Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha.
Wakati Jumuiya ya Kimataifa ikitoa wito kwa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (Zec), iendelee na mchakato wa kuhesabu kura na
kuheshimu maoni ya wananchi kupitia sanduku la kura, tangazo la kufuta
uchaguzi huo limeibua maswali magumu yanayohitaji ufafanuzi wa kina.
Aidha, waangalizi wa kimataifa wameitaka Zec kuweka wazi ni vituo
gani kasoro zilizosababisha uchaguzi kufutwa kwa kuwa wanaamini kwamba
uchaguzi ulifanyika katika hali ya uwazi, amani na utulivu.
Juzi, Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, alitangaza kufuta
uchaguzi wa rais na wawakilishi Zanzibar kutokana na sababu tisa
mojawapo ikiwa ni kutofahamiana (kutoelewa), kwa wajumbe wa ndani ya
tume na kufikia hatua ya baadhi ya wajumbe kuvua mashati na kuanza
kupigana.
Swali: Ni katika kituo gani tukio hili lilitokea? Je, liliripotiwa kwenye mamlaka husika?
Sababu ya pili ya kufutwa kwa uchaguzi huo ni baadhi ya wajumbe
badala ya kuwa makamishna wa tume wamekuwa wawakilishi wa vyama vyao
wakati kuna vyama ambavyo vilishiriki uchaguzi, lakini havina wajumbe
ndani ya Zec.
Swali: Ni nani mlalamikaji katika hilo?
Sababu nyingine kwa mujibu wa Jecha ni kugundulika kwa kasoro
nyingi katika uchaguzi huo miongoni mwake ni baadhi ya vituo hasa Pemba
kuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapigakura wa kituo husika huku
wapiga kura wengine wakiwa hawajachukua vitambulisho vyao.
Swali: Ongezeko hili la wapigakura lilibainika kwenye vituo vipi na
hatua gani zilichukuliwa na Zec? Je, kwa uandikishaji kupitia Biometric
Voters Registration (BVR), iliwezekanaje wananchi kuacha vitambulisho?
Sababu ya nne ni uhamishaji wa masanduku ya kura na kuhesabiwa nje ya kituo kinyume na taratibu.
Swali: Uhamishaji huu ulitokea katika vituo vingapi, majimbo gani na Zec au Polisi walichukua hatua gani?
Sababu ya tano kwa mujibu wa Jecha ni kutolewa nje na kupigwa kwa
mawakala wa vyama vingine, hasa wa chama cha Tadea visiwani Pemba.
Swali: Uhalifu huu ulitokea kwenye vituo gani na Polisi walichukua hatua gani?
Kasoro ya sita iliyosababisha kufutwa kwa uchaguzi ni kuvamiwa kwa
vituo na vijana walioonekana kuandaliwa na vyama vya siasa na kufanya
fujo kwa kupiga watu na kuzuia watu wasiokuwa wa vyama vyao kufika
katika vituo vya kupiga kura na kupiga kura.
Swali: Hili nalo lilitokea katika vituo vipi na polisi walichukua hatua gani?
Ya saba ni vyama vya siasa kuonekana kuingilia majukumu ya Tume ikiwamo kujitangazia ushindi na kupeleka mashinikizo kwa tume.
Swali: Mamlaka ya Zec yanafutwa na hili?
Sababu ya nane ni kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa vyama
mbalimbali yanayoashiria kutoridhika na mchakato mzima wa upigaji kura,
kuhesabu na kutoa matokeo.
Swali: Ni vyama vingapi vinalalamikia uchaguzi huo?
Sababu ya tisa ya kufuta uchaguzi wa Zanzibar ni namba katika fomu
za matokeo vya vituo vingi vya Pemba kuonekana kufutwa na kuandikwa upya
namba nyingine juu yake.
Swali: Zec imechukua hatua gani kwa wahusika wa uhalifu huu na je, hili lilitokea katika vituo gani?
