
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi
(CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema sababu kubwa ya kufutwa
matokeo ya uchaguzi Zanzibar ni baada ya juhudi za kutaka kumtangaza
mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein kuwa mshindi wakati
hakushinda kukwama.
Maalim Seif alisema hayo wakati akizungumza na Nipashe mjini hapa
jana, huku akisisitiza msimamo wake bado upo palepale wa kuitaka Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (Zec) iendelee kuhakiki matokeo yalioyobakia na kisha
kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.
“Sababu kubwa ya uchaguzi kufutwa baada ya juhudi za kulazimisha
mgombea wa CCM Dk. Shein kuwa mshindi wakati hakushinda kukwama na sie
hatutakubali maamuzi ya kidemokrasia ya wananchi kupigwa teke na watu
wachache,” alisema.
Maalim Seif alisema uamuzi alioufanya Mwenyekiti wa Zec, Jecha
Salim Jecha, ni sawa na kufanya mapinduzi ya kuondoa utawala madarakani
jambo ambalo ni kinyume na misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.
“Kilichofanyika ni sawa na kufanya mapinduzi kama wananchi
wamefanya maamuzi ya kuchagua kiongozi wanaemtaka haiwezekani watu
wachache wapinge maamuzi ya wananchi na kuingiza nchi katika mgogoro wa
kikatiba?” alihoji.
Maalim Seif ambaye anawania wadhifa huo kwa mara ya tano, alisema
Cuf inaendelea kuchukuwa hatua za kidemokrasia kuhakikisha uchaguzi huo
unaendelea ikiwamo kuhakiki majimbo yaliyobakia na kuyatangaza na kama
juhudi za kidiplomasia zitashindwa chama hicho kimepanga hatua za
kuchukua ili haki ya wananchi ipatikane.
Mgombea huyo alisema uamuzi wa Mwenyekiti wa Nec kufuta matokeo
yote unavunja Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na sheria
mbalimbali za uchaguzi ikiwamo kifungu cha 119 (1) kinachoanzisha tume
ya uchaguzi na tume hiyo haitakiwi kufanya maamuzi bila ya suala husika
kujadiliwa na kukubaliwa na akidi ya wajumbe inayotakiwa kabla ya
wajumbe kuamua.
Alisema hatua ya makamishna wawili wa Zec kutofautiana na uamuzi wa
mwenyekiti wao, Cuf ina amini uamuzi wa kufuta uchaguzi ulikuwa ni
uamuzi binafsi wa mwenyekiti huyo, kitendo ambacho ni kinyume cha
kifungu cha 119(10) ambacho kinaitaka tume izingatie kila uamuzi
ujadiliwe na uungwe mkono na wajumbe walio wengi.“Kwa sababu tume
haikukaa pamoja ikiwa na mwenyekiti au makamu mwenyekiti na angalau
wajumbe wanne na kwasababu na uamuzi uliotolewa ulikuwa ni wa peke yake,
kikatiba ni batili na hauna nguvu zozote,” alisema Maalim Seif akiwa
ameongozana na Mwenyekiti wa kampeni wa Cuf, Nassor Ahmed Mazrui na
msaidizi wake Mansor Yussuf Himid.
“Majimbo 31 ya uchaguzi yameshahakikiwa na tume na matokeo yake
kutangazwa baada ya kusainiwa na mwenyekiti na kubakia 23 yakiwamo 18 ya
Pemba na hakukuwa na kasoro zilizojitokeza, tunamtaka arudi kazini
kumalizia kiporo kilichobakia,” alisema.
Maalim Seif alisema uamuzi wa Mwenyekiti wa Zec wa kufuta matokeo
yote ya uchaguzi umeiingiza Zanzibar katika mgogoro mkubwa wa kikatiba
na kwamba kuanzia Novemba 2, mwaka huu visiwa hivyo vitakuwa havina
Rais kwa vile aliyepo sasa atakuwa amemaliza muda wake wa miaka mitano
kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1984.
Aidha, alisema kifungu cha 92 (1) cha Katiba ya Zanzibar kinaelezea
uhai wa Baraza la Wawakilishi ni miaka mitano tokea lilipoitishwa na
kwamba baraza jipya linatakiwa kuitishwa ndani ya siku 90 kama
kinavyosisitiza kifungu cha 90 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
“Ni Rais yupi ataitisha baraza la wawakilishi, yote haya yanaleta
mgogoro wa kikatiba ambao umesababishwa na mtu mmoja anaeitwa Jecha
Salum Jecha kwa sababu tu ya kufuata maelekezo ya chama chake cha CCM,”
alisema. Maalim Seif alitoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa
Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar,.
Dk. Ali Mohamed Shein, kubeba dhamana ya uongozi kwa siku chache
zilizobakia za uongozi wao kwa kusimamia katiba na sheria za nchi
ikiwamo kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari yaliofanywa Oktoba 25, mwaka
huu kupitia uchaguazi mkuu na kuzuia matumizi ya nguvu yanayofanywa na
vyombo vya ulinzi dhidi ya raia.
WAGOMBEA WENGINE WAGOMA
Wakati huohuo, wagombea sita wa nafasi ya urais wa Zanzibar wametoa
msimamo wa pamoja kuwa hawako tayari kushiriki uchaguzi wa marejeo
iwapo tume ya uchaguzi itashindwa kuendelea kuhakiki matokeo ya uchaguzi
na kumtangaza mshindi.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar JANA, wagombea
wa vyama vya Demokrasia Makini, Sau, Chaumma, NRA, Jahazi Asili na DP,
walisema sababu alizotoa mwenyekiti wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi
huo hazina mashiko ya kikatiba na kisheria kwani kasoro ndogondogo
zilizojitokeza tume ilikuwa na uwezo wa kufanya marekebisho bila
kuathiri uchaguzi wote.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment