Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(Chadema), anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameitaka Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec), kusitisha kutangaza matokeo ya urais yanayoendelea
kutangazwa.
Kadhalika, Lowassa ameitaka Nec kuhesabu upya matokeo hayo kwa kutumia mfumo usio wa kidijitali (manual). Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam, kuhusiana na mwenendo mzima wa utangazaji
wa matokeo hayo.
Lowassa aliitaka Nec isitishe kutangaza matokeo hayo kwa maelezo kuwa siyo matokeo halisi bali, yamechakachuliwa.
Kwa mujibu wa Lowassa, matokeo ambayo waliyakusanya wenyewe kabla
ya vituo vyao kuvamiwa na Jeshi la Polisi, yalikuwa yanaonyesha kuwa
Chadema imeshinda kwa zaidi ya asilimia 60, lakini wanashangaa matokeo
yanayotangazwa na Nec, ambayo yanaonyesha kuwa Mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameshinda.
Alidai kuwa yapo majimbo mengi ambayo kura za mgombea wa Chadema zimepunguzwa na kuongezewa mgombea wa CCM. “Mimi pamoja na Mgombea Mwenza, Dk. Juma Duni Haji, kwa pamoja
tunawaambia Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa hatukubaliani na
matokeo hayo, na tunaiomba Nec isitishe kutangaza na kuanza kuhakiki
upya matokeo hayo kwa mfumo usio wa kidijitali,” alisema Lowassa.
Lowassa aliongeza: “Wasipositisha tutakaa tujadili namna ya kuchukua hatua nyingine.”
JUMA DUNI HAJI
Kwa upande wake, Duni alisema pamoja na matukio yaliyojitokeza
katika uchaguzi huo ikiwamo matukio ya kukamatwa kwa masanduku ya kura
bandia, lakini Nec haijatoa tamko lolote.
Alitolea mfano kwa majimbo ambayo alidai kuwa Dk. Magufuli
ameongezewa kura kuwa ni Makunduchi ambalo ameongezewa kura 2,650,
Donge kura 357, Kiwengwa kura 3,889, Kwahani kura 2,530, Chalinze kura
100 na Mkuranga kura 1,000.
FREDERICK SUMAYE
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mtaafu, Frederick Sumaye, ambaye
alisaidia kampeni za Ukawa, alisema mpango wa uchakachuaji ulipangwa
mapema.
“Mimi nashangaa kwamba, inawezekanaje masanduku ya kura ambayo ni
nyaraka za ndani za Nec ambazo zinapaswa kulindwa, zikapatikana kwa
watu, hapa kuna mawili ama imeshiriki au imezidiwa nguvu,” alisema na
kuongeza: “Lakini ni kwa nini mpaka sasa Tume haijasema lolote juu ya tukio hilo.”
JAMES MBATIA
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa na Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema hatua ya Nec ya kuendelea kutangaza
matokeo ni batili na kwamba kuna mgogoro mkubwa wa kitaifa kutokana na
kinachoendelea.
Mbatia alisema wanafanya vikao kujadili kabla ya kuamua hatua mbalimbali watakazozichukua.
SAEED KUBENEA
Kwa upande wake, Mbunge Mteule wa jimbo la Ubungo, Saeed Kubenea,
alisema kwa upande wa jimbo hilo wamekataa kusaini matokeo ya urais kwa
kile alichodai kura za Lowassa zimechakachuliwa.
Aidha, Lowassa aliwataka Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati hatua mbalimbali zikichukuliwa. “Ninawaomba wananchi wasishtuke kwa hiki kinachoendelea hivi sasa,
ninaomba muwe watulivu wakati hatua nyingine zinachukuliwa na nawaomba
vijana wasifanye fujo zozote,” alisema.
NEC: HATUCHAKACHUI MATOKEO YA URAIS
Hata hivyo, Nec imezikanusha tuhuma hizo na kueleza kuwa haiko tayari kuendelea kulumbana na vyama vya siasa au wagombea.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kutangaza matokeo ya
majimbo 51 ya urais yaliyopokelewa usiku wa kuamkia jana na kufanya
jumla ya majimbo 164 yaliyotangazwa hadi jana saa 6:00 mchana, Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema matokeo
yanayotangazwa ndiyo yaliyopokelewa kutoka kwenye majimbo husika.
Jaji Lubuva alisema matokeo yanayotangazwa yameshahakikiwa na
kukubaliwa na mawakala waliopo katika majimbo husika na kwamba Chadema
ina wakala kila kituo anayeyakubali. “Tunachosoma ni hukumu ya wananchi wenyewe, upotoshwaji unaofanywa
haukubaliki, ni mbaya sana kwa Nec inayofanya kazi zake kwa mujibu wa
sheria na Katiba, hatujaongeza hata nukta, tunatangaza jinsi
walivyotuletea,” alisema Jaji Lubuva.
CHANZO:
NIPASHE


No comments:
Post a Comment