Kutokana na wadadisi wa masuala ya kisiasa kuuliza maswali hayo,
mwanasheria nguli nchini, Prof. Chris Peter Maina, aliiambia Nipashe
jana kuwa:
“Siyo rahisi kujua kilichotendeka Zanzibar kwa sababu kasoro
zimekuwa za ujumla mno. Mambo mengine hayana ushahidi kwa sababu hata
tume yenyewe (Zec), imegawanyika na haijulikani ninini hasa kilitokea.
Ni vigumu kueleza kisheria kinachoendelea Zanzibar.”
UINGEREZA, IRELAND
Uingereza na Ireland zimetoa taarifa ya pamoja zikieleza
kusikitishwa na tangazo la Jecha la kufuta uchaguzi na kutaka tangazo
hilo lifutwe na mchakato wa kuhesabu kura uendeleee.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana na Ubalozi wa Uingereza ilieleza kuwa
waangalizi wa kimataifa walivutiwa na ubora wa mchakato wa uchaguzi wa
Zanzibar, hivyo wameitaka Zec kuendelea kuhesabu kura na kutoa matokeo
bila kuchelewa. “Tunawapongeza watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna walivyoshiriki uchaguzi kwa shauku na amani.
Tunatoa wito kwa wadau wote wa kisiasa kutafuta ufumbuzi ambao
unaheshimu matakwa ya watu wa Zanzibar kama walivyoonyesha katika
uchaguzi wa Oktoba 25,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo fupi.
Iliongeza: “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina heshima kubwa ya
amani, utulivu na kuheshimu misingi ya demokrasia. Tunawaomba
Wazanzibari wote waendelee kudumisha amani na tunawapongeza kwa utulivu
waliouonyesha hadi sasa.”
MAREKANI
Marekani imetoa tamko ikieleza kushtushwa na uamuzi wa kufutwa kwa
matokeo ya uchaguzi ambao umeonekana kufanyika vizuri na kwa amani.
“Tunatoa wito wa kuondolewa kwa tamko hilo na kuzisihi pande zote
kudhamiria kwa dhati kuukamilisha mchakato huo wa kidemokrasia kwa uwazi
na amani. Watu wa Zanzibar wanastahili jambo hilo,” ilieleza taarifa ya
ubalozi huo nchini.
WAANGALIZI WA KIMATAIFA
Waangalizi wa Jumuiya ya Kimataifa ambao ni Jumuiya ya Madola,
Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC), wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali ya Zanzibar na
kutoa wito wa uwazi kwenye mchakato wa uchaguzi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kama walivyoeleza Oktoba 27, upigaji kura ulikuwa huru. “Tathmini yetu kwa ujumla kuanzia upigaji na kuhesabu kura katika
vituo vya kupigia kura, kwa kuzingatia uchunguzi wetu ni kwamba
ulifanyika katika hali ya amani na kwa maandalizi mazuri kwa mujibu wa
taratibu zilizoainishwa katika sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na sheria za Zanzibar. Bado tunasimama katika tathmini hii,” ilieleza
na kuongeza:
“Tulifurahishwa kwamba mchakato wa upigaji na kuhesabu kura
ulifanyika katika hali ya amani na kwamba wananchi wa Tanzania
walionyesha dhamira kubwa ya mchakato huu wa kidemokrasia kwa kujitokeza
kwa idadi kubwa kupiga kura,” ilieleza taarifa hiyo.
Walishauri kuwa wadau wote hususan uongozi wa kisiasa Zanzibar kuwa
mchakato huo ungehitimishwa kwa kuangalia umoja wa kitaifa, maridhiano,
amani na utulivu.
“Kwa heshima tunaiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuweka bayana
vituo vya kupigia kura ambavyo kulikuwa na kasoro. Tunatoa wito kwa Zec
kutoa uamuzi wake wa kufuta uchaguzi kwa uwazi kamili. Tunauomba uongozi
wa kisiasa wa Zanzibar kuweka kando tofauti zao na kuweka maslahi ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kwanza, na kukaa pamoja ili
kupata utatuzi wa haraka kwa masuala ambayo yamesababisha hali hii.
Demokrasia, amani na umoja Zanzibar upo hatarini.” Ilieleza taarifa
hiyo.
EOM WAZUNGUMZA
Waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EOM),
wameeleza kuwa uchaguzi wa urais uliofutwa Zanzibar ulifanyika kwa amani
na uwazi kutoka katika vituo vya kupigia kura hadi hatua ya kuhesabu.
Kiongozi wa ujumbe huo, Moody Athur Awori, alisema viongozi wa
kisiasa nchini wanapaswa kutatua tatizo lililopo ili kuleta demokrasia
na amani katika nchi.
UMOJA WA MATAIFA
Umoja wa Mataifa (UN), umetoa wito kwa viongozi wa kisiasa nchini
kukuza mazingira ya mazungumzo ya amani ili kutatua tofauti zao na
kuhakikisha muendelezo wa mchakato wa uchaguzi wa kidemokrasia na wa
amani.
Taarifa ya Mratibu Mkazi wa UN nchini, Alvaro Rodriguez, ilieleza
jana kuwa ni kupitia katika mchakato wa amani na wa kidemokrasia ndipo
maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanaweza kufikiwa.
“UN inafuatilia kwa ukaribu uchaguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika
Oktoba 25, na tunampongeza rais mteule pamoja na wananchi wa Tanzania
kwa kutimiza haki yao ya kidemokrasia kwa njia ya amani,” alisema
Alisema wanalirejea tamko la waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi
huo (Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika na Umoja wa Ulaya) lililotolewa jana, likionyesha
kufurahishwa kwao na shughuli ya kupiga kura na kuhesabu ilifanyika
kwenye mazingira ya amani.
Hata hivyo Rodriguez alisema, waangalizi hao, ubalozi wa Marekani
na wa Uingereza wameonyesha wasiwasi wao mkubwa na kauli iliyotolewa na
Mwenyekiti wa Zec Zanzibar ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa
Zanzibar.
ACT-WAZALENDO
Nacho Chama cha ACT-Wazalendo kimeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa tangazo la Zec kufuta uchaguzi visiwani Zanzibar.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba, ilieleza
jana kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki na kwamba haina mantiki kwa kuwa
waangalizi mbalimbali wa ndani na nje wameshatoa taarifa yao ya awali
wakieleza waziwazi kwamba uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar
ulifanyika katika mazingira ya uwazi, haki na uhuru.
“Wananchi wamefanya maamuzi kupitia sanduku la kura…chama chetu
hakikubaliani na maamuzi ya Jecha kwa kuwa maamuzi hayo hayana msingi wa
kisheria na yalifanywa na Jecha binafsi kwa kutumia vibaya kofia yake
ya uenyekiti wa Tume,” ilieleza taarifa hiyo.
ACT-Wazalendo pia imeitaka Zec imalize haraka mchakato wa uchaguzi na kumtangaza mshindi kwa kuzingatia kura za wananchi.
UTATA
Wakili Mwandamizi wa Kujitegemea ambaye hakutaka jina lake litajwe
akizungumza na Nipashe, alisema kufutwa uchaguzi wa Zanzibar itakuwa
vigumu kuitisha Baraza la Wawakilishi ambalo limemaliza muda wake
lililomalizika muda wake kwa ajili ya kupanga tarehe nyingine.
Alisema kufuatia uamuzi huo, kuna mgongano wa kisheria kwamba nani
atakayepanga tarehe ya uchaguzi mpya kama ni Zec ama Baraza la
Wawakilishi.
“Hata rais aliyatetea kiti hicho atapanga tarehe kwa mamlaka gani
ya kikatiba kwa kuwa tayari Baraza la Wawakilishi lilishavunjwa tamko
la kufuta uchaguzi lina uzito wa kisheria,” alisema.
Naye Wakili Juma Thomas, alisema inapotokea dharura Baraza la
Wawakilishi au Bunge linaitishwa kwa ajili ya kushughulikia dharura
hiyo.
Alisema wawakilishi wanaoitwa kwenye dharura ni wale walikula kiapo hata kama baraza hilo limevunjwa.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment