Pages

Tuesday, May 12, 2015

STEPHEN WASIRA: WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira
Kati ya mwaka 1964–1967, Wasira alisoma elimu ya Sekondari katika Chuo cha Ukufunzi Uingereza (British Tutorial College) na kuhitimu kidato cha nne.
Historia yake
Stephen Wasira alizaliwa mwaka 1945 katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara (ana miaka 70). Alisoma katika shule tatu tofauti, ya kwanza ni Shule ya Msingi Bariri 1956-1959, ya pili ni Shule ya Msingi Nyambitilwa 1960–1961 na kisha akamalizia Shule ya Msingi Kisangwa mwaka 1962 - 1963.
Kati ya mwaka 1964–1967, Wasira alisoma elimu ya Sekondari katika Chuo cha Ukufunzi Uingereza (British Tutorial College) na kuhitimu kidato cha nne.
Wakati anasoma sekondari (1965–1967), pia alifanya kazi akiwa msaidizi wa masuala ya maendeleo ya jamii na alipohitimu kidato cha nne alianza kuitumikia Tanu akiwa katibu wa wilaya mwaka 1967-1973.
Mwaka 1975–1982 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mwaka 1982 akateuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington, D.C. Alipokuwa huko alisoma na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi na Uhusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Amerika (American University) kilichopo Washington DC mwaka 1982–1985.
Wasira alisoma Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Umma kati ya mwaka 1985–1986 na aliporejea nchini kuendelea na utumishi wa uwakilishi wa wananchi, aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 1990-1991.
Kati ya mwaka 1993–1995 alisoma tena Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Amerika.
Ndani ya chama chake CCM, amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) tangu mwaka 2007 na mwaka 2012 akachaguliwa katika wadhifa huo na tena kwa kura nyingi kuwashinda wajumbe wote wa Tanzania Bara. Lakini pia amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM tangu mwaka 2011 na tena 2013 hadi sasa.

Mbio za ubunge
Wasira alianza utumishi wa ubunge akiwa na miaka 25, hii ilikuwa mwaka 1970 aliposhinda ubunge wa Jimbo la Mwibara na akaongoza hadi mwaka 1975 huku Rais Julius Nyerere akimteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Mwaka 1985, Wasira aligombea na kushinda ubunge wa Jimbo la Bunda (wakati huu likiwa limemeguliwa kutoka lilikuwa Jimbo la Mwibara. Katika kipindi hiki aliteuliwa na Rais Mwinyi kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na baadaye Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo mwaka 1989 hadi 1990.
Kipenga cha vyama vingi kilipopulizwa mwaka 1995, Wasira alihitaji kuwaongoza wana Bunda lakini akaangushwa kwenye kura za maoni za ndani ya CCM, aliyemwangusha ni Jaji Joseph Warioba (Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu). Wasira hakuridhishwa na ushindi wa Warioba na aliamua kuihama CCM na kwenda NCCR Mageuzi wakati huo ikiwika na akachaguliwa kwa kura 18,815 dhidi ya 17,527 za Warioba na hivyo akawa mbunge kupitia NCCR.
Warioba alikata rufaa Mahakama Kuu nayo ikatengua ubunge wa Wasira mwaka 1996 baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na rafu nyingi zilizofanyika ikiwamo matumizi ya rushwa na ikampiga marufuku kugombea kwa miaka kadhaa. Wasira alikata rufaa mara kadhaa na kushindwa. Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu.
Uchaguzi wa marudio ulipofanyika mwaka 1999 Wasira alikuwa amekwishatangaza kuihama NCCR kutokana na siasa za ugomvi na mara hii alimuunga mkono mgombea wa UDP, Victor Kubini lakini mara baada ya uchaguzi huo aliamua kurejea CCM. Miaka mitano iliyofuatia (2000 – 2005) na hata minne iliyopita (1996 – 2000), Wasira alijielekeza katika biashara ya kusafirisha mazao ya bahari nje ya nchi.
Alirejea katika ulingo wa siasa mwaka 2005 na kushinda kura za maoni ndani ya CCM na akapitishwa kugombea ubunge wa Bunda na akapita bila kupingwa. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Maji Januari 2006- Oktoba 2006.
Kati ya Novemba 2006 – Novemba 2010 alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, lakini Februari–Mei 2008 aliwahi kutumikia kwa muda Ofisi ya Waziri Mkuu akiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Wasira aligombea tena ubunge wa Bunda na kushinda kwa asilimia 66.1 na Rais Kikwete akamteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu kabla ya mwaka huu kurudishwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

Mbio za urais
Wasira ni miongoni mwa wana CCM ambao bado hawajatangaza rasmi kuwania nafasi hiyo, lakini amewahi kunukuliwa mwaka jana akisema yupo tayari kwa hilo. Aliwahi kufanya mahojiano na gazeti moja la kila wiki, Septemba 2014 na kuthibitisha kuwa ataomba ridhaa hiyo kwa kile alichokiita “maombi mengi kutoka kwa wanaCCM wanaoona anaweza kukabiliana na changamoto zinazolikabili Taifa katika wakati huu”
Wasira amenukuliwa akithibitisha jambo hilo kwa kusema “Kwa kifupi, nimekwishashauriwa sana, lakini nasubiri ruhusa ya kanuni za chama. Kwa kweli kwa kiasi kikubwa nimeshafikia uamuzi wa kugombea. Nitagombea kupitia CCM.”

Nguvu yake
Wasira ni mmoja wa mawaziri maarufu katika Serikali ya Kikwete, mwonekano wake, vituko vyake, uongeaji wake na kila anachokifanya, kinamtofautisha mno na wenzake. Umaarufu huu una maana kubwa kwa mtu anayehitaji kuongoza nchi, kufahamika ni muhimu na hili ameshalivuka.
Pili, amekuwa na rekodi nzuri ya kiutendaji katika awamu zote alizopitia. Uchapakazi, ufuatiliaji na usimamizi ni moja ya sifa kubwa za Wasira kwa watu waliofanya naye kazi. Rekodi hii pia inamuongezea alama muhimu.
Tatu, amekuwa mhimili muhimu wa Serikali ya Kikwete na ndiyo maana ili kujipunguzia mzigo wa kazi na kuhitaji mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi katika Ofisi ya Rais, Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu. Wasira anakuwa mmoja wa watu walio karibu sana na Rais Kikwete kushinda watu wanavyofikiria. Hii ni nguvu nyingine muhimu kwake.
Mwisho Wasira ni mcheshi na ni mtu wa kawaida sana. Kwa wanaomfahamu wanajua kuwa hajajitengenezea “himaya binafsi”, uwezo wa kifedha wenye kuibua shaka na mambo mengine kama hayo. Maisha haya ya kawaida yanamfanya awe mmoja wa viongozi wa kawaida. Lakini zaidi ya yote, anapenda mijadala, kubishana na kushindanisha hoja na ni rahisi hata kuwamudu vijana.

Udhaifu wake
Kauli za vitisho na zinazoashiria udikteta. Moja ya udhaifu mkubwa wa Wasira ni kupenda kudharau haki, hoja na hata madai ya watu wengine. Mathalani, zilipotokea vurugu kadhaa katika mikutano ya vyama vya siasa zikihusisha polisi kuzuia shughuli za vyama hivyo na baadaye mapambano ya polisi na raia na labda raia kuuawa, Wasira alijitokeza hadharani na kushangaa kwa nini Msajili wa Vyama vya Siasa hajavifuta, ilhali akijua kwamba waliozuia mikutano ya vyama kinyume na sheria inavyotaka ni Polisi na walioua Raia ni polisi. Kauli hizi zinaashiria kuwa Wasira ni mtu anayeamini katika dola zaidi kuliko haki na mustakabali wa wananchi.
Jambo jingine ni “ubishi na ujuaji”. Ukimsikiliza Wasira katika vyombo vya habari, bungeni na kwingineko, unaona kabisa kuwa kauli zake mara zote hazitolewi kujibu maswali yaliyoulizwa au kutatua matatizo yaliyopo, bali maswali hayo huishia kuuliza maswali mengine kwa kejeli na weledi mkubwa wa kiuzungumzaji.
Kwa mfano, alipoulizwa na mwandishi mmoja wa habari juu ya kuteswa na kuumizwa kwa Absalom Kibanda, Wasira alijibu: “…Kibanda ni nani katika siasa za vyama vingi Tanzania hadi Serikali imsake na kumtesa? Yeye siyo Mbowe, Slaa au Lipumba. Hata kama Serikali ingeamua kupambana na maadui zake Kibanda bado hawezi kufuzu kwa sababu yeye hayuko chama cha upinzani.”
Unaweza kuona kuwa mwandishi amemuuliza swali muhimu ambalo lilihitaji ufafanuzi mkubwa wa Serikali, badala ya kulijibu, anaanza kumshusha Kibanda na kuonyesha kuwa si lolote wala chochote katika ulingo wa raia muhimu katika nchi.
Wangapi tunajua mchango wa Kibanda katika kusimamia ukuaji wa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari Tanzania? Kwa nini waziri mwenye hadhi ya Wasira haanzi hata kusema alivyosikitishwa kutokana na kuumizwa vibaya kwa mhariri huyo mwandamizi na badala yake anaanza kuonyesha kuwa “Kibanda si lolote”. Kauli hizi zisidharauliwe hata kidogo, ndizo zinapaswa kuwagutusha wananchi kujua aina ya viongozi wao wanaohitaji kuongoza dola.
Nilikuwa najiuliza, Kama kesho Wasira akiwa Rais wa nchi hii halafu mwandishi mwingine ameuawa au kuumizwa, atajibu nini? Unaposhindwa kuwa mwaminifu na mlinzi wa maisha na haki za watu unapokuwa mdogo, huwezi kujifunza kufanya hivyo utakapokuwa mkubwa.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe
Kama Wasira atapitishwa na CCM, basi uzoefu wake ndani ya chama hicho na Serikali itakuwa moja ya silaha zilizomvusha. Uzoefu wa Wasira ndani ya CCM na Serikali wa miaka zaidi ya 50, unambeba. Huyu anaweza kuwa waziri mwenye uzoefu mkubwa katika Baraza la Mawaziri la Kikwete kuliko mwingine yeyote. CCM ikihitaji mtu mkongwe ili awe mgombea wake bila shaka Wasira ndiye atakuwa moja ya chaguo muhimu.
Lakini pia, Wasira anaungwa mkono na makundi hasimu ndani ya CCM. Mara kadhaa imeelezwa namna makundi hasimu yanavyovutana kiasi cha kutishia uhai wa mbele wa chama hicho. Bahati aliyo nayo Wasira ni kuwa mmoja wa watu ambaye anaheshimiwa mno na makundi husika. Kama CCM itahitaji kutuliza hali ya ndani ya chama chake kwa kupata mtu ambaye hatatumia nguvu kubwa kuyaunganisha makundi hasimu, basi Wasira ni mmoja wao.
Kwa kiasi fulani, Wasira ana uwezo mkubwa wa kushughulikia masuala ya kimataifa. Hata nchi yetu ilipopata ugeni mkubwa wa Rais Barack Obama wa Marekani, nimeambiwa kuwa ni Wasira ndiye aliyekabidhiwa jukumu kubwa la kuwa karibu na wageni muhimu na kuwaelekeza masuala muhimu.
Kuna taarifa kuwa kulitokea manung’uniko kwa baadhi ya mawaziri wengine ambao waliona kama Wasira anapewa “promo” kubwa japokuwa taarifa ya chanzo kimoja cha Ikulu inasema; “mzee (yaani Kikwete) anamuamini sana Mzee wa Wasira na ni mshauri wake mkuu, ndiyo maana alipewa umuhimu mkubwa kwenye ujio wa Obama.”
Jambo jingine linaloweza kumvusha ni kuwa mmoja wa viongozi wasio na kashfa za wizi wa fedha za umma. Kama ndivyo basi unaweza kusema kuwa uadilifu wake nao siyo wa kutiliwa shaka. Hata dhoruba zote ambazo zimeikumba Serikali ya Kikwete tangu mwaka 2005 na kila mara akibadilisha mawaziri na manaibu wao, Wasira ameendelea kuwa na namba ya kudumu. Moja ya vitu vinavyombeba ni uaminifu na kujua kazi yake. Hili nalo linaweza kuifanya CCM ihitaji mtu wa namna yake. Japokuwa, tuhuma za kutoa rushwa Bunda mwaka 1995, haziwezi kufutika.

Nini kinaweza kumwangusha?
Mambo kama matatu hivi yanaweza kumwangusha Wasira.
La kwanza ni dhana ya ukigeugeu. Mwaka 1995 aliposhindwa kura ya maoni ndani ya CCM kule Bunda, alihamia NCCR na kushinda ubunge. Kwa hivyo, yeye ni mmoja wa wana CCM waliowahi kukihama chama hicho kabla hawajarejea tena baadaye. Katika rekodi ya marais walioongoza nchi hii kupitia CCM, hapakuwahi kuwa na mmoja ambaye aliwahi kuhama chama chake na baadaye akarejea kisha akapewa nafasi ya kugombea urais. Kuna baadhi ya wana CCM wahafidhina wanamtizama kama mtu anayeweza kufanya uamuzi wowote ilimradi aendelee kuwa kiongozi. Kwa sababu ya kasumba hii, Wasira anaweza kujengewa hoja ya uimara wake wa kudumu ndani ya CCM kisha akaondolewa.
Lakini pili, Wasira si mtu mwenye nguvu ya pesa. Kwa wanaomfahamu wanalijua hili. Nimeshaeleza kuwa hadi sasa hana mitandao ya kifedha inayomuunga mkono na ili upite na kugombea urais kwa CCM ya sasa unahitaji kuwa na fedha za kutosha, hakuna maajabu mengine. Sioni kama Wasira ana ubavu wa kuvuka kizingiti hiki ili walau awe mmoja wa wagombea wenye nguvu na watakaoonekana kwenye mchujo wa mwisho.
Umri mkubwa ni jambo jingine muhimu. Tanzania haikuwahi kuwa na Rais ambaye anamaliza miaka yake 10 akiwa na miaka 80. Ikiwa CCM itampitisha ndiyo itakuwa mara ya kwanza tunaongozwa na mtu ambaye anamaliza akiwa kikongwe kabisa, nadhani haitakuwa tayari kwa hilo. Kwa changamoto za nchi hii ambazo zinahitaji watu wenye nguvu, ubongo unaofikiri sawasawa, wanaoweza kujisomea na kutafakari kila jambo – nadhani Wasira pia anaweza kuangushwa na kipengele hiki.

Asipopitishwa (Mpango B)
Tayari Wasira anaonekana kuwa ana mpango thabiti mkononi ikiwa hatagombea urais, mpango wake ni kurejea Bunda na kugombea ubunge kwani amekuwa mkali mno kila washindani wake (Esther Bulaya kutoka CCM, Dk Lucas Webiro na makada wengine kadhaa kutoka Chadema), wanapoonyesha kufanya harakati jimboni humo na hasa wanapoonyesha kuwa hajafanya jambo kubwa kwa watu wa Bunda. Lakini kwa sababu yeye ni mjasiriamali, namuona pia akiwa na chaguo la kurudi kufanya biashara na kupumzika majukumu na mikikimikiki ya umma na au kuendelea kuishauri Serikali na kuhamasisha maendeleo mkoani Mara, akiwa mtu aliyekaa serikalini muda mrefu.

Hitimisho
Ukweli ni kuwa, nafasi ya Wasira katika uwanja wa kisiasa za kitaifa na hata ndani ya Jimbo la Bunda kwenyewe ni ndogo sana. Kama hatasoma alama za nyakati hata ndani ya jimbo nadhani vijana watamuadhiri aidha, ndani ya kura za maoni za CCM au ataangushwa na mgombea kijana wa Ukawa ikiwa bado CCM itampitisha.
Katika safari hii ya urais simuoni akifika mbali lakini lolote linaweza kutokea. Jambo la msingi ni kuwa, namtakia kila lililo jema katika kufikia malengo aliyojipangia.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment