kuathiri uchaguzi wa wabunge
na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kuwa kura zilipigwa siku moja na
hakuna anayeweza kuthibitisha kuwa wapigakura hao (wasio halali),
hawakuchagua viongozi hao.
Aliongeza: “Kama Zec au Nec ikifuta uchaguzi wa wabunge visiwani
Zanzibar itawezekanaje kuzindua Bunge la Jamhuri bila wabunge kutoka
Zanzibar au uteuzi wa Baraza la Mawaziri utafanyikaje wakati baadhi ya
wabunge wa Zanzibar huteuliwa kwenye Bazara la Mawaziri la Jamhuri ya
Muungano.”
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 74 (13), ya Katiba ya Zanzibar na
Ibara ya 74 (13), ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zec na Nec
zinapaswa kushauriana kwenye masuala mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi
hivyo akashauri kuwa jambo hilo ni muhimu likazingatiwa katika hali ya
sasa.
Alisema hilo linapaswa kufanyika kwa kuzingatia kuwa Zec ndiyo
iliyosajili wapigakura kwa kukasimiwa madaraka na Nec kwa mujibu wa
kifungu cha 12 (A) cha sura namba 343 ya uchaguzi baada ya kukasimiwa
madaraka na Nec.
Hata hivyo, alisema uchaguzi wa rais na wawakilishi Zanzibar siyo
suala la Muungano hivyo Zec ina mamlaka ya kuamua chochote pindi
inapobaini kasoro kwenye mwenendo wa uchaguzi.
MAREKANI WATAKA UWAZI URAIS ZANZIBAR
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani jana jijini Dar es
Salaam, imewataka maofisa wote wa serikali kuheshimu wajibu wa
waangalizi rasmi wa uchaguzi kwa kuwaruhusu bila kipingamizi chochote
kuangalia vipengele vyote vya mchakato wa uchaguzi.
Aidha, taarifa hiyo ya Marekani ilisema inafuatilia kwa karibu mchakato wa uchaguzi nchini kote Tanzania.
“Tunaendelea kufuatilia zoezi la majumuisho ya kura, ikiwa ni
pamoja na zoezi linaloendelea la majumuisho ya kura za urais wa
Zanzibar linalofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), tunatoa wito
kwa mchakato huu kukamilishwa kwa wakati na kwa uwazi,’ ilisema taarifa
hiyo
Wakati taarifa hiyo ikitolewa na Marekani na kuitaka Zec
kukamilisha mchakato huo kwa wakati na kwa uwazi, tayari jana mchana
tume hiyo ilitangaza kufuta uchaguzi na matokeo yote ya Zanzibar.
JAJI MIHAYO
Jaji mstafu Thomas Mihayo alisema hatua ya kufutwa matokeo ya urais
Zanzibar, hayawezi kuathiri mchakato wa kumpata mgombea urais Bara kwa
ni serikali mbili tofauti.
Alisema Zec, imetengua kura za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar na siyo za wagombea ubunge na urais wa Serikali ya Muungano.
Alisema kwa mujibu wa sheria, rais anayemaliza muda wake wa uongozi
Dk. Shein, ataendelea kuongoza Zanzibar hadi pale uchaguzi
utakapofanyika tena.
WAKILI KAMALA
Naye Wakili wa kujitegemea Pascal Kamala , alisema kwa mujibu wa
Katiba ya Zanzibar ibara ya 28 kifungu cha 1(a), Rais ataendelea kuwa
madarakani hadi pale rais mwingine atakapopatikana na kuapishwa.
Alisema kutokana na maelezo ya kifungu hicho, Dk. Shein ataendelea kuwa madarakani. Alisema kifungu cha 28 (ii) cha Katiba hiyo kinaeleza kuwa rais atakuwa madarakani kwa miaka mitano toka siku alipokula kiapo.
Hata hivyo, alisema vifungu hivyo vinakinzana kisheria kwa kuwa
kimoja kinampa madara rais aliyopo madarakani kuongoza hadi pale rais
mwingine atakapopatikana, lakini kifungu kingine kinamwelezea kuwa
ataongoza kwa miaka mitano tu.
Kuhusu kufutwa kwa matokeo ya urais Zanzibar alisema hakuwezi
kuathiri matokeo ya uchaguzi wa matokeo ya Serikali ya Muungano kwa kuwa
ni serikali mbili zinazoendeshwa na Tume mbili tofauti za uchaguzi.
WAKILI NDUSIEPO
Lakini Wakili wa Kujitegemea, Apson Ndusiepo, alisema tukio la Zec
kufuta matokeo ya uchaguzi linaathiri moja kwa moja kwa Rais wa Muungano
kwa kuwa Rais wa Muungano hawezi kupatikan kabla ya kura za wananchi wa
Zanzibar.
Alisema sababu kubwa ni kutokana na uchaguzi huo kutokuwa wa uaminifu, haki na huru.
Alisema hadi Zec wanafikia hatua ya kufuta matokeo, inamaanisha uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.
Alisema Katiba ya Zanzibar haijaeleza kama endapo uchaguzi
ukisitishwa, serikali itaongozwa na nani, bali Katiba imeeleza tu endapo
rais akifariki dunia, akiugua ama akipata ugonjwa, nchi itaongozwa na
Makamu wa Rais.
MHADHIRI RUCO
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha
mkoani Iringa (RUCo), Rwezaura Kaijage, alisema hatua ya Zec kutangaza
kuufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kutokana na madai ya kugubikwa na
kasoro mbalimbali, kunaleta athari kubwa za kisheria katika matokeo ya
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema: “Baada ya Zec kutangaza kufuta uchaguzi huo na matokeo
yake yote, athari inayojitokeza ni kwamba wakazi wa Zanzibar watakosa
Rais wao katika muda mwafaka uliowekwa kikatiba, lakini pia kujiongezea
muda wa kukaa madarakani kwa Rais wa Zanzibar ni kuvunja katiba.
Alisema na kuongeza, Katiba inasema uchaguzi mkuu wa Zanzibar
utafanyika kila baada ya miaka mitano na ukomo wa Rais kimadaraka ni
vipindi viwili, hivyo Dk. Shein atakuwa amejiongezea muda kinyume cha
Katiba katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mwingine.”
Alisisitiza kitakachoathiri kisheria uhalali wa matokeo ya uchaguzi
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ni kwamba Rais mpya aliyechaguliwa
hawezi kutangazwa kwa sasa mpaka upande wa pili ambao ni Zanzibar ufanye
uchaguzi mkuu mpya, kitu ambacho kinaweza kikauvuruga mchakato mzima
licha ya kuwapo kwa mamlaka mbili ambazo ni Nec na Zec.
Kwa mujibu wa Kaijage, hata kama sheria inairuhusu Zec kufuta
uchaguzi huo kutokana na kuwapo kwa kasoro, ilipaswa ieleze sababu za
msingi ambazo si za kuiridhisha tume peke yake, lakini pia ziwe wazi
mbele ya Watanzania na walimwengu wote.
CHANZO:
NIPASHE


No comments:
Post a Comment