Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ambaye alikuwa mafichoni kwa
zaidi ya mwezi mmoja, jana aliibuka na kuzungumza mambo mbalimbali huku
akitoa hutuma zisizo na ushahidi dhidi ya watu kadhaa.
Dk. Slaa baada ya kutoa kauli mbalimbali katika mkutano wa waandishi wa habari, alitangaza rasmi kuachana na siasa. Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya kitalii ya
Serena, Dk. Slaa alisema ameamua kujing’atua katika siasa kutokana na
kutoridhishwa na mambo kadhaa ndani ya Chadema ukiwamo uamuzi wa chama
hicho kumpokea Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
UJIO WA LOWASSA
Dk. Slaa alikiri kuwa alihusika katika majadiliano ya kumpokea
Lowassa, lakini wakati wakifanya hivyo, aliweka wazi msimamo wake juu ya
namna ya kumkaribisha mwanasiasa huyo tangu hatua ya kwanza ya
mazungumzo hayo.
Alisema baada ya jina la Lowassa kukatwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) mjini Dodoma kugombea urais, mtu wake wa karibu, Askofu Josephat
Gwajima, alimpigia simu na kumuuliza kuwa mambo ya Dodoma yameiva nini
kifuate?.
Alisema baada ya kupokea simu hiyo, alijibu kuwa asubiri hadi atakapowasiliana na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. “Nilikuwa ofisini kwangu... nikaenda ofisini kwa Mbowe na
kumjulisha. Tukampigia simu askofu, akafika baada ya dakika 20,
tukajadiliana,” alisema Slaa.
Alisema yeye alikuwa na msimamo wa kumsikiliza Lowassa anataka nini
kwa kuwa Chadema ni chama cha siasa na hakikatai kumpokea mtu yeyote. Kwa mujibu wa Dk. Slaa, baada ya kukubaliana, waliwateua vijana
ili kujua wafuasi wa Lowassa wanataka kuja Chadema kufanya nini.
Alisema wakati wa majadiliano ya kumkaribisha Lowassa, yeye
aliweka misingi ya kumtaka Lowassa kutangaza hadharani kuwa ameondoka
chama chake CCM na kwamba, baada ya kutangaza hivyo, aseme vilevile
hadharani kuwa anakwenda chama gani.
Pia, alisema alitoa masharti ya kumtaka Lowassa aitishe mkutano wa habari na kujisafisha kwa tuhuma zote zinazomkabili. Dk. Slaa alisema misimamo hiyo yote aliyoitoa haikutekelezwa na Lowassa, badala yake alishangaa viongozi wa Chadema wanampokea.
Alisema aliweka msingi wa kumtaka Lowassa aeleze anakuja kujiunga
na Chadema kama mtaji au vinginevyo na kwamba hilo swali aliliweka tangu
siku ya kwanza ya vikao vya ndani vya chama chao.
“Lowassa anakuja Chadema kama Asset au Liability (mali au mzigo)...
ijulikane suala siyo urais kwa kuwa sikuchukua fomu yoyote ya kugombea
nafasi hiyo,” alisema Dk. Slaa ambaye kabla ya ujio wa Lowassa alikuwa
akitajwatajwa kuwa atagombea urais kupitia chama hicho kama ilivyokuwa
mwaka 2010.
Dk. Slaa alisema ili kujua kama ni Lowassa ni mali ama mzigo,
anapimwa kwa kukidhi kigezo kuwa je, anahamia Chadema na nani? Peke
yake? Na wafuasi hao ni wa aina gani? Au anakuja na viongozi serious
(makini) ndani ya chama?”
Alisema jibu alilopewa ni kuwa Lowassa anakuja na wabunge
wanaomaliza muda wao wasiopungua 50, wenyeviti wa mikoa wasiopungua 22
pamoja na wenyeviti 88 wa wilaya wa CCM. Alisema alisubiri majina ya wafuasi hao wanaojiunga Chadema kwa muda mrefu, lakini hakuyapata.
Dk. Slaa alisema 25, Julai Chadema walikaa kikao na kumfuata
nyumbani kwake na kumtaka kuitisha Kamati Kuu ya dharura Julai 27, kikao
ambacho hatimaye alikiitisha bila kupata majibu ya Lowassa kuwa anakuja
Chadema kama mali au mzigo.
Aliwataja washiriki wengine katika kikao hicho kuwa ni pamoja na
Tundu Lissu, Mbowe na Askofu Gwajima kutoka saa 3:00 asubuhi hadi saa
9:00 alasiri wakibishana kuhusu ujio wa Lowassa. Alisema kikao hicho kilivunjika na wakaenda katika kikao cha Kamati
Kuu kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 12:00 jioni na kikao hicho
kilivunjika kabla ya kuamuliwa kuundwa kamati ndogo ya kumshawishi Dk.
Slaa akubaliane na maamuzi ya kumpokea Lowassa.
Alisema baada ya hapo aliamua kuandika barua ya kujiuzulu kwa
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Profesa Abdallah Safari, lakini
iliishia kuchanwa. Alisema alipoandika barua ya pili kwa makamu mweyekiti wa chama
hicho Zanzibar na kumueleza kuwa anajiuzulu, alijibiwa kuwa anajisumbua
bure kwani mambo hayo yalikuwa yameshapangwa.
Alisema kesho yake, picha ilitoka kwenye vyombo vya habari na
viongozi wa Chadema walikanusha kuwa Lowassa hakuhudhuria kikao cha
Kamati Kuu.
Dk. Slaa alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake iliyorushwa na vituo
vitatu vya vya runinga takribani saa 1:15 kuwashambulia mawaziri wakuu
wa zamani waliokihama CCM hivi karibuni na kujiunga katika kambi ya
upinzani ambao ni Lowassa aliyeteuliwa na Chadema kugombea urais kwa
tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kugombea urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Frederick Sumaye. Dk. Slaa alielezea mambo kadhaa yakiwamo madai kuwa aliwahi kupewa
hongo ya Sh. milioni 500 na watu watatu ambao hakuwataja kwa nia ya
kumfunga mdomo kuhusu kashfa ya Richmond.
Katika tuhuma hizo dhidi ya Lowassa, pia Dk. Slaa aliwataja makada
wa CCM, Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta kumsaidia katika kuueleza
umma juu ya uhusika wa Lowassa katika sakata la Richmond.
Sitta alikuwa Spika wa Bunge wakati sakata la Richmond lilipoibuka
bungeni na Lowasa kujiuzulu wakati Dk. Mwakyembe alikuwa Mwenyekiti wa
Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa na Sitta kuchunguza mkataba wa
Richmond.
Alisema hivi sasa, Chadema inapokea makada walewale wa CCM
waliokuwa wakiwatangaza kila uchao kuwa ni mafisadi na wengine
wamepokewa kwa sifa ya kuwa ni wezi wazuri wa kura.
Alisema CCM imekuwa waoga kuchukua hatua kwa watu waliokiuka maadili akiwamo Lowassa aliyelelewa ndani ya chama hicho.
KUHUSU RICHMOND
Dk. Slaa alisisitiza kuwa mwaka 2008, Lowassa alihusika kwa
asilimia zote katika suala la Richmond, lakini leo anakumbatiwa na
kuitwa msafi.
Anasema yeye (Dk. Slaa) na Lowassa wana ugomvi baada ya kumwambia
kuwa aeleze hadharani Richmond ni ya nani, jambo ambalo hajalitekeleza
hadi sasa. Alisema wakati kamati ya Harrison Mwakyembe inawasilisha ripoti
bungeni, aliwahi kufuatwa (Dk. Slaa) na watu watatu waliotaka kumpatia
rushwa ya Sh. milioni 500 ili ripoti hiyo isiingie bungeni, lakini
alikataa.
Alisema suala la Richmond halikuanza katika utawala wa Rais Jakaya
Kikwete bali lilianza utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutokana na
dharura ya umeme. Alisema baada ya kuingia Kikwete madarakani Februari 10, 2006,
alipokea ripoti hiyo na kuiagiza kamati iendelee lakini ifuate sheria.
Alisema kipindi hicho waziri mkuu Lowassa alisimamia utekelezaji wa maauzi yote ya mkataba wa Richmond. “Halafu leo Lowassa anakuja kutuambia kuwa hakuhusika, maana yake
nini? Halafu amnawaeleza Watanzania kuwa asiye na ushahidi afunge
mdomo,” alisema Dk. Slaa.
Alisema Kamati ya Mwakyembe ilitoa mapendekezo kuwa Bunge lijadili
na lichukue hatua au Waziri Mkuu ajitathmini mwenyewe na achukue hatua
kama anaweza kuendelea, lakini Lowassa alikimbia kwa kuwa aliona bunge
lingemfukuza.
Hata hivyo, Lowassa amekaririwa akisema mara kadhaa kuwa hakuwahi
kuhusika na ufisadi wowote bali kinachoelezwa ni jitihada za wapinzani
wake kumchafua; na kwamba, kama kuna mtu ana ushahidi kuhusiana na
madai hayo autoe hadharani.
Kadhalika, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, David
Silinde, alikaririwa juzi akisema kuwa ndani ya Chadema walimhoji
Lowassa kwa zaidi ya wiki mbili na aliwaletea vielelezo kadhaa vikiwamo
vya sauti kuthibitisha kuwa hakuhusika katika sakata la Richmond na
ndiyo maana wakamkaribisha na kumteua kuwa mgombea wao wa urais.
KUWA LIKIZO
Kuhusu taarifa kuwa alipewa muda wa kupumzika Chadema na kuwa
atakuwa na nafasi ya kurejea kuendelea na shughuli za chama wakati
utakapowadia, Dk. Slaa alipinga taarifa hiyo na kusema hakuna ukweli
wowote kuwa likizo na kwamba hakuwahi kupewa barua yoyote ya kwenda
likizo.
Alisema ukweli wa jambo hilo ni kwamba yeye aliachana na siasa
tangu Julai 28, mwaka huu baada ya kuona yale yaliyokuwa yakifanyika
ndani ya chama chake hayamridhishi. “Mimi sikuwa likizo. Mengi yalisemwa kwenye vyombo vya habari
sikuwahi kupewa barua na mtu yeyote kwenda likizo,” alisema Dk. Slaa.
KUFUNGIWA CHUMBANI NA MKEWE
Dk. Slaa alisema hakuna ukweli wowote wa yeye kufungiwa na mkewe
Josephine na kwamba, maamuzi yote alikuwa akiyatoa yeye mwenyewe (Slaa)
pasipo kushawishiwa na mtu. Anasema mkewe Josephine ni Mtanzania na
aliwahi kukipandisha chama hicho tokea Januari 5, 2011.
Aliongeza kuwa hakuna ukweli wowote vilevile kuhusiana na madai
kwamba alikuwa analipwa milioni saba kila mwezi ili kukitumikia chama
hicho, bali ukweli ni kuwa mara zote alikuwa akitumia fedha zake
mwenyewe na familia yake ilikuwa ikila mihogo. “Mke wangu alizunguka nchi nzima katika harakati za ukombozi wa nchi kwa fedha zangu mwenyewe,” alisema Dk. Slaa.
AMVAA LOWASSA, SUMAYE
Alisema alitoa agizo la kumtaka Lowassa kuwaleta wabunge aliokuwa
anaeleza atakuja nao Chadema, lakini wabunge hao hawakuja hadi pale
walipoondolewa katika kura za maoni katika mchakato wa uteuzi ndani ya
vyama.
Alisema Wwatanzania wote wanafahamu kuwa Sumaye na Lowassa hawakuwa
watu safi na niliwahi kuwatuhumu mara kadhaa kwa ufisadi, huku akidai
kuwa aliwahi kugombana na Sumaye baada ya kiongozi huyo kuchukua shamba
la Magereza Kibaigwa na kulimiliki binafsi.
ASIYOYAFAFANUA DK. SLAA
Licha ya sehemu ya maelezo ya Dk. Slaa kueleza kwamba amekuwa akila
mihogo na familia yake, hakueleza kwa kina jana ni kwa namna gani
ameweza kuitisha mkutano na waandishi wa habari kwenye hoteli mojawapo
ya hadhi ya juu jijini Dar es Salaam jana.
Aidha, Dk. Slaa hakueleza pia ni kwa namna gani alifanikiwa kurusha
‘live’ mazungumzo yake na waandishi wa habari jana kupitia vituo vya
televisheni, tena kwa muda wa zaidi ya saa moja.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment