
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Asad.
Dhambi ya kuendelea kulipa mishahara hewa kwa
watumishi wa umma imesababisha serikali kupoteza Sh. bilioni 1.01
zilizokuwa zitumiwe na halmashauri na serikali za mitaa kwa mwaka wa
fedha unaoishia Juni 30, 2014.
Hasara hiyo imetokana na halmashauri 36 kulipa zaidi ya Sh. bilioni
1.0 kwa wafanyakazi marehemu, wastaafu, watoro na waliofukuzwa. Taarifa
hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) iliyotangazwa jana mjini Dodoma . Mkaguzi Mkuu ,Profesa
Musa Asad, alisema na kuongeza kuwa hali kama hiyo ilijitokeza kwenye
watumishi wa umma na serikali ambako zaidi ya Shilingi milioni 141. 4
zililipwa kwa mwaka huo.
Mkaguzi Mkuu alieleza kuwa marehemu walioacha kazi, wastaafu mbali
na kulipwa mishahara walilipiwa bima za matibabu, kodi ya mshahara
(Paye) na michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii. “Hili linatokana na kuchelewa kuwaondoa watumishi hao kwenye mtandao ya orodha ya mishahara ya watumishi wote.”
Aliongeza: “Hali hii bado inaendelea licha ya kuwa serikali
imewekeza kwenye mfumo wa kompyuta wa LAWSON kama njia mojawapo ya
kudhibiti upotevu huu,” alisema Mkaguzi Mkuu. Aliongeza kuwa milioni 845 zinazohusiana na halmashauri 32
zililipwa kama makato ya pensheni, bima ya afya, TRA kwa watumishi
hewa.
HUJUMA MADINI
Makampuni ya madini ya Geita Gold Mine na Resolute Tz Ltd,
yameisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 22.33 kwa kuhujumu
misamaha ya kodi waliyopewa. Wawekezaji hao walipewa msamaha wa kodi ya mafuta yanayotumika
kwenye migodi yake ambayo yana thamani ya Sh. bilioni 22.33, kwa mujibu
wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Musa Asad.
Alikuwa akizungumzia ripoti ukaguzi ya hesabu za serikali kwa mwaka unaoishia Juni 30,2014. Alisema ufisadi huo uliotokea kwa vile kampuni hizo, hazikutumia
mafuta hayo badala yake iliyatoa kwa wakandarasi wasiostahili msamaha
huo hivyo kutumiwa bila kulipiwa ushuru na kuisababishia serikali hasara
ya Sh. bilioni 22.33.
Alitaja ufisadi mwingine uliosababisha hasara ya Sh. milioni 392.7
ulifanywa na kampuni ya Kiliiwarrior Expeditions ya Arusha iliyokuwa
imesamehewa kodi ya Sh. milioni 465.2 ili kuingiza magari 28. Alifafanua kuwa kampuni hiyo ilitumia misamaha hiyo kinyume cha
malengo na Mamlaka ya Mapato (TRA) ilipata kiasi cha Sh. milioni 72.
CCM, CHADEMA CUF HATI MBOVU
VYAMA vya siasa vya CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi vimepata hati
zenye shaka zilizotolewa na Ofisi ya CAG, kutokana na taarifa za fedha
zisizoridhisha. Alisema vingine vilivyopata hati hiyo ni TLP na Chaumma, huku vyama
vya NLD, UMD, ADC, NRD, APPT na SAU vilipata hati mbaya ya ukaguzi.
Akizungumzia vilivyopata hati zenye shaka, alisema katika ukaguzi
wa vyama 12 ilibainika kuwa taarifa zao za fedha zilifanywa tofauti na
misingi ya uhasibu na mfumo wa uandaaji wa taarifa za fedha. Alieleza kuwa hadi Juni mwaka 2013 hesabu za vyama vya siasa 21
zilikaguliwa kati ya hivyo ni vyama 12 vilivyowasilisha taarifa zake
wakati vyama tisa havikuwasilisha taarifa.
“Vyama hivi ni UPDP, TADEA, UDP, Demokrasia Makini, CHAUSTA, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.” Alisema Profesa Asad. Alisema katika ukaguzi wa taarifa za fedha tatizo la kuchelewesha
uwasilishaji ripoti za fedha za vyama kwa CAG limejiri na kupendekeza
kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya
Wahasibu waandae muongozo wa aina ya muundo wa taarifa za fedha
utakaotumiwa na vyama vyote vya siasa.
MASHIRIKA YANAYOCHAKACHUA
Pia GAC ameitaja Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro kuwa imefanya
ufisadi wa zaidi ya Sh. bilioni 2.3 (Dola milioni 5.54) kwa kununua
bidhaa zisizokuwa na sababu ya msingi. Pia Kampuni ya Simu ya TTCL nayo ilinunua manunuzi yasiyokuwa na
lazima yenye thamani ya Sh. milioni 381.97 (Dola 986, 938) kama
ilivyofanya Ngorongoro.
Kadhalika imelitaja Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC) kuwa
limefanya manunuzi bila kushindanisha wazabuni yenye thamani ya Sh.
bilioni 1.75. Kwa upande wa deni la serikali katika mifuko ya hifadhi ya jamii
limefikia Sh. bilioni 1.6 Juni mwaka jana, kwa mujibu wa Mkaguzi Mkuu
Profesa Mussa Asad.
Akizungumzia suala la kukataa kutumia mashine za stakabadhi za
kielektroniki (EFDs) , ameshauri serikali isifanye biashara na kampuni
kama haitumii EFDs. Alisema ofisi yake ilibaini kuwa yamefanyika malipo ya Sh. bilioni
4.4 yasiyo ya risiti hizo kwenye serikali kuu, wakati malipo mengine
ya Sh. bilioni 4.6 yalifanywa kwa halmashauri mbalimbali.
Alisema ili kuondoa kiburi cha kukataa EFDs serikali kuu na zile za mitaa zisifanye biashara na wasiotumia risiti hizo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